Ya Dk. Salim: Namuelewa Mzee Warioba, lakini….  

Picha: Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere akiwa na Dk. Salim

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

KWENYE tukio la uzinduzi wa Makavazi ya Dk. Salim Ahmed Salim jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Profesa Said Yahya Othman aliuliza swali gumu kwa wazungumzaji watatu katika tukio lile; kuhusu ubaguzi ulio wazi katika siasa za Tanzania.

 

Kama mwanazuoni, Profesa Saida alizungumzia kuhusu rangi. Akasema inaonekana katika Tanzania kuna rangi zinafutika na kusahaulika lakini kuna rangi moja haifutiki – nyekundu, inayohusishwa na kilichokuwa kikifahamika kama Chama cha Hizbu.

 

Dk. Salim aliwahi kuwa mwanachama wa Hizbu zaidi ya miaka 60 iliyopita. Uhusiano wake na chama hicho umekuwa ukitumiwa kama fimbo dhidi yake kila alipotaka kuwania nafasi ya juu ya uongozi hapa nchini.

 

Sidhani kama miongoni mwa wazungumzaji; Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, waziri mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amina Salum Ally na mwanadiplomasia mstaafu, Balozi Christopher Liundi, walitaraji Saida angeuliza swali lile.

 

Jaji Warioba aliyetakiwa kujibu wa kwanza, hakufanya jitihada zozote za kujibu swali lile. Alilikwepa kwa kuzungumzia mambo mengine yanayohusu namna alivyomfahamu Salim bila kujibu swali. Balozi Liundi naye alicheza mchezo huo wa Warioba.

Ni Balozi Amina pekee ambaye walau alijielekeza kujibu swali hilo na alipigiwa makofi ukumbini. Yeye alisema Salim aliamini kwamba siasa chafu huachia wanaozifanya makovu ya kudumu. Kwamba wabaguzi, mwisho wa siku, ndiyo wanaoumia zaidi, kuliko wanaotendewa.

 

Sikufurahishwa na majibu ya Warioba ingawa nilielewa kwa nini alifanya alichofanya. Aina ya siasa tunazofanya Tanzania ni siasa za kuepuka kujibu maswali magumu. Na kama mwana sayansi ya siasa, naamini hili huenda ni sehemu ya saikolojia ya kimaisha kwenye maisha ya watu weusi wa Afrika.

 

Mijadala mizito na yenye kufikirisha huwa haipendelewi kujadiliwa. Kimsingi, wale ambao hupenda kuibua na kujadili mambo ya namna hiyo, huonekana kama watu wasiofiti kwenye jamii zetu. Ni kawaida kuona kuna tatizo, liko pale linaonekana, lakini hakuna mtu anayetaka kulizungumzia.

 

Sababu zinaweza kutolewa nyingi. Unaweza kuambiwa kwamba jambo hilo ni mwiko na halijadiliwi, ni kinyume cha maadili ya kabila, jamii au taifa husika na wakati mwingine utaambiwa wakati wa kuzungumzia hilo haujafika.

 

Jaji Warioba na Liundi wanatoka katika jamii yetu hii yenye imani za namna hiyo. Kwa sababu hiyo, naelewa kwa nini walifanya walivyofanya. Lakini, naamini kwa kufanya kwao vile, wamepoteza fursa ya kuweka hadharani mjadala ambao ungekuwa na faida kubwa zaidi kwa taifa letu.

 

Pengine kuliko mwanasiasa mwingine yeyote mashuhuri wa Tanzania, Salim amekinywea kikombe cha siasa za kibaguzi za Tanzania. Yeye ndiye mwanasiasa pekee wa Tanzania ambaye anaweza kusema rangi yake ilimnyima nafasi ya kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu ya siasa za kibaguzi zilizofanywa dhidi yake.

 

Mwaka 1985 ilipokuwa ikifahamika hadharani kuwa yeye ndiye alikuwa chaguo la Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kuwa Rais wa Tanzania, kuliibuka kabisa makundi ya wanasiasa waliopinga kwa kumhusisha kwake na Hizbu. Hakuwahi kuhusishwa nayo kwenye majukumu mengine yoyote aliyoyafanya kwa Tanzania isipokuwa pale tu alipotaka urais!

 

Alipoamua kuwania tena urais wa Tanzania miaka 20 baadaye, mwaka 2005, ubaguzi dhidi yake haukuishia kwenye chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee, bali ulienda hadi katika vyombo vya habari.

 

Mwaka 1985 nilikuwa sijaanza hata shule ya msingi na sikujua chochote kinachoendelea. Yaliyotokea mwaka 2005 yalinikuta nikiwa mwandishi tayari na angalau nilishuhudia kilichotokea. Hadi leo, baadhi yetu katika tasnia ya habari tunaona kilichotokea wakati ule kilikuwa wakati mbaya zaidi kwa vyombo vyetu na uandishi.

 

Ninaamini kwamba wazo la Salim kwenye kuweka kumbukumbu zake hadharani kupitia makavazi yake si kukaa kimya. Naamini anataka tuzungumze mambo haya na ikiwezekana yakemewe yasiwakute wengine.

 

Ukiniuliza mimi, uzinduzi ule wa makavazi ulikuwa ni mahali sahihi pa kufanya Mea Culpa kwa kizazi cha wanasiasa kilichoshuhudia ubaguzi wa wazi kwa Salim na watu wa aina yake ukitokea. Hakuna mtu anayeweza kusema Jaji Warioba ni miongoni mwa walioshiriki kwenye ubaguzi dhidi ya Salim na kwa sababu hiyo alikuwa na haki zote za kusema kuna makosa yalifanyika na hayatakiwi kurudiwa.

 

Kukaa kimya kunaweza kusaidia kuondoa fukuto au kuahirisha tatizo lakini hakusaidii kuondoa tatizo. Kinachotakiwa ni kuzama kwenye tatizo na kusema “tulikosea wakati ule na tunaendelea kukosea”.

 

Vinginevyo, miaka 20 au 30 ijayo, tutakaa tena chini na kujadiliana kuhusu mabaya aliyofanyiwa mtu kutokana na rangi, kabila au hali yake ya uchumi. Ubaya wa dhambi ya ubaguzi, kama alivyopata kuasa Baba wa Taifa miaka mingi nyuma, ni kwamba ukianza huwezi kuacha. Ni sawa na mtu aliyeamua kula nyama za watu.

 

Kwa hakika kabisa, kama taifa, tunapaswa kuzungumza kwa uwazi kabisa kuhusu ubaguzi na mambo yote yanayotweza utu wa wenzetu. Tunaweza kuamua kukaa kimya, lakini tutakuwa sawa tu na ule mkasa wa mbuni kuficha kichwa kwenye mchanga.