Na Ahmed Rajab
HUU ni wakati muhimu na mgumu kwa Kenya. Taifa hilo linawaka moto na siasa zake zimefikia patamu. Rais William Ruto ambaye wiki chache tu zilizopita alionekana kuwa imara hivi sasa ni wazi kwamba amedhoofika. Wapinzani wake waliomiminika barabarani wamelivua guo la woga na wamekuwa na ujasiri wa kutamka wazi kwamba lazima aondoke madarakani.
Kuna hoja ya maana kwa nini Ruto anapaswa ajiuzulu na aitishe uchaguzi mkuu mwingine. Ruto amejitia kitanzi kwa kuukataa muswada wake wa Fedha uliokuwa na lengo la kupandisha kodi. Pamoja na kuukataa muswada huo, polisi wake wanatuhumiwa kuwaua waandamanaji chungu nzima.
Historia inatufunza mengi. Wito kama huo wa kumtaka Ruto ang’oke madarakani tuliusikia Misri wakati wa enzi ya Rais Hosni Mubarak na pia Sudan wakati wa Rais Omar Hassan al Bashir. Kabla ya hapo kilio kama hicho kilisikika Tunisia ilipokuwa chini ya Rais Zein el-Abidin Ben Ali.
Kilio hicho sasa kimelivuka jangwa la Sahara na kinagonga lango la Ruto. Jee, atang’oka madarakani au atasalimika?
Harakati za barabarani zikiendelea majeshi ya Kenya yamekaa chonjo. Kwa sasa, wakuu wa majeshi wamesimama kidete na Ruto. Lakini kuna dalili kwamba baadhi ya wanajeshi wa ngazi za chini wana huruma na waandamanaji.
Katika hali kama hizi, kuna uwezekano wa wanajeshi wa aina hiyo kuamua kuwaunga mkono moja kwa moja waandamanaji. Kadhalika, katika hali kama hizi akili za viongozi wa juu wa majeshi huwa hazitabiriki. Wakiona kama madaraka yanamponyoka Rais, akili zao huwashawishi waingilie kati na wampige kisugudi Rais ili wamuondoe madarakani.
Halafu kuna ile iitwayo Jumuiya ya Kimataifa, ambayo kwa uhalisia ni Marekani na washirika wake, pamoja na taasisi zao kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Mataifa (IMF).
Mataifa ya Magharibi na taasisi zao za kifedha ndio hasa waliomponza Ruto kwa msisitizo wao kwamba lazima apandishe kodi ili kupata fedha za kulilipa deni la serikali linalofikia dola za Marekani bilioni 2.7.
Mambo yalipochacha mataifa hayo, taasisi zao pamoja na hata baadhi ya asasi za kiraia za Kenya zenye kufadhiliwa na nchi za Magharibi zilimshauri Ruto aunde serikali ya mseto ili aliokoe jahazi lake. Mataifa ya Magharibi, na vishawishi vyao, yakafanya yaliyozea kufanya. Yalimshawishi kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga, ampe mkono Ruto na washirikiane kuitawala Kenya.
Raila amebobea katika siasa za kupeana mikono. Lakini mara zote siasa hizo hazikumfikisha mbali. Safari hii waandamanaji walimkumbusha kwamba hapo zamani alimsaidia Rais Daniel arap Moi kubakia madarakani, alimsaidia pia Rais Mwai Kibaki na mwisho Rais Uhuru Kenyatta.
Waandamanaji wakamwambia wazi Raila kwamba wamechoka kuchezewa naye. Walimwambia kinagaubaga kwamba akishirikiana na Ruto naye pia atakuwa adui.
Raila hakuwa na hila ila kuja matao ya chini na akalitupilia mbali wazo la kushirikiana na Ruto. Alifanya hivyo shingo upande kwa sababu anamhitaji Ruto amuunge mkono katika juhudi zake za kutaka awe mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Raila anayataka ya AU na pia ya Kenya. Ya Kenya yamemponyoka na huenda ya AU pia yakambwaga chini hata kama Ruto ataendelea kumuunga mkono. Sababu ni kwamba kuna wengi katika duru za kisiasa za bara la Afrika wenye kumpinga asiwe mwenyekiti wa AU. Hoja yao kubwa ni kwamba Afrika ni bara la vijana na linahitaji kuongozwa na vijana na si na wazee wa rika lake Raila.
Lazima yanayojiri Kenya yamevifanya vyombo vya usalama na vya kijasusi katika nchi jirani za Afrika Mashariki vizidi kutafakari juu ya mustakbali wa mifumo yao ya kiutawala pamoja na watawala wao.
Mvuvumko huo wa kizalendo ulioanzishwa na kuongozwa na vijana umewaumbua wanasiasa, hasa wakongwe. Haukuzuka tu ghafla bin vu bali umekuwa ukifukuta kwa miaka na ukipaliliwa na manung’uniko ya wananchi kuhusu makali ya maisha kwa Wakenya walio wengi wakati wenzao wachache, pamoja na wanasiasa wa mirengo yote, wakiwa wanaishi maisha ya kifahari.
Walioanzisha mvuvumko huu wa sasa ni vijana wa kizazi cha leo, kile kiitwacho kizazi cha Z, “Generation Z” kwa kimombo (au Gen Z, kwa ufupi).
Kwa wenye macho na wenye masikio sasa ni wazi kwamba mpambano ulio Kenya ni mpambano wa kitabaka lakini ni mpambano wa kitabaka ulio tafauti na ule asilia, yaani ule wa baina ya matabaka ya kijamii.
Mpambano wa sasa wa kitabaka ni wa baina ya tabaka la wanasiasa likikabiliwa na tabaka la vijana.
Wanasiasa wa sampuli zote, wa itikadi na mirengo yote, wamejikuta katika kapu moja. Hawauziki tena kwa wananchi. Tabaka hili la wanasiasa limetingishwa na mvuvumko wa vijana.
Na hao vijana nao wamejikuta katika kapu moja ijapokuwa wametoka katika matabaka tofauti ya kimaisha na kutoka makabila mbalimbali. Vijana wamekuwa wakisisitiza kwamba wao hawana kabila, hawana woga na hawana chama.
Wengi wa vijana hawa hawana ajira licha ya kwamba baadhi yao wamesoma na kuhitimu katika vyuo mbali mbali. Hata wale waliobahatika kupata kazi za vibarua wana vyeti vya vyuo. Baadhi yao wanaendesha bodaboda. Ndio maana nadhani wanazungumza lugha moja na vijana wa familia zenye kujiweza ambao nao wamejikuta hawana mbele hawana nyuma wakiwa wanateswa na gharama za maisha.
La muhimu kukumbukwa ni kwama vijana hawa ndio waliochomoza kuwa wapinzani halisi. Wamejikuta wakipaza sauti zao kwa pamoja, wakiwa na madai mamoja.
La kusikitisha katika sakala lote hili ni taswira inayojitokeza Kenya kwamba Ruto anairudisha nchi katika mfumo wa kidikteta, utekwaji wa wakosoaji wake, mauaji na mateso wanayofanyiwa wapinzani. Ni kana kwamba Ruto anajivisha ngozi ya Rais wa zamani Moi na uMoi umerudi kuitamalaki nchi.
Wakati wa Moi tulishuhudia maelfu ya Wakenya wakisozwa jela bila hatia, baadhi yao wakiteswa na wengine wakiuawa. Jengine la kujikumbusha na kulitafakari ni kwamba Ruto ni mtoto wa kisiasa wa Moi.
Juu ya yote hayo, kuna wenye kuhoji kwamba Ruto anaonewa, kwamba aliyoyafanya katika kipindi cha miezi 18 ni mengi zaidi na yenye manufaa makubwa kwa Kenya kushinda aliyoyafanya Uhuru Kenyatta katika muda wa miaka 10 ya utawala wake.
Wanachoshuku wenye hoja hiyo ni kwamba ingawa malalamiko na manung’uniko dhidi ya Ruto ni halali lakini yamezidi kupaliliwa makaa ya moto na hisia za kikabila za Wakikuyu. Kuingiza ukabila katika uchambuzi wa siasa za nchi kama ya Kenya ni jambo la hatari kwa sababu kufanya hivyo kunawafanya watu wasizingatie sababu halisi za kimsingi zinazoifanya Kenya itokote chini ya Ruto.
Ukweli wa mambo ni kwamba Kenya ikiwa chini ya Ruto au Rais ye yote mwengine itaendelea kutokota madhali viongozi wake wanajiachia wawe vibaraka wa madola ya Magharibi wakifuata amri zao na sera zao.
Mvuvumko huu unaoshika kasi Kenya na harakati zake umo katika hali ya kimazingira iliyo tafauti na zile za zamani. Hivi sasa kumezidi ukosefu wa haki na uadilifu katika jamii — ubadhirifu wa watawala umekithiri katika wakati ambapo wananchi wengi hawana ajira, hawana hohe hawana hahe.
Kwa mara nyingine tena, Wakenya wametuonesha jinsi walivyokomaa katika harakati za ukombozi. Vijana wao wanajijua walipo ingawa bado sidhani kama wanakujua waendako. Na nafikiri wenyewe wanalitambua hilo.
Ili kujua waendako wanahitaji wawe na dira ya muono wao. Ili waweze kufanya mapinduzi ya kweli ni muhimu wawe na mwongozo, itikadi itayoendesha sera zao na uongozi unaotambulika. La sivyo, mvuvumko wao utageuka povu na hautowafikisha mbali.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.