Babu Duni na binti yangu: Somo la Unyenyekevu  

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

SIKU moja majira ya saa tano usiku, nilipokea simu kutoka kwa mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar, Juma Duni Haji. Alikuwa ananipigia kwa vile hakupokea wakati alipopigiwa simu kutoka kwangu saa kadhaa nyuma.

 

Nilipoiona tu nilitabasamu maana nilijua kilichotokea. Sikuwa nimempigia mimi isipokuwa binti yangu mwenye umri wa miaka mitatu wakati huo. Kwa sababu ya namna simu yangu nilivyohifadhi majina, jina la Babu Duni lilikuwa miongoni mwa majina ya mwanzo na sijajua kwa nini ilikuwa binti akipiga inapigwa kwa waziri huyo wa zamani.

 

Siku hiyo akaniambia kwa utani tu; “Najua leo kapiga simu mchumba wangu, nimepiga kumsalimia tu”. Nikamwambia ni ukweli na tukabaki kucheka tu. Na mara nyingine, Duni alinipigia kuniuliza tu binti yangu anaendeleaje.

 

Huyu ndiye Juma Haji Duni niliyekuja kumfahamu katika miaka yake ya mwisho kwenye siasa. Fikiria pengine mwanasiasa maarufu zaidi wa upinzani Zanzibar hivi sasa, apigiwe simu na mtoto zaidi ya mara tatu kwa usumbufu na badala ya kukasirika au kufoka, atafute namna ya kunipooza kwa kuniambia eti ‘’Labda mchumba alikuwa amem –‘miss’.

 

Hii ni ishara ya unyenyekevu ambayo huwezi kuihusisha moja kwa moja na watu wengi ambao wamewahi kuwa viongozi – achilia mbali uongozi wa ngazi za juu wa aina ya Mzee Duni.

 

Nadhani nilianza kulisikia jina la Duni wakati nilipoanza kujua kusoma na kuandika mwanzoni mwa miaka ya 1990. Watu wa kizazi changu, tulikua kwa kusikiliza zaidi redio na kusoma magazeti. Televisheni zilikuja baadaye na maarifa ya kusoma vitabu pia hayakuwa jambo la kusisitizwa kama ilivyo sasa.

 

Nilisoma habari zake wakati nikiwa mwanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari. Lakini kumwona mara ya kwanza uso kwa uso ni baada ya kuingia kwenye uandishi wa habari na nadhani mara ya kwanza ilikuwa takribani miaka 20 iliyopita, kwenye mojawapo ya ziara za viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kwenye mikoa ya Kusini.

 

Akiwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, viongozi hawa wawili walinifungua sana macho kuhusu maisha ya wanasiasa – hasa wa upinzani nyakati zile. Kwanza walikuwa wakilala katika nyumba za wanachama wao kwenye maeneo walikofikia na pale walipolazimika kulala kwenye hoteli, walilala kwenye hoteli zilezile tulizolala waandishi na viongozi wengine.

 

Asubuhi tulikunywa chai pamoja. Na sote tulikula kitu hicho. Tofauti kubwa ya Lipumba wa wakati ule na Duni ilikuwa kwamba Mzanzibari huyu kutoka Unguja Kaskazini alikuwa akijulikana kwa kupiga vijembe na kuchomeka maneno ya kisiasa yaliyochekesha watu.

 

Lipumba alikuwa tofauti kidogo. Kabla ya yeye kupanda jukwaani, ilibidi viongozi wengine wawili; Richard Hizza Tambwe au Mazee Rajab – ambao sasa wametangulia mbele ya haki na Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema, wapande kwanza jukwaa ili kwanza kuweka wasifu wa profesa na kulainisha kidogo mambo.

 

Naamini Duni alikuwa mmoja wa wanasiasa walioshiriki kwenye kumjenga Lipumba. Baadaye, Lipumba alianza kuwa mahiri wa kuibua misemo kama ya “kifo cha mende” na mingine ambayo kwenye miaka yake ya awali kwenye siasa hakuwa nayo.

 

Lakini sijasahau kumwona mtu niliyekuwa namsoma na kumfahamu kama waziri wa zamani kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, akila kwa pamoja nami pasi na kujali tofauti zetu na wakati huohuo tukizungumza masuala ya kisiasa ya kitaifa na kimataifa.

 

Katika wiki ambayo Chama cha ACT Wazalendo kimeitumia kumuenzi Duni aliyepata kushika nyadhifa tofauti kwenye chama hicho, nimekumbuka pia unyenyekevu wake kwenye eneo ambalo watu wengi hawalizungumzi.

 

Huyu ni mwanasiasa aliyekubali kuachia kugombea uwakilishi au ubunge nyumbani kwao Zanzibar na kuja kuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kabla ya hapo, Duni alikuwa mara nyingi akitumika kama mgombea mwenza wa Lipumba kwenye uchaguzi wa urais Tanzania.

 

Moyoni mwangu naamini kwamba mara karibu zote Duni alikuwa anajua anawania nafasi ya uongozi ambayo ni ngumu kuipata. Kwa Unguja au Zanzibar kwa ujumla, Duni angeweza kugombea uwakilishi kwenye majimbo ya huko na kupata. Hilo lingempa cheo na riziki ya maisha ambayo ndiyo tamaa kubwa ya ubinadamu.

 

Kuna watu wanadhani sadaka ya namna hiyo ni rahisi kwa kila mwanasiasa. Ukweli ni kuwa hilo si jambo rahisi. Kwa tuliokuwa waandishi wa habari mwaka 2010, tunakumbuka namna aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, alivyoweka masharti ya chama chake kuendelea kumlipa mshahara wake wa ubunge ili akubali kuwania urais kupitia chama hicho wakati huo.

 

Kwenye hesabu zake, Slaa aliona kwamba kutakuwa na ugumu kwake kushinda urais. Lakini angewania ubunge wa Jimbo la Karatu, angeshinda na kuendelea kufaidi mshahara na marupurupu ya Bunge. Hakutaka kucheza ‘kamari’ na maisha yake na ilibidi CHADEMA ikubali kumlipa mshahara wake huo.

 

Kwa Duni, hali ilikuwa tofauti. Yeye hakuwahi kuomba chochote kutoka CUF ili akubali kuwa mgombea mwenza. Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha utiifu na unyenyekevu kwa chama chake cha kisiasa. Ni rahisi kufikiri na kufanya kama alivyofanya Slaa. Njia ya Duni ni ngumu kupita.

 

Fedha au vyeo havijawahi kuwa na thamani kubwa kwake kuliko utiifu na unyenyekevu kwa chama chake. Na hata hatua yake ya kukaa pembeni na kukiachia chama miongoni mwa wanasiasa wa kizazi cha vijana zaidi kilichopo sasa, ni alama nyingine ya tabia ya kipekee ya Juma Duni Haji.

 

Nilisikitika sana wakati fulani mwanzoni mwa mwaka huu wakati baadhi ya watu walipoanza kutumia ukosefu wake wa ukwasi kama fimbo ya kumchapia wakati chama chake kikianza mchakato wa uchaguzi.

 

Ni jambo la bahati mbaya kwamba siasa za Tanzania zina aina fulani ya unafiki wakati tunapozungumzia masuala ya maadili ya viongozi. Kila Mtanzania akiulizwa anataka kiongozi wa namna gani, mojawapo ya sifa za awali kabisa ni kutaka yule mwenye uadilifu usio na shaka na asiye mla rushwa.

 

Lakini, mwishoni mwa maisha ya kiuongozi au kisiasa ya mwadilifu huyo, utaanza kusikia maneno kuwa “ fulani alikuwa waziri au mkurugunzi mahali fulani kwa muda mrefu lakini kafa hajajenga hata nyumba”.

 

Mwanasiasa wa Tanzania ni kiongozi ambaye anatakiwa kuishi maisha ya aina mbili yanayotofautiana kama mchana na usiku. Kwa wakati mmoja aonekane masikini au mwadilifu lakini wakati huohuo awe na mali za kutosha ‘kusaidia wapiga kura’ au asionekane lofa.

 

Kwa Duni, pasi na shaka yoyote, mzani wake ulielekea kwenye uadilifu na utiifu kwa chama chake. Moyo wake na dhamira yale mara zote ilimwelekeza kwenye mapambano ya kupambania Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

 

Huko siku za usoni pengine kuna mtu atafanya utafiti na kuleta rejea ya uhakika lakini mpaka wakati ACT inatangaza rasmi kumuaga, ninaamini Duni ndiye mwanasiasa Mzanzibari aliyefika maeneo mengi zaidi ya Tanzania Bara kuliko mwingine yeyote tangu Uhuru.

 

Mara nyingi huwa tunawataka viongozi wetu waandike vitabu kueleza maisha yao lakini kwa Duni, naamini maisha yake pekee yalikuwa kitabu tosha kwa wale wanaotamani au kufikiria kuwa wanasiasa kwenye miaka ijayo.

 

Panapo majaliwa, nimepanga kwenda kumsalimu Babu Duni nyumbani kwake Unguja nikiwa na binti yangu kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka huu. Na kama siku moja atataka kuwa mwanasiasa, nitamweleza kuwa kama akipenda, anaweza kufuata nyayo za Juma Duni Haji.