Miaka 10 ijayo ya ACT Wazalendo

Na Ezekiel Kamwaga

 

WIKI iliyopita, chama cha siasa cha ACT Wazalendo kilitimiza miaka tisa kamili tangu kuanzishwa kwake mnamo Mei mwaka 2014. Ingawa katika muda huo kimepita katika misukosuko mingi, naamini kwamba miaka 10 inayokuja itakuwa muhimu zaidi kwake.

 

Kama ilivyo kwa viumbe hai vingi, chama cha siasa kina maisha ya aina tatu – ya awali wakati kingali kinategemea wazazi na mazingira kuishi, maisha ya kujitegemea na hatua ya tatu ni ile ya ama kufikia malengo au kufa. Kama chama kitavuka hatua ya awali kikiwa salama, uwezo wa kudumu katika hatua ya pili kama chama tawala au cha upinzani unahitaji sifa tofauti kabisa na za hatua ya awali.

 

Miaka tisa ya kwanza ya ACT Wazalendo ilikuwa ni miaka ya awali. Wakati chama hiki kinaanza, sikuwa na matumaini kama kingeweza kudumu hadi leo. Kilizaliwa katika wakati ambapo siasa za Tanzania zilianza kuonekana kama za vyama viwili – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuondoa upande wa Zanzibar ambako CCM ilikuwa inashindana zaidi na Chama cha Wananchi (CUF).

 

Ni wazi kwamba ACT Wazalendo – hasa baada ya matukio ya mwaka 2019 ambapo vigogo wa CUF Zanzibar walijiunga nacho, kimeingia katika hatua yake ya pili. Na hata kama bado Chadema na CCM vinabaki kuwa vyama vikubwa zaidi nchini Tanzania, ile dhana ya siasa ya vyama viwili inaondoka taratibu kwa sababu ACT imeanza kujichomoza kama chama cha tatu.

 

Makala hii inajaribu kuangalia ni kwa namna gani ACT inatakiwa kuenenda katika kipindi cha miaka 10 ijayo ili iwe na nafasi ya kuingia madarakani – kama mazingira mengine yote yatabaki kama yalivyo, na kisijifie kama ambavyo vyama vingine vilivyowahi kutamba hapa Tanzania vimepita kwenye njia hiyo. Ninajibu swali la ACT kinatakiwa kufanya nini ili kikue zaidi?

 

Unyumbufu kwenye miungano ya kisiasa

 

Kwa sasa, ACT ni chama cha tatu kwa ukubwa hapa nchini. Si chama cha kwanza wala cha pili. Ninapofanya uchambuzi wa aina yoyote unaohusu vyama vya siasa, mara nyingi hurejea katika maandishi ya Giovanni Sartori kwenye kitabu chake maarufu cha Parties and Party Systems. Ni maoni yangu kwamba kitabu hicho na kile cha mwaka 1951 cha Maurice Duverger cha Les Partis Politiques, pengine ndivyo vitabu muhimu zaidi kuandikwa kuhusu vyama vya siasa.

 

Maandishi ya Sartori yanatoa ushauri mmoja kwa chama aina ya ACT Wazalendo kwa sasa. Kwamba namna bora zaidi ya kuendelea kukua kwake ni kuishi na kujionyesha kama chama kilicho tayari kuingia kwenye muungano na vyama vingine. Kwa kadri vyama vingine vinapokiona kama aina ya chama wanachoweza kufanya nacho kazi pamoja, ndiyo fursa ya kuongezeka kwa ushawishi wa chama hicho inavyoweza kukua.

 

Mifano ya hili iko mingi. Chukulia mfano wa jirani zetu nchini Kenya. Wakati Raila Odinga alipoamua kufanya kazi na TANU kupitia kilichokuwa chama chake cha NLD, chama chake kilikuwa cha tatu au nne kwa ushawishi nchini Kenya. Ni baada ya mpasuko wa TANU wakati yeye akiwa ndani yake, ndiyo uliompa nguvu zaidi baada ya kupata marafiki wa chama tawala cha KANU akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Joseph Kamotho. Leo hii, Raila Odinga ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kuzidi mwingine yeyote nchini humo.

 

Mfano mwingine unahusu ACT yenyewe. Kabla ya vigogo wa CUF wakiongozwa na watu kama hayati Maalim Seif Shariff Hamad na Nassor Mazrui kuhamia kwao katika tukio lile la “Shusha Tanga, Pandisha Tanga”, ACT haikuwa na ukubwa ilionao leo. Kuna kitu kiliwafanya waliokuwa viongozi wa CUF kujiunga na ACT badala ya chama kingine. Kama CUF waliona hivyo, CCM na Chadema nao wanapaswa kuiona ACT kama chama pekee wanachoweza kuingia nacho kwenye ushirikiano.

 

ACT ni muhimu kiwe wazi katika mazungumzo yoyote ya ushirikiano wa kisiasa ili mradi lengo lao la kuingia madarakani litimie. Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa, anaamini kwamba lengo muhimu zaidi la kuanzisha chama cha siasa ni kushika hatamu za dola na kama kuna ushirikiano wa aina yoyote unaoweza kuipa ACT dola, ACT inatakiwa kuukumbatia.

 

Nidhamu kwenye chama

 

Hakuna kitu muhimu kwenye taasisi yoyote kama suala la nidhamu. Ninaposema nidhamu kwenye chama simaanishi nidhamu ya kuamkia wakubwa. Nazungumzia nidhamu kwenye kubaki kwenye ajenda kuu ya kuanzishwa kwa chama, nidhamu kwenye matumizi ya rasilimali za chama, nidhamu kwenye kuheshimu maamuzi yaliyofikiwa kwenye vikao na nidhamu kwenye ushirikishwaji wa wanachama kwenye masuala ya chama.

 

Katika kitabu cha Do Not Disturb, mwandishi Michela Wrong alitoa mfano wa kusisimua kuhusu tofauti ya nidhamu baina ya majeshi ya Uganda na Rwanda wakati wa vita ya DRC kwenye miaka ya 1990. Mwandishi huyo wa habari alikwenda kwenye kambi ya Uganda akakuta Mkuu wa Vikosi anakunywa pombe aina ya Whisky asubuhi wakati alipokwenda kwa mwenzake wa Rwanda, alimkuta anakunywa maziwa. Uganda walipigwa na Rwanda.

 

Hakuna kitu chama kinaweza kufanikisha katika maisha yake kama hakiwezi kuwa na nidhamu. Na nidhamu haitoki kwa wanachama au wafuasi wa ngazi za chini kwenda kwa viongozi. Inakata kote kuwili. Kuanzia kwa viongozi kwenda chini na kinyume chake. Inahusu nidhamu kwenye namna ya kuwasiliana na umma na kwenye uwasilishaji wa hoja. Watu wanapenda kujihusisha na taasisi zenye nidhamu.

 

Masuala ya Watu

 

Katika andishi lake la mwaka 1996 kuhusu Democracy and Multi-Party Politics in Africa, Profesa Samuel M. Makinda aliandika kwamba kile kinachoonekana kama Waafrika kukosa mshawasha na siasa au masuala ya uwajibikaji kinatokana na kuwa na matatizo mengi yanayowafanya wasiwe na muda kwa masuala yasiyotibu kero zao.

 

Aliandika Profesa Makinda; “Baada ya sera za kupunguza wafanyakazi na ubinafsishaji zilizoletwa na taasisi za Bretton Woods, watu wengi walipoteza ajira na vipato vya uhakika. Hili limeleta tatizo kubwa la ajira miongoni mwa vijana. Nchi nyingi za Afrika pia hazina mifumo ya hifadhi ya jamii inayohudumia watu walio nje ya ajira. Badala ya kuhangaika na siasa, watu wanapambania maisha yao”.

 

Ni vizuri kwamba ACT Wazalendo ndicho chama pekee ambacho kimezungumza kwa upana masuala ya hifadhi ya jamii. Hili ni eneo moja. Lakini inatakiwa huo ndiyo uwe utaratibu wa kudumu wa chama hicho kwenye kuzungumzia kero halisi zinazogusa maisha ya walio wengi na kutoa suluhisho. Siasa ni watu. Siasa ni masuala ya watu.

 

Rasilimali Fedha

 

Tafiti mbalimbali zilizofanywa katika nchi za Magharibi na Afrika zimeonyesha kwamba vyama vilivyofanikiwa katika chaguzi ni vyama vilivyojijengea uwezo mkubwa kifedha. Kama ACT hakitakuwa na namna yake ya kutengeneza fedha, haitaweza kufanikisha ndoto zake za kukamata dola.

 

Siasa za Kenya zimechangamka kwa sababu vyama vya upinzani vina watu wenye ukwasi. Upinzani ulikaribia kutwaa dola nchini Tanzania kwa sababu – kwa mara ya kwanza, upinzani ulikuwa na uwezo wa kifedha kufanya kampeni za kisasa na zilizofika katika maeneo yote.

 

Vyama vya upinzani vinahitaji kuwa na siasa safi. Vinahitaji kusambaza siasa yao katika maeneo ya mbali. Siamini kama ACT inafanya inayofanya sasa kwa sababu ya ruzuku kiduchu inayopatikana. Siwaoni matajiri – wa aina ya marehemu Philemon Ndesamburo alipokuwa Chadema, wanaojulikana waziwazi kwa kusaidia chama hicho kufanya shughuli zake.

 

ACT wanaweza kuendelea kuchangisha kupitia malipo ya kadi za wanachama. Inaweza kutengeneza Idara rasmi ya masuala ya uchumi itakayobungua bongo za chama kuhusu miradi inayoweza kukiingizia chama fedha. Kama ACT ikianza kuonekana kutoa ajira kwa vijana kingali chama cha upinzani, kinaweza kuaminisha umma kuwa kitatoa ajira kikiwa Ikulu.

 

Lakini, kama ulivyo msemo maarufu wa Kiswahili wa “hadhari, mti na macho”, ACT inapaswa kuwa makini na aina ya wachangiaji na michango inayopokea kutoka kwa watu tofauti. Kama hakitakuwa na nidhamu kwenye kupokea michango na misaada, kinaweza kujikuta kwenye uhusiano usio na afya na baadhi ya watu au vikundi maslahi.

 

Kivuli cha Zitto

 

Mwaka huu, Zitto Kabwe ataacha kuwa Kiongozi Mkuu wa chama hicho. Katika miaka tisa iliyopita, Zitto na ACT wamekuwa chanda na pete. Ni vigumu, walau kwa muda huu, kuiona ACT bila Zitto katika wadhifa huo. Hata hivyo, kama Zitto amemaliza muda wake uliowekwa kikatiba, ni muhimu akafuata kilichoandikwa.

 

Huu utakuwa wakati muhimu kwa ACT kujionyesha kama chama kinachoweza kwenda chenyewe pasi na mtu. Huu unaweza kuwa wakati ambapo sura nyingine inaweza kutawala siasa za chama hicho hata kama Kiongozi huyu wa sasa anaweza kupewa majukumu mengine. Tatizo kubwa la vyama vya siasa vya upinzani vya Tanzania – na kwa sehemu kubwa bara la Afrika, ni kwamba kuna shida ya kutofautisha baina ya chama na kiongozi wake. ACT si Zitto na Zitto si ACT. Huu ni mtihani ambao ACT Wazalendo itahitaji kuuvuka vizuri katika wakati huu ambako chama kitakwenda kuongozwa na mtu asiye Zitto.

 

Tunarudi tena kwenye suala la nidhamu. Itahitajika nidhamu kubwa kwenye kuamua nani atakuwa Kiongozi wa Chama baada ya Zitto. Chama kinahitaji kufanya uamuzi wa muhimu kwenye kuamua nani anaweza kuvaa viatu vya kiongozi huyo muhimu zaidi kwenye historia ya chama hicho.

 

Damu changa

 

Takwimu za masuala ya idadi ya watu zinaitaja Tanzania kama mojawapo ya mataifa yatakayokuwa na idadi kubwa ya watu katika siku zijazo. Takwimu pia zinaonyesha kwamba zaidi ya nusu ya Watanzania walio hai sasa wana umri chini ya miaka 30. Kuelekea miaka 10 ijayo, ni muhimu kwa ACT Wazalendo kujitanabaisha kama kimbilio la vijana.

 

Ni muhimu chama hicho kikawekeza sana kwenye kujua vijana wa Tanzania wanapenda kusikia nini, wanafuatilia nini na wanataka nini kwenye maisha yao. Chama kitakachochukua nafasi ya CCM huko tuendako kitakuwa chama kitakachokuwa na ufuasi mkubwa miongoni mwa kundi la vijana.

 

Tofauti kubwa ya siasa za nchi za magharibi na siasa za Afrika ni kwamba wenzetu waliunda vyama vyao kwa kuangalia matabaka ya watu (classes) na uwezo wa kuunganisha maslahi ya pamoja ya vikundi. Vyama vingi vya Afrika vinafanya siasa za kutaka kumpata kila mtu. Chama kitakachopiga hatua kubwa kisiasa katika miaka inayokuja ni kile kitakachokuwa cha kwanza kutambua kinafanya siasa kwa ajili ya nani na kundi lipi.

 

Kwa sababu kundi kubwa zaidi ni la vijana kwa sasa, chama chenye maarifa ni kile kitakachojua namna ya kuwasiliana, kuaminiana na kupatana na kundi hili. Hili ni jeshi moja kubwa linalosubiri mtu au chama wa kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi.

 

Mpira uko miguuni mwa ACT Wazalendo. Happy Birthday. 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ready to Mix

 

Disciplined

 

Pragmatic

 

Relevant

 

Resources

 

Youth Based