Kenya ya Ruto: Ndoto ya pepo kwa hustlers imetimia?

Picha: Rais William Ruto. Kwa Hisani ya BBC

 

 

Image

Na Paul Sewe

 

UCHAGUZI Mkuu wa Kenya uliofanyika mwaka jana ulimalizika kwa ushindi wa Rais William Ruto na aliyekuwa mgombea mwenza wake, Rigathi Gachagua. Sasa miezi tisa imepita tangu ushindi wao huo lakini bado kuna maswali kuhusu mwelekeo ambao serikali yao imeamua kuchukua.

 

Ni vigumu sana kupata mtu anayeitakia nchi yake maovu tu ila kuna nchi zinazochosha kuzitakia mema, maana yote wanayofanya wenye dhamana ya kuendesha nchi ni maovu tu. Duniani kote sasa hivi kuna changamoto za kiuchumi na taifa la Kenya halijapona kwenye changamoto hizo.

 

Kama mojawapo ya watu waliokuwa kwenye mstari wa mbele kabisa kwenye siasa za Kenya, ninaulinganisha msimu huo wa siasa na uchaguzi kwa ujumla wake na bahari chafu, ambapo mawimbi yanasomba na kuleta ufukweni aina yote ya uchafu; pamoja na vipande vya mbao, mimea, vifusi, miili ya wafu na kila kitu kilichomo baharini.

 

Nithibitishe ninayoyasema kama ifuatavyo; Siasa zina Kenya huwa zina msisimko mkali sana na ni kawaida, japo huu wa mwisho ulinishtua kidogo hasa pale ambapo upande mmoja ulijinadi kuwa wao ndiyo wacha mungu na wana upako fulani na upinzani ulikuwa na nguvu za giza. Siasa za aina hiyo hazistahili kuvumiliwa na mtu yeyote kwenye nchi yoyote ile.

 

Hata baada ya uchaguzi, kauli hizi zinaendelea na zinatia nchi hatarini maana nyufa zinazidi kutanuka kwenye jamii na taifa kwa ujumla. Uchumi wa nchi upo vibaya na kimsingi huwezi kurekebisha uchumi kawa propaganda kama alivyosema Mamadu Bawumia na hatua ya kwanza ya kurekebisha uchumi ni kurudisha imani kwa wawekezaji na pia kuhakikisha usalama wa watu na mali zao unadumishwa ambapo kwa sasa hali ni kinyume, japo maisha ya viongozi ni kana kwamba kila kitu kipo shwari.

 

 

Migawanyiko:

 

 

Wahenga wetu walituachia msemo mmoja maarufu wa aliyezoea kunyonga hawezi vya kuchinja na naweza pia kusema kwamba viongozi wenye tabia ya kugawa wananchi nao hawawezi tena kuwaunganisha kamwe. Walipoanza, walisema uchaguzi uliopita ulikuwa ni kati ya waumini na wasiomuamini Mungu yaani makafiri. Wakasema wao ni  hasla (hustler) na kwamba washindani wao walitoka katika koo za kifalme (dynasty) na sasa Muswada wa Fedha wa mwaka 2023 nao unasema waziwazi kuwa utakuwa ni waliojiriwa dhidi ya wasiojiriwa (Payslip holder vs Non pay slip holders). Hizi si kauli za kuunganisha bali za kusambaratisha taifa. Ni muhimu viongozi wakakoma kutumia kauli za kichochezi kama hizi hapa maana taifa ni moja na ni letu sote.

 

Kenya ipo pabaya kwa sababu mihimili ya Bunge na Mahakama inaelekea kutekwa na Serikali Kuu na hili ni hatari kwa demokrasia kwa ujumla. Ni wakati wa mihimili hii kujitathmini upya. Mbinu ya uhakika kabisa ya kuteka mtu au kitu ni kuahidi utawapa nafasi ya kukandamiza wengine.

 

 

Kwa maoni yangu, sifa kuu tano za kiongozi asiyefaa ni; kujinasibu, kuwadharau wanaokukosoa, kujiona wewe ndiyo mwamba wa miamba, kuzingirwa na wanaokumbatatia hata ujinga wako pasipo kukuambia ukweli na kuwadhalilisha viongozi wengine hadharani. Mwandishi maarufu, Fyodor Mikhailovich Dostoevsky, alishauri kwamba yote kwa yote tusiwe tunajidanganya wenyewe yaani “Above all else do not lie to yourself.”

 

Hatma ya nchi

 

Katika miezi hii tisa ya utawala wa Ruto, zimekuwepo tuhuma dhidi ya serikali zinazoonyesha upendeleao wa hali ya juu kwenye uteuzi anaofanya ambako inaonekana watu kutoka mahali anakotoka, ndiyo wanapewa nafasi zilizo nono. Kinachoonekana sasa ni kwamba sifa kubwa ya uteuzi sasa si weledi au uwezo wa kazi bali kabila anakotoka mhusika.

 

Sasa, pasi na shaka yoyote moyoni mwangu, naamini kuhusu umuhimu wa kuwabadilisha wanasiasa kwenye nafasi za uongozi sawa na namna tunavyobadilisha nepi za watoto wachanga maana wakiachwa muda mrefu sana wanazoea wananchi na kuingiwa na kiburi hata kwenye maandiko ya dini Mungu mara  nyingi anawapa adhabu watu wenye kiburi na taifa letu linaweza pia kupata pigo kwa viongozi kujawa kiburi na dharau.

 

Binafsi naweza kutamani Ruto na serikali yake wafanikiwe, ila napata ukakasi kusema maana hamna jitihada yoyote wanayofanya kuileta nchi pamoja na baraza lake la mawaziri limesheheni mabingwa wa uwezo hasi na wasiyojulikana kwa kufanikiwa kokote kwenye chochote cha maana.

 

 

Labda, nimewaonea lakini nina uhakika na ninachokisema kwamba wana uwezo mdogo na kwa hiyo kutegemea makubwa kwao naona kama ni dhambi. Tutawavumilia kadri itakavyowezekana, yaliyobaki atafanya Mungu kama itawezekana na cha mno ni kwamba kazi ipo na siyo kazi ndogo na waache kutishia mhimili wetu wa mwisho ambao ni vyombo vya habari.

 

 

Hitimisho 

 

Ingawa ni mapema kutoa hukumu sana, dalili zote zilizoko zinaashiria kwamba mbele kuna mawimbi ambayo watakaostahimili ndiyo watafika kwenye nchi ya ahadi. Mimi langu leo ni kuwaasa viongozi wa Kenya kutanguliza maslahi ya nchi na siyo ya kwao wao, maana nchi itaingingizwa kwenye machafuko pasipo sababu yoyote ya msingi. Wanaojua wanasema la kuvunda halina ubani. Mimi bado sijawalaani hawa kuwa la kuvunda ila tunakoelekea wengine uzalendo utatushinda, viongozi  waache lugha ya vitisho vya a majukwaa wajue kazi ipo na kazi yenyewe ni kujenga nchi yetu , taifa letu tukufu la Kenya – vitu pekee tukufu ni taifa  na wananchi wake, siyo kiongozi au viongozi ambao wapo leo , kesho hawapo tena.

 

 

Mwandishi ni Mchambuzi wa Masuala ya  Kisiasa na Kisheria.

Email: Sewepaul8@gmail.com