Tanzania Tower: Idan na Picha kubwa

Mwonekano wa majengo pacha ya Tanzania Tower mara yatakapokamilika

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MAPEMA mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje, January Makamba, alipokea simu kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Serikali ya Nigeria kuhusu suala la kiwanja ambacho Tanzania ilipewa katika eneo zuri la Lagos takribani miaka 34 iliyopita lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

 

 

January aliulizwa kama Tanzania bado inahitaji eneo lile au serikali ya Nigeria ilipangie matumizi mengine. Itoshe tu kusema kwamba mara baada ya mazungumzo yao, Nigeria ilikubali kuliacha jengo lile kwa matumizi ya Tanzania kama ilivyokuwa makubaliano ya awali.

 

 

Jambo hilo la Lagos si jambo la kipekee. Katika majengo 109 na viwanja 11 ambavyo Tanzania inamiliki duniani kote – vingine kwa kununua na vingine kwa kupewa kwa sababu za kirafiki na uhusiano mwema kidiplomasia, yako ambayo yana hali mbaya kiasi kwamba hata kinga yake ya kidiplomasia imeondolewa.

 

 

Uzinduzi wa ujenzi wa majengo pacha ya Tanzania Tower jijini Nairobi, Kenya ni sehemu ya mpango mkubwa ambao serikali imeuanza wa kuhakikisha inatumia kibiashara mali zake za miliki kwenye maeneo tofauti duniani kuingiza kipato. Lengo la mpango huo ni kubadili hali ya sasa ambapo serikali inatumia shilingi bilioni 29 kulipa kodi za pango kwa mwaka na badala yake kuingiza shilingi bilioni 36 kwa yenyewe kupangisha majengo yake.

 

 

Eneo la Upper Hill ambako majengo hayo yatajengwa, ni mojawapo ya maeneo mazuri na yenye hadhi kwenye jiji la Nairobi na serikali ya Kenya ilitoa ardhi hiyo kwa Tanzania zaidi ya miongo miwili iliyopita – kama ambavyo Tanzania ilitoa ardhi kwa Kenya kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Kenya Complex pale Bongoyo, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

 

 

Wakenya walitumia nafasi hiyo vizuri na sasa wamejenga jengo ambalo siyo tu linatumika kama Ofisi ya Ubalozi wa Kenya hapa nchini, lakini pia limekodishwa na Benki ya Kenya Commercial Bank na biashara nyingine ambazo zinaingiza kipato kwa taifa hilo. Sijui Wakenya walikuwa wanatuonaje lakini kutofanya kitu katika ardhi iliyo mkabala na ulipo Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya, lilikuwa ni jambo lisiloeleweka vema kwa wenzetu.

 

 

Ni vizuri kwamba serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, imeamua kujenga jengo hilo la Tanzania Tower – litakalokuwa na majengo mawili yenye urefu wa ghorofa 22 kila moja. Ilikuwa vema pia kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Deo Ndejembi, alisema ujenzi huo umefanyika baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu ulioonyesha kwamba jengo hilo litaleta faida kiuchumi.

 

 

Na ni rahisi kuona ni kwa nini Kenya imekuwa taifa la kwanza ambalo serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan – ambaye ni muhimu kusema amechukua uamuzi muhimu ambao pengine watangulizi wake hawakuweza kuuchukua, imeamua kuanza kutekeleza mkakati wake mpya wa matumizi ya kibiashara ya miliki zetu.

 

 

Jiji la Nairobi ndilo jiji kuu la kibiashara katika eneo la Afrika Mashariki, ndiyo makuu ya vyombo na taasisi nyingi za kimataifa vikiwemo vyombo vya habari na mashirika ya kimataifa, ndiyo kitovu cha kiuchumi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki na jiji lenye mahitaji makubwa ya kiofisi kuliko mengine kwenye eneo hili.

 

 

Lakini pia tayari Tanzania inaingia gharama kubwa kulipia mahali ziliko ofisi zake za ubalozi hivi sasa – kwenye ghorofa ya tisa ya jengo la Re Insurance, na kulipia wafanyakazi wa ubalozi wake wanaolazimika kupangisha nyumba. Tanzania Tower itaifanya Tanzania kuokoa gharama za makazi kwa ubalozi na watumishi wake.

 

 

Na kuna mambo mengine ambayo hayawezi kupimwa kwa kiwango cha fedha pekee. Nilitabasamu wakati Waziri Makamba alipomtania Waziri Mkuu wa Kenya, Musalia Mudavadi, kwamba ingawa imechelewa kujenga jengo lake, likikamilika, litakuwa kubwa zaidi na zuri zaidi kulinganisha na lile lililojengwa na Kenya nchini kwetu.

 

 

Kwa zaidi ya miongo minne, kumekuwa na ushindani wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Kenya kuhusu ni nani hasa anatakiwa kuonekana kama “Super Power” wa eneo hili baina ya majirani hao. Mojawapo ya mambo yanayoonyesha ukubwa wa nchi ni namna inavyojionyesha kwa majengo yake.

 

 

Sidhani kama kuna Mkenya angeipa Tanzania heshima kwa kuiona ikiwa imejibana kwenye kighorofa kimoja, huku ikiwa imepakana na maduka ya kutoa ‘fotokopi’ na kuuza nywele bandia na vifaa vya wanafunzi kutumia shuleni.

 

 

Yeyote atakayeliona jengo la Tanzania Tower wakati litakapokamilika, ataiona nchi yetu kwa jicho tofauti na lile la anayeuona ubalozi wetu sasa pale ‘tulipojibanza’ hivi sasa. Hili si jambo unaloweza kulipima kwa fedha.

 

 

Kuna sababu kwa nini mataifa makubwa hujenga balozi kubwa kote duniani. Mara zote, ukubwa hautakiwi kuwa jambo la kujificha. Ukubwa ni jambo linalotakiwa kuonekana, wakati mwingine kwa macho makavu.

 

 

Kiuchumi, unaona pia faida ya jengo hili kwa namna zaidi ya moja. Kwanza, kuna uwezekano wa eneo hili kugeuka kuwa kitovu cha biashara na makutano ya Watanzania nchini Kenya. Hakuna nchi ya Afrika inayofanya biashara na Tanzania kuliko majirani zetu hawa. Unaona Watanzania wote wanaofanya biashara zao kwa jirani zetu hao, wakihamia Tanzania Tower – kama ambavyo KCB wameenda kwa ubalozi wao hapa Dar es Salaam.

 

 

Pili ni faida ambayo NSSF itaweza sasa kupata baada ya kuanza kwa matumizi ya jengo hilo. Waziri Mkuu Mudavadi alizungumza kwa busara sana aliposema kwamba namna pekee ya kusaidia kuongeza mafao ya wafanyakazi ni kwa mifuko kuwekeza kwenye miradi itakayoongeza ukwasi wa mifuko kuliko kubaki na fedha zikiwa bwete.

 

 

Ni kweli kwamba mifuko yetu ya hifadhi mara nyingine imejikuta ikiingiza katika uwekezaji ambao faida zake hazionekani au inaonekana imekula hasara. Lakini, kwa kinga ya kufanya upembuzi yakinifu kabla ya kuingia kwenye miradi – kama alivyoagiza Rais Samia na kama walivyofanya NSSF kupitia mradi huu, unaona akiba ya wafanyakazi ikiwa inatumika vizuri na kuongeza kibaba chao.

 

 

Natarajia kuiona serikali ikiharakisha sasa na mpango wa ujenzi wa jengo lingine kubwa katika jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo(DRC) ambako tayari inafahamika gharama za kupangisha ni kubwa kuliko popote katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

 

 

Kwa uhitaji wa majengo ulioko Kinshasa hivi sasa, hakuna sababu ya kuchelewa kwenda kujenga katika taifa hilo kwa vile faida ya kimahesabu inafahamika na tayari maeneo ya kufanyia ujenzi yapo. Na mradi huo ukikamilika, Tanzania itakuwa taifa lenye majengo mazuri kabisa ya kidiplomasia kwenye eneo letu.

 

 

Uingereza na Ulaya

 

 

Hakuna mfano mzuri wa kuelewa hiki kinachofanywa na utawala wa Rais Samia kama kutazama hali yetu ilivyo kwenye ubalozi wetu wa London, Uingereza. Huu ni ubalozi ambao walau naufahamu vizuri kwa sababu nimeutembelea mara kadhaa wakati naishi nchini humo.

 

 

Ubalozi upo katika eneo la kibiashara zaidi katika jiji la London na kama litafanyiwa ukarabati unaotakiwa – niliambiwa wakati fulani, na kuanza pia kupangishwa kibiashara kwa watu wengine, mapato yake yanaweza kutumika kuendesha karibu balozi zetu nyingine zilizoko barani Ulaya ambazo hazizidi tisa.

 

 

Jambo pekee ambalo ningeshauri ni kwa serikali kutengeneza taasisi ambayo itafanya kazi ya usimamizi wa uwekezaji huu ambao unaenda kufanywa na Wizara ya Mambo ya Nje. Kazi ya wizara ni ya kisera zaidi na nina imani kutaundwa taasisi – au labda NHC wanaweza kupewa mamlaka ya kuwa wasimamizi wa miradi hii inayokwenda kutekelezwa na serikali.

 

 

Nina matumaini makubwa kwamba mara baada ya rafiki zetu wa Nigeria kusikia na kuona kinachoendelea Nairobi, simu itakayofuata kwa Waziri Makamba, neno lake la kwanza kwake litakuwa Idan (magic). Na kwa uhakika kabisa, najua iko siku Tanzania itakwenda Nigeria kutumia vizuri ardhi iliyopewa.