Nani atataka kuwa Katibu Mkuu wa CCM?

Picha: Daniel Godfrey Chongolo. Kwa hisani ya tovuti ya CCM.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

WIKI mbili zilizopita, mmoja wa rafiki zangu ambaye ni kiongozi serikalini, alikuja Dar es Salaam kikazi. Katika mazungumzo yetu tulipoonana, suala la kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, lilichukua sehemu kubwa ya mazungumzo yetu.

 

 

Ni sadfa kwamba mimi na rafiki yangu huyo tunafahamiana pia na Chongolo. Jambo moja aliloniambia na limebaki kwenye kumbukumbu zangu ni kuwa; “kwa sasa, sina sababu ya kukubali kuwa Katibu Mkuu wa CCM kama chama kitataka kuniteua kushika wadhifa huo”.

 

 

Kwa nini rafiki yangu huyo aliniambia maneno hayo? Ni kwa sababu katika mazungumzo yetu, tulijadili namna kuondoka kwa Chongolo kulivyofuatana na fedheha, hadaa na ukatili ambao haujawahi kuonekana katika historia ya chama hicho.

 

 

Chongolo si Katibu Mkuu wa kwanza wa CCM kuomba kuachia ngazi au kuondolewa katika wadhifa wangu. Katika miaka yangu 20 ambayo nimekuwa mwandishi wa habari, nimewashuhudia Philip Mangula, Yusuph Makamba, Wilson Mkama, Abdulrahman Kinana na Bashiru Ally wakiwa makatibu wakuu wa chama hicho na wakiondoka kwa sababu tofauti.

 

 

Hata hivyo, hakukuwa na kiwango cha sumu, hadaa na fedheha vilivyotokea kwa Chongolo. Imesadifu pia kwamba hata katika barua ya kujiuzulu iliyosambazwa katika vyombo vya habari, tuhuma zilizorushwa kupitia mitandao ya kijamii zilitajwa kama mojawapo ya sababu zilizosababisha mwandishi huyo wa habari kitaaluma aachie ngazi.

 

 

Ni kweli kuwa mitandao ya kijamii imeongeza nguvu ya sumu na hadaa katika suala hili la Chongolo lakini uwepo wa mitandao pekee hauelezi picha kamili ya kwa nini lililotokea limetokea na kwa nini hatua ya mashambulizi kwake ilifikia hapo.

 

 

Jambo la kuogofya kwa baadhi ya wana CCM ni kwamba kilichotokea kwa kada wake huyo kimetengeneza kitu ambacho kwenye lugha ya sheria kinaitwa precedent – kwamba kuanzia sasa, kama hukubaliani au humtaki Katibu Mkuu au pengine Mwenyekiti wa chama, namna ya kushughulika naye ni namna iliyotumika kwa Chongolo.

 

Namna ipi ilitumika ‘kummaliza’ Chongolo? Ni kutengeneza hadithi na picha zilizokuwa na lengo la kumvunjia hadhi na heshima kwa Watanzania – na mbaya zaidi, kwa familia yake. Kwa sisi ambao tumefikia umri wa kuwa na watoto wanaokwenda shule na wanaojua kutumia simu na mitandao, kilichofanywa kwa Katibu Mkuu huyo ni ndoto mbaya kabisa kuwa nayo.

 

 

Kama alivyoniuliza rafiki yangu yule, “hebu fikiria umekaa zako na last born unamsaidia homework halafu Junior (si jina halisi la mtoto wake mkubwa), anakufuata kukuonyesha picha zako zilizosambazwa mitandaoni ambazo anasema watoto wenzake walikuwa wanamtania darasani. Kama mambo yenyewe ni haya, si afadhali niendelee kulima maharage kuliko kuwa Katibu Mkuu?”.

 

 

Chongolo na Uhai wa Vyama vya Siasa

 

 

Tafakari kuu ambayo ilinijia kichwani kuhusu suala hili la Chongolo lilihusu ni njia ipi ambayo CCM imeamua kuifuata kuanzia sasa. Niseme mapema kwamba siandiki makala haya kwa lengo la kumtetea kada huyo wa chama tawala. Siku aliyokubali kuwa Katibu Mkuu wa CCM, ndiyo siku aliyojua pia kwamba cheo hicho si cha kudumu. Walikuwepo wengine kabla yake na watakuja wengine baada yake.

 

 

Na kuondoa Kinana ambaye tuliambiwa kwamba aliomba mwenyewe kuachia Ukatibu Mkuu wakati wa Magufuli ili apumzike, makatibu wengine wote waliobaki waliondoka kwa sababu iliyohusu muktadha wa wakati husika. Ishu ya Chongolo inahusu CCM kama chama na taratibu zake.

 

 

Katika kitabu chake mashuhuri cha Party Brands in Crisis, Dk. Noam Lupu, ametoa sababu mbili za ni kwa vipi vyama vilivyokuwa madarakani huondolewa au kufa baada ya muda fulani. Kuna vitu viwili husababisha vyama kufa; cha kwanza ni hali mbaya ya uchumi na pili ni kubadilika kwa tabia au mwelekeo wa chama.

 

 

Kimsingi, la pili ni la hatari zaidi. La kwanza, ameandika Lupu, linahimiliki hasa kwa wale wanachama kindakindaki wa chama husika. Kama tunavyoona nchi kama Venezuela, pamoja na hali ngumu ya uchumi, bado kuna watu wana imani na chama tawala cha taifa hilo. Hata hali ikiwa ngumu kiasi gani kiuchumi na watu wengi wakahama, wafia chama watabaki ali mradi tabia na mwelekeo wa chama umebaki uleule.

 

Lupu anasema tabia na mwonekano wa chama ni jambo muhimu kwa chama chochote kinachotaka kuendelea kudumu madarakani. Kuna vitu ambavyo inatakiwa watu wakiona wajue kwamba hii ndiyo CCM, CHADEMA au ACT Wazalendo wanayoijua. Nje ya hapo, ni rahisi kwa chama kumomonyoka.

 

 

 

CCM kwa zaidi ya nusu karne sasa, imekuwa na utaratibu wake wa kubadilisha makatibu wakuu wake kistaarabu. Hatujui kwa nini Mangula alichukua nafasi ya Lawrance Gama na wala hatukuambiwa sababu zilizosababisha Mzee Makamba achukue nafasi ya Mangula. Huko ndani wenyewe wanajua kinachoendelea lakini huku nje hakuna ajuaye. Ni imani tu kwamba kila zama zina kitabu chake.

 

 

Kwa nini vyama hubadili tabia na mwonekano wake (brand)? Lupu anaamini sababu kubwa ni kutaka kushinda uchaguzi kwa gharama yoyote. Matokeo yake ni kukubali kushirikiana na watu ambao hawajali gharama ya kulinda tabia au mwonekano wa chama. Ni kukubali kufanya kazi na makundi tofauti mkiamini kwamba lengo lenu ni moja.

 

 

Ukweli ni kwamba hali hugeuka tofauti baadaye. Kwa sababu ya kutaka kukishinda chama cha Democrat – Republican wa Marekani waliamua kushirikiana na watu wa mrengo mkali wa kulia – wanaoishi kwa uzushi; kama wa kusema Rais Barack Obama hakuzaliwa Marekani na baba yake alikuwa gaidi wa mwenye msimamo mkali wa Kiislamu; uongo mtupu, ili washinde mwaka 2016.

 

 

 

Matokeo yake ndiyo yakamfanya Donald Trump awe mgombea urais wake. Hivi sasa, Republican imebaki kama kasha tu likifuata tabia na matamko ya Trump na watu wake na mara nyingi ni masuala yasiyo na uhusiano wowote na tabia na mwonekana wa Republic kama ulivyozoeleka kwa zaidi ya miaka 200.

 

 

 

Hisia zangu ni kwamba kwa sababu ya kutaka kushinda uchaguzi wa mwaka 2025 na kuendelea, CCM imeamua kushirikiana na kushirikisha watu ambao hawajali na hawana uhusiano wowote na chapa ya chama hicho iliyojengwa kwa zaidi ya nusu karne sasa.

 

 

Kama anavyoasa Lupu, huu ni mwelekeo mbaya kwa chama kinachotaka kuendelea kuishi kisiasa au kubaki madarakani. Hatari kubwa iliyopo ni kwamba wafia chama wanaweza kuvumilia shida za kiuchumi lakini uvumilivu wao ni mdogo kwa mambo ambayo hayasimamii tena misingi, maana na chapa ya taasisi iliyotengenezwa na waanzilishi miaka mingi nyuma.

 

 

Ndiyo sababu namuelewa rafiki yangu aliyeamua kwamba kulima maharage kutamlindia heshima yake kuliko kushika cheo kikubwa lakini ambacho baadaye kinaweza kumletea fedheha na kumvunjia heshima kwa Watanzania wenzake – na mbaya zaidi, kwa familia yake.

 

 

Kwa vyovyote vile, CCM na vyama vingine vya kisiasa vinavyotaka kubaki madarakani au kuwa hai kisiasa, suala la ulinzi wa tabia na mwonekano wa chama ni suala la kufa au kupona. Na hili sijasema mimi. Kama ukipata nafasi ya kumuuliza Noam Lupu kuhusu jambo hilo, hata yeye atakueleza hivyo.

 

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.