Chapo tayari, Tanzania icheze kete ya kwanza

Na Ezekiel Kamwaga

 

MAPEMA kabisa, ni muhimu nikaweka wazi kwa nini naandika uchambuzi huu. Kwanza Msumbiji ni rafiki wa damu wa Tanzania, pili kwenye mpaka wetu nao kuna tishio la kiusalama na tatu tunapakana katika eneo ambako huenda nchi yetu ikafanya mradi mkubwa zaidi wa uwekezaji kwenye historia yake – wa LNG. Ni nchi chache sana zina uhusiano zinatuhusu kidamu, kiusalama na kiuchumi kwa kiasi hiki.

 

 

Kwa nini Msumbiji ni ndugu zetu wa damu? Kwanza, damu ya mwasisi wa chama tawala cha FRELIMO kilichopambania uhuru wa Msumbiji kwa damu, Eduardo Chivambo Mondlane, ilimwagika katika ardhi yetu baada ya kuuawa kwa bomu lililotegwa kwenye bahasha na wakoloni Wareno.

 

 

Halafu Tanzania tukatuma askari wetu, silaha zetu na pesa zetu kwenda kusaidia mapambano ya Uhuru wa taifa hilo mpaka walipofanikiwa mwaka 1975. Majemedari wetu, kama Kanali Ali Mahfoudhi, wamezikwa kwenye eneo la makaburi ya Mashujaa wa Msumbiji jijini Maputo.

 

 

Lakini si kwamba wao hawajatufanyia kitu. Kwenye vita yetu dhidi ya Nduli Idi Amini, Msumbiji ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zilizoungana nasi waziwazi, kwa kuleta askari na zana kutusaidia. Kuna askari wa taifa hilo wamewahi kumwaga damu yao kwa ajili yetu.

 

 

Na tulipoingia kwenye mgogoro na Malawi enzi za Rais Joyce Banda na jirani zetu hao walipoamua kuagiza boti ya kivita kwa ajili ya kulinda Ziwa Nyasa lililokuwa na mgogoro, Ni mamlaka za Msumbiji ndizo zilizotutonya kuwa jirani zetu hao wameagiza silaha za kutuumiza. Kosa la Malawi lilikuwa kupitisha silaha yao kwenye bandari ya ndugu zetu wa damu. Vita ya Msumbiji ni vita yetu. Vita ya Tanzania ni ya Msumbiji.

 

 

Ilikuwa muhimu kwangu kuweka utangulizi huu wa kihistoria kabla sijaingia kwenye masuala ya kisiasa na kijiopolitiki yaliyotokea kufikia kuchaguliwa kwa Daniel Chapo kuwa mgombea urais wa FRELIMO na pengine Rais ajaye wa Msumbiji.

 

 

Namna Chapo alivyopatikana

 

 

Kupitishwa kwa Chapo kuwa mgombea urais wa FRELIMO katika Uchaguzi Mkuu wa Msumbiji uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, hakukutarajiwa na wengi. Huyu hajawahi kuwa waziri au mjumbe katika vyombo vikuu vya uamuzi vya Msumbiji.

 

 

Marais waliomtangulia baada ya Samora Machel; yaani Joachim Chissano, Armando Guebuza na Felipe Nyusi walikuwa ni maveterani wa vita ya ukombozi na watu waliowahi kushika nyadhifa za juu kwenye serikali na FRELIMO. Chapo amezaliwa mwaka 1977 ikimaanisha miaka miwili baada ya Uhuru wa taifa hilo.

 

 

Ilikuaje Chapo akashika nafasi hiyo? Kupitia mfumo uliopo Tanzania, kwa mfano, hakuna uwezekano walau kwa sasa kwa mtu aliyewahi kuwa Gavana wa Jimbo (tuseme Mkuu wa Mkoa kwa hapa kwetu), kushinda urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa hajawahi kuwa walau waziri au Mjumbe wa Halmashauri Kuu au Kamati Kuu ya CCM.

 

 

Mfumo wa FRELIMO kwenye kupata mgombea wake wa urais haufanani na wa CCM – au vyama vyote vikubwa vya siasa hapa nchini. Hapa kwetu mgombea anatakiwa kutangaza nia. Kwa Msumbiji, Kamati ya Siasa ya Chama (Political Commission) ndiyo hufanya kazi ya kuchagua majina matatu ya watu wanaofaa ambao ndiyo huenda kupigiwa kura kwenye Kamati Kuu.

 

 

Mwaka huu, mtoto wa hayati Samora, Samora Machel Jr, alivunja mwiko kwa kutangaza mwenyewe nia yake ya kuwania urais baada ya kuonekana kana kwamba Rais Felipe Nyusi ana nia ya kubadili Katiba ili aendelee.

 

 

Kwa wafuatiliaji wa siasa za Msumbiji, hii si mara ya kwanza kwa mtu asiyepewa nafasi kushinda kwenye uchaguzi wa ndani ya chama. Wakati Nyusi akiwania nafasi kwa mara ya kwanza mwaka 2014, wengi walitaraji Luisa Diogo – aliyekuwa Waziri Mkuu enzi za Chissano, ndiye ambaye angeshinda. Lakini Nyusi akaibuka kidedea.

 

 

Lakini angalau Nyusi alikuwa Waziri wa Ulinzi na veteran wa vita ya ukombozi. Chapo amemshinda aliyekuwa Katibu Mkuu wa FRELIMO, Roque Silva, ambaye ni kigogo wa chama. Kushindwa kwake na Chapo kumemfanya Silva ajiuzulu wadhifa wake huo wa Ukatibu Mkuu.

 

 

Binafsi, siamini kwamba Chapo ameshinda kwa bahati mbaya. Ninaamini kuna ‘mkono’ uliofanya kazi kwa mlango wa nyuma kuhakikisha anashinda. Inafahamika Silva hakuwa anapendwa na wanachama wengi wa FRELIMO kwa vile alionekana mtu wa karibu wa Nyusi. Naamini Chapo ni chaguo la Nyusi na amechaguliwa kwa mbinu kali.

 

 

Kwa nini naamini hivi? Kwa sababu zipo taarifa za kutosha kuwa Chapo ni swahiba wa Waziri wa Kilimo wa Msumbiji, Celso Ismael Correia. Na ndani ya nchi hiyo, inafahamika kwamba Correia ni mtu wa karibu na Nyusi.

 

 

Kwa miaka miwili nyuma, baadhi ya ripoti zinaonyesha, Celso aliweka kambi kwenye Jimbo la Sofala lililoko katikati ya Msumbiji. Mkoa wa Inhambane anakotoka Chapo, upo Sofala alikoweka kambi Celso. Akili yangu inaniambia Nyusi alishafahamu kuwa mtu wa karibu naye hatakubalika na akijua Msumbiji haijawahi kutoa Rais kutoka katikati ya nchi, akampa swahiba yake kazi ya kutafuta mtu. Ndiyo huyu sasa Daniel Francisco Chapo.

 

 

Tanzania inatakiwa kufanya nini?

 

 

Mara baada ya kupitishwa kwake na FRELIMO, Nyusi aliifanya Tanzania kuwa nchi yake ya kwanza duniani kuja kujitambulisha. Na alipokuwa Rais, ilikuwa nchi yake ya kwanza kututembelea. Huo ni utaratibu aliorithi kwa Chissano na Guebuza.

 

 

Na marais wote hao watatu; Nyusi, Chissano na Guebuza walikuwa na mahaba na Tanzania kiasi kwamba walikuwa wanazungumza lugha ya Kiswahili. Kwa nyakati tofauti katika maisha yao, waliwahi kuishi Tanzania. Walikuwa wanajua udugu wetu wa damu.

 

 

Chapo amezaliwa baada ya vita. Sifahamu kama anazungumza Kiswahili lakini ni jambo la hakika kwamba hawezi kuwa na mahaba na Tanzania kama waliyokuwa nayo watangulizi wake.

 

 

Ninafahamu pia kwamba uhusiano wetu na Msumbiji uliyumba kidogo enzi za utawala wa Rais John Magufuli. Baadhi ya vigogo wa taifa hilo hawakuwahi kuelewa kwa nini Tanzania haikutuma vikosi vyake kuihami Msumbiji wakati magaidi walipoanza kuishambulia.

 

 

Magufuli hakuamini kwamba kazi ya kuihami Msumbiji ni sehemu ya wajibu wetu kama “kaka mkubwa”. Yeye aliamini kwamba mara baada ya Uhuru, Msumbiji ilitakiwa kujijengea uwezo wa kijeshi na kiusalama kupambana na magaidi hao. Kwamba Tanzania ilishajitolea sana huko nyuma na haiwezi kuendelea kufanya hivyo.

 

 

Rwanda ikaamua kutuma Jeshi lake na hadi leo liko huko. Ziko ripoti za kutosha zinazoonyesha kwamba katika miaka ya karibuni, Nyusi amekuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Rwanda kwa sababu hiyo. Vikosi vya SADC viko lakini inaonekana Rwanda ndiyo yenye wajibu mkubwa zaidi.

 

 

Naamini hatua ya kwanza kwa Tanzania kuanzia hapa tulipofika ni kuhakikisha Chapo anatembelea kwetu kujitambulisha kama walivyofanya watangulizi wake. Kuna faida mbili za kufanya hivi; ya kwanza ni kuonyesha kwamba uhusiano wetu bado uko palepale na pili ni kubwa zaidi.

 

 

Katika umri wake wa miaka 47 na akiwa hajawahi kushika wadhifa wowote mkubwa kisiasa, Chapo ni mwanasiasa mchanga. Kwa lugha ngumu kidogo, Rais huyu ajaye wa Msumbiji ni mtoto. Nchi yake ya kwanza kutembelea, itakuwa na nafasi kubwa ya kumtengeneza kimaono. Labda nikupe picha kidogo, miaka minane tu iliyopita, alikuwa mtangazaji wa kawaida katika redio ya Miramax iliyopo nchini kwake. Kasoma sheria kwenye vyuo vya ndani ya nchi yake. Hajawahi kutoka nje kusaka maarifa.

 

 

Huyu ni wa kupelekwa Oysterbay alikouawa Mondlane. Huyu ni wa kuonyesha ilipokuwa Farm 17. Huyu ni wa kufikishwa mahali ambako akina Uriah Simango na wenzake waliuawa kwa kunyongwa na wapigania uhuru wenzao wa FRELIMO.

 

 

Kama atahitaji msaada wowote, Tanzania iwe na mpango wa kumsaidia. Na muhimu sana kwa watu wetu wa Mambo ya Nje pamoja na uwekezaji kuangalia ni maeneo yapi tunaweza kufanya kukuza uchumi wa nchi zetu mbili.

 

 

Kwa nini tunasikia kila siku kuhusu Namanga, Tunduma, Sirari, Horohoro lakini hatusikii sana kuhusu Mtambaswala? Kuna barabara ya maana ya kuunganisha Tanzania na Msumbiji? Kuna ndege zinazofanya safari baina ya nchi zetu mbili? Kuna mikutano ya wafanyabiashara baina ya nchi zetu mbili? Kile chuo cha diplomasia – sasa cha Dk. Salim Ahmed Salim, kinatumikaje kwenye miaka ya karibuni kukuza uhusiano wetu na Msumbiji.

 

 

Katika mojawapo ya insha nilizowahi kuandika kama sehemu ya masomo ya Shahada ya Uzamili katika African Politics kwenye Chuo Kikuu cha SOAS, Uingereza, nilisaili kuwa tatizo la Cabo Delgado ni tatizo la umasikini. Namna ya kupambana na ugaidi wa Cabo Delgado ni kuhakikisha gesi iliyopo pale inanufaisha watu wa Msumbiji.

 

 

Wakati Tanzania ikiajiandaa pia kuingia kwenye mradi wa LNG – kama ambavyo Msumbiji inaingia, kuna haja ya kusaidiana maarifa na uzoefu kuona ni kwa vipi tunaweza kufaidika kwa pamoja na utajiri huu aliotupa Mwenyezi Mungu.

 

 

Tanzania na Msumbiji ziko katika sehemu tofauti kwenye mradi huo lakini bado kuna fursa ya kushirikiana na kusaidiana kwa faida ya watu wetu. Haya ndiyo mambo ambayo Daniel Chapo anatakiwa kuelezwa mapema kabisa.

 

 

Kwa sababu, kama hamuwezi kuelewana katika masuala ya uchumi na usalama, hamuwezi kuelewana tena katika jambo lingine. Hii ni kwa sababu, binadamu – kwa hakika, anaogopa vitu viwili tu; njaa na kifo.

 

 

Utajiri wa gesi asilia unaweza kusaidia kuondoa njaa kwa jamii yetu. Na tishio hili la la usalama la Cabo Delgado linatuunganisha sote – iwe tunapenda au hatupendi.

 

 

Ni wajibu wa Tanzania kucheza kete ya kwanza.

 

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.