Katibu Mkuu wa CCM: Historia Fupi

Na Ezekiel Kamwaga

DANIEL Godfrey Chongolo amemaliza muhula wake kama Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuandika barua ya kujiuzulu na kuhitimisha takribani miaka miwili na miezi saba ya kutumikia nafasi hiyo. Wakati alipotangazwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, si watu wengi walikuwa wamewahi kumsikia kabla – ingawa aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Longido na Kinondoni, lakini pasi na shaka, sasa hakuna ambaye hajawahi kumsikia.

 

Ni muhimu nikaeleza mapema kwamba Chongolo ni mtu ninayefahamiana na kuheshimiana naye na kwa hakika sijafurahishwa na namna na aina ya mashambulizi yaliyoelekezwa kwake katika siku za mwisho za uongozi wake. Ninafahamu kwamba katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Chongolo ameifanyia CCM mambo mengi makubwa nyuma ya pazia na baadhi ya wale waliokuwa wakiongoza mashambulizi dhidi yake, hawajawahi kutoka damu na jasho kwa ajili ya CCM kama alivyofanya Daniel mbele na nyuma ya pazia. Lakini hii ni mada ambayo nitaisawiri vizuri zaidi kwenye makala zijazo.

 

Makala yangu ya leo inataka kueleza kuhusu wadhifa huu wa Katibu Mkuu wa CCM. Ni wadhifa wenye majukumu makubwa na wakati watu wakiwa wanajiuliza ni nani anaweza kuvaa viatu vya Chongolo baada ya kumalizika kwa kadhia yake, ni muhimu kufanya uchambuzi wa nafasi yenyewe kwa asili ili kuweza kubashiri ni nani anaweza kuwa mrithi wake.

 

Ni muhimu kujua kwamba kabla ya Chongolo, watu wengine 10 waliwahi kushika wadhifa huo; Pius Msekwa, Daudi Mwakawago, Rashid Kawawa, Horace Kolimba, Lawrance Gama, Philip Mangula, Yusuph Makamba, Wilson Mukama, Abdulrahman Kinana na Bashiru Ally. Yeye alikuwa Katibu Mkuu wa 11 na muda si mrefu kutoka sasa kutakuwa na Katibu Mkuu wa 12.

 

Kabla ya kufahamu ni nani anaweza kuwa Katibu Mkuu ajaye wa CCM, ni muhimu tukafahamu sifa na aina ya makatibu wakuu waliotangulia huko nyuma. Lakini, muhimu zaidi, ni kurudi nyuma na kuelewa nini kilitokea nyakati za chama cha TANU ambacho muungano wake na ASP ya Zanzibar ndiyo uliozaaa CCM.

 

Doa la Kambona

 

Baada ya Uhuru wa Tanganyika, Katibu Mkuu wa chama tawala cha TANU alikuwa Oscar Salathiel Kambona. Waliobahatika kuwa watu wazima na jirani na mamlaka nyakati zile, wanamueleza kama mwanasiasa aliyekuwa wa pili kwa mvuto nchini Tanganyika – pengine akizidiwa na Baba wa Taifa, Julius Nyerere. Katika mazungumzo niliyowahi kufanya na aliyekuwa Mnadhimu wa Jeshi la Tanganyika, Ameen Kashmiri, katika baadhi ya maeneo na makundi, Kambona alikuwa akipendwa kuzidi Nyerere.

 

Baada ya kunusurika katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1964, uhusiano wa Nyerere na Kambona ulivurugika. Kwa kutazama hali ilivyokuwa, Kambona alikuwa Katibu Mkuu mwenye sifa kubwa tatu; anayeaminiwa na Rais kwa sababu ya ukaribu wao (Nyerere alikuwa best man kwenye harusi ya Kambona), anayekubalika kwa wananchi na ambaye anaonekana kama mbadala wa Rais pale itakapolazimu kutokea kwa mabadiliko ya uongozi. Katibu Mkuu wa TANU alikuwa sawa na Rais anayeandaliwa.

 

Na hili wala si jambo la ajabu. Katika vyama vingi vyenye mrengo wa kikada kama ilivyo CCM, nafasi ya Katibu Mkuu wa chama ni nafasi kubwa. Nchini China, kwa mfano, Rais Xi Jinping pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China, chama tawala nchini humo. Kwa kifupi, katika vyama vya kikada, Katibu Mkuu anatakiwa kuwa mtu ambaye watu wanamwona kama mtu anayeweza au anayeandaliwa kuwa Rais au kiongozi ajaye wa taifa husika.

 

Baada ya tukio la Januari, 1964, ni kama vile Nyerere aliamua kuwa na mtazamo mpya kuhusu nafasi ya Katibu Mkuu. Baada ya Kambona kuamua kukimbia nchi na kwenda kuishi ughaibuni huko Uingereza, hata jina la Katibu Mkuu wa chama lilibadilishwa kuwa Katibu Mtendaji. Wakati CCM inaanza mwaka 1977, Katibu Mtendaji wa kwanza alikuwa Pius Msekwa. Msekwa, kwa usuli, aliwahi kuwa mwanafunzi wa Nyerere na hakuna Mtanzania aliyemwona kama mwanasiasa anayeweza kuwa mbadala wa Nyerere.

 

Makatibu waliomfuata, Mwakawago na Kawawa, walikuwa wanasiasa mahiri na watu wa karibu na Nyerere lakini ni wazi Nyerere aliwaamini zaidi kwa uaminifu wao na si kama wanasiasa ambao wangeweza kumsumbua kwa kuwa na tamaa au dhamira ya moyoni ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania baada yake.

 

Wakati alipokuwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Ally Hassan Mwinyi aliamua kutafuta Katibu Mkuu wake. Kura yake iliangukia kwa Horace Kolimba aliyejenga jina kupitia Vyama vya Wafanyakazi wa Tanzania. Ni muhimu kuweka muktadha hapa. Mwinyi alikuwa akijulikana kama Rais kutoka Zanzibar na hivyo ilikuwa muhimu kuwa na Katibu Mkuu ambaye walau ana base – kundi miongoni mwa makundi yaliyo ndani ya CCM. Baadaye Kolimba akawa tatizo kubwa kiasi kwamba ilibidi aondolewe kwenye wadhifa huo na nafasi yake kuchukuliwa na Lawrance Mtazama Gama, mtu ambaye aliaminiwa na mfumo (deep state) ingawa Watanzania hawakumuona kama Rais mbadala.

 

Benjamin Mkapa ndiye Mwenyekiti pekee aliyekaa na Katibu Mkuu mmoja tu kwenye Uenyekiti wake wa CCM. Philip Japhet Mangula alikuwa mtu wake kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2007. Mangula hakutoka katika kundi lolote mashuhuri ndani ya CCM lakini alikuwa ni Katibu aliyejua majukumu yake na ‘kulinda’ ofisi kwa ajili ya Mwenyekiti.

 

Kwenye uenyekiti wa Jakaya Kikwete, aliamua kumpa nafasi Yusuph Makamba, kada wa CCM waliyekuwa wakifahamiana na kuaminiana. Baada ya miaka 10 ya Uenyekiti wa Mkapa na Mangula ambao wengi ndani ya chama walikuwa wakiwaona kama “Wakuja”, Kikwete aliamua kukirejesha chama kwa wenye chama. Makamba hakuwa mtu ambaye watu walimwona kama Rais ajaye lakini bado alikuwa ni mtu ambaye alikijua chama na akiaminiwa pia na Mwenyekiti kama mtu ambaye asingemgeuka ndani ya chama.

 

Kikwete alikwenda mbele zaidi. Alimteua swahiba wake wa muda mrefu, Jaka Mwambi, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama. Pasi na shaka yoyote, lengo lilikuwa si tu kuwa na chama ambacho viongozi wake wanakijua chama nje ndani, lakini kuwa na watu ambao Mwenyekiti anawajua na kuwaamini.

 

Uteuzi wa Wilson Mukama – mwenye rekodi ya kuwa Katibu Mkuu aliyetumikia chama kwa muda mfupi zaidi, ulikuwa ni wa kimazingira zaidi. Huyu ni mtu ambaye aliandika waraka wa kueleza ni kwa vipi chama kinaweza kujijenga upya kufuatia minyukano ya makundi ya CCM Asilia na CCM Mtandao iliokuwa ikitafuna chama nyakati zile. Mukama alionekana kama kiongozi asiye na upande ambaye angefanya kazi za chama pasi na kuwa na upande. Inaonekana hakufanikiwa katika wajibu huu.

 

Uteuzi wa Abdulrahman Kinana baada ya Mukama ulikuwa na malengo makubwa mawili; kwanza kumpa nafasi kada anayekijua chama vilivyo na mwenye uwezo mkubwa na pili anayeaminiwa na Mwenyekiti. Tofauti na makada wengi wa CCM, Kinana hajawahi kufahamika kuwa na nia ya kuwania Urais wa Tanzania na hivyo Kikwete hakuwa na hofu ya kutengeneza nguzo mbili za mamlaka ndani ya chama kimoja.

 

Kinana aliomba mwenyewe kupumzika wakati wa utawala wa Rais John Magufuli ambaye alimteua Dk. Bashiru Ally kuwa Katibu Mkuu wake. Uteuzi wa Bashiru uliwashangaza wengi lakini Magufuli aliamini hakuwa na wafuasi ndani ya CCM na hivyo aliamua kuwa na mtu wa nje kushika wadhifa huo. Mtu ambaye angekuwa mwaminifu kwake na asingetengeneza ngome yake binafsi ya kisiasa isiyo ya Mwenyekiti.

 

Uteuzi wa Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan aliyechukua nafasi ya Magufuli uliwashangaza. Kama mtu angetaja watu 10 waliokuwa wanastahili kuwa Makatibu Wakuu wa CCM wakati wa Uenyekiti wa Samia, jina la Chongolo lisingekuwepo. Hakuwa anajulikana sana nje ya CCM. Hata hivyo, uteuzi wake ulionesha imani ya kipekee ambayo Mwenyekiti wa CCM alikuwa nayo kwake.

 

Nini kinafuata?

 

Kwa kutazama historia ya Makatibu Wakuu wa CCM waliopita, kuna vitu kadhaa vinajiweka wazi. Kwa mfano, mambo yafuatayo yanajipambanua yenyewe; utii kwa Mwenyekiti, ukaribu na mwenyekiti, kukijua chama, utendaji usio na mashaka na mtu anayependekezwa na deep state.

 

Kwa vyovyote vile, Katibu Mkuu ajaye wa CCM atakuwa na sifa mojawapo kati ya zifuatavyo; mtu anayeaminiwa na Mwenyekiti, mtu ambaye hatatengeneza kundi lake ndani ya chama, asiye na malengo ya kuwa Rais mbele ya safari na mwenye uwezo wa kuchapa kazi na ushawishi usio na shaka.

 

Kihalisia, si jambo rahisi kama namna hii nilivyoandika. Lakini, kwa hakika kabisa, simuoni Mwenyekiti akipendekeza kwa Halmashauri Kuu ya CCM jina la mtu ambaye hatamsaidia kushinda uchaguzi – kuanzia wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.  Hii ni kwa sababu, pamoja na mambo mengine yote; kazi ya kwanza ya chama cha siasa ni kutafuta namna ya kushinda uchaguzi.

 

Kushinda uchaguzi kuko kwa namna nyingi. Unaweza kushinda uchaguzi kwa sababu Katibu Mkuu – tuchukulie mfano wa Kolimba aliyekuwa Katibu Mkuu aliyepewa nafasi na Rais kutoka Zanzibar wakati ule, ni mtu ambaye ana kundi lake tayari na uteuzi wake unamaanisha moja kwa moja kura zote za kundi hilo zinakuja kwa Mwenyekiti.

 

Mwenyekiti Samia anaweza pia kuchagua Katibu Mkuu ambaye hawakilishi kundi lolote katika chama lakini ni mtu anayejua nini maana ya cheo hicho na anayeweza kuyabeba makundi yote mkononi kwake. Anaweza hata kuamua kuchukua mtu kutoka nje kabisa ya chama – kama alivyofanya Magufuli kwa Bashiru, lakini akawa mtu anayefahamika na kuheshimika na Watanzania na makundi yote ndani ya chama. Huyu ni mtu wa kujenga chama pasipo makundi.

 

Ndugu yangu Chongolo alikuwa anahusishwa na mojawapo ya makundi maslahi ndani ya CCM na pengine walioongoza mashambulizi dhidi yake katika siku za mwisho za uongozi, ni wale walioona kwamba hana msaada kwao sasa na anasaidia kundi lake zaidi kuliko wao. Kwa sababu hiyo, kufanikisha kutolewa kwake ilikuwa ni kufanikisha mpango wa kuwa na mtu wanayemwamini katika nafasi hiyo.

 

CCM inaweza kuamua pia kuwa na mtu ambaye kundi lake ndani ya chama linajulikana lakini ni mtu ambaye wengi wa wanachama watasema ni “mwenzetu” na zimwi likujualo halikuli likakwisha. Baada ya miaka mingi ya Mangula, Jakaya aliamua kumpa nafasi Makamba ambaye usuli wake ndani ya chama ulifanya wanachama waamini ni mwenzao aliyepata nafasi si mgeni au wa kuja.

 

Upo uwezekano pia wa kumchagua mtu ambaye Mwenyekiti ana imani naye ni mtu ambaye hana wasiwasi naye. Ni kama vile Mwalimu alivyoamua kumchagua mtu kama Msekwa kuchukua wadhifa wa Katibu Mtendaji mwaka 1977. Shida ya jambo hili ni kwamba katika dunia ya sasa ambako siasa za ubaguzi wa utaifa zinamea duniani, Rais Samia anahitaji mtu wa Bara ambaye anaweza kumwongezea kura kwa ile tu kuonekana kwamba ni mtu wa ndani na mwenye mamlaka kwenye serikali yake.

 

Kama mdadisi wa siasa za Tanzania katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, naona watu wawili tu wenye nafasi ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM baada ya Chongolo; ama mtu kutoka nje ya chama anayeheshimiwa na Watanzania, asiye na kundi maalumu ndani ya CCM na mwenye rekodi nzuri ya utendaji au kada kindakindaki wa chama, anayeaminiwa na Mwenyekiti na mwenye uwezo wa kuongeza kura kwenye chaguzi zinazoikabili CCM kuanzia mwakani.

 

Tusubiri