Tunafuturu futari, hatufutari futuru

 

Na Ahmed Rajab

 

MIAKA kadhaa iliyopita katika siku kama hizi za mfungo wa Ramadhani niliwahi kuandika makala katika gazeti la Raia Mwema ambamo nililalama jinsi aina kwa aina ya mapishi asilia ya Kiswahili yalivyotoweka Zanzibar baada ya Mapinduzi ya 1964.

 

 

Nilijawa na furaha nilipoona kwamba makala hayo yaliwachochea wengine kuendeleza na kuandika katika mitandao ya kijamii kuhusu mada hiyo.

 

 

Makala yangu hayajakusudia kuvitaja vyakula vya Zanzibar nzima vilivyoadimika au kupotea kabisa. Nisingaliweza. Nilijikita katika sehemu tu ya Mjini, Unguja, nilikozaliwa na kukulia. Kumbukumbu zangu zilinipeleka kwenye mitaa ya Vuga, Mkunazini, Kajificheni, Shangani na Baghani.  Kumbukumbu hizo hazikuuranda mji mzima, hazikufika Ng’ambo wala shamba seuze Pemba.

 

 

 

Walionifuata kuandika walifanya kazi kubwa ya kutukumbusha vilaji au maakuli ya zamani yaliyokuwa yakipikwa na kuliwa katika sehemu nyingine za Unguja. Waliongeza idadi ya aina ya vyakula ambavyo siku hizi havinusiki wala havionjeki kwa sababu havipikwi tena.

 

 

 

Pamoja na kutupa nguvu za kuishi, vyakula vina umuhimu wa kutuwezesha kujitambulisha kijamii na hata kitaifa.  Kwa hivyo ni muhimu si kwa uhai wa watu tu bali pia kwa uhai wa utamaduni wa watu, na wawe wa wapi.

 

 

 

Vyakula vyetu vya Kiswahili vina historia ndefu inayotokana na biashara pamoja na uhamiaji wa watu wa tamaduni tafauti katika eneo linalotambuliwa kuwa ni la Uswahilini — yaani kutoka kusini mwa Somalia, kuteremka chini kupitia miambao ya Kenya na Tanganyika, Zanzibar, Msumbiji hadi visiwa vya Comoro na kufikia kijipembe cha Bukini (Madagascar). Visiwa vya Kenya vya Lamu, Pate na Siyu na vile vya Tanganyika vya Mafia, Kilwa Kisiwani na Kilwa Kivinje, navyo vimo katika chungu hicho cha Uswahilini.

 

 

 

Eneo hilo lina historia ya karne zisizopungua elfu moja za kufanya biashara na watu ajinabi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Majahazi ya Wahindi yaliikata, kwa mfano, Bahari Kuu ya Hindi yakatuletea pilau, masala na viungo mbalimbali vya vyakula.

 

 

 

Wachina nao waliyakata mawimbi ya bahari hiyo na wakatuletea tambi; Wafursi (Waajemi) walituletea zaafarani na biriani; Wayemeni walituzoesha kahawa na papa wakavu na Waarabu wengine walikuja na tende na haluwa.

 

 

Tukiacha biashara kulikuwako pia ukoloni uliolivamia eneo letu na kuathiri utamaduni wetu wa vyakula.  Wavamizi Wareno, kwa mfano, walituletea mahindi, viazi vitamu na muhogo mnamo katikati mwa karne ya 15.

 

 

 

Tumebahatika kupata utajiri mkubwa wa kuingiliana na watu wa tamaduni mbalimbali zilizochanganyika na utamaduni asilia wa eneo letu. Matokeo yake ni kuchipuka kwa ustaarabu wa aina ya pekee tunaojivunia.

 

 

 

Bahati mbaya, mikondo ya maisha imevichukua baadhi ya vyungu, sufuria na vikaango vya mapishi yetu na kwenda navyo na maji.  Wapishi wetu wataufanyia jamala kubwa ustaarabu wetu wakiweza kuyafufua mapishi ya hivyo vyakula vyetu vilivyokwenda na maji. Wakifanikiwa wataufanyia hisani kubwa ustaarabu wetu na mapisi yetu kwa maana ya historia yetu kwani mapisi ya mapishi yetu ni sehemu adhimu na ya tunu katika Uswahili wetu.

 

Namna tunavyovipika vyakula vyetu kumechangia kwa sehemu kubwa katika utambulisho wetu wa kitamaduni kama namna wapikavyo watu wengine kulivyochangia katika utambulisho wa tamaduni zao.

 

 

 

Siku hizi kumezuka mtindo unaosikitisha wa wasio Waswahili wenye kusema Kiswahili kutubadilishia hata majina ya vyakula vyetu.  Hubadilisha istilahi, kama kwa mfano, badala ya samaki wa kupaka na kuku wa kupaka wao husema samaki wa nazi na kuku wa nazi.  Nyama ya kima (yaani ile iliyosagwa) wao huiita nyama “iliyokunwa”.

 

 

Siku hizi kwetu Zanzibar na hata katika mwambao wa Kenya, huwasikii sana watu wakiitaja mikate ya kusukuma. Badala yake tangu mwongo wa 1970 watu wamekuwa wakiita mikate ya kusukuma kwa jina la chapati ingawa huko Bangladesh, India na Pakistan zinakoliwa hizo chapati sura zake hazifanani na mikate yetu ya kusukuma. Mikate yao inayofanana na yetu ya kusukuma huitwa parata.

 

 

Sijui kwa nini ikawa mikate yetu ya kusukuma inaitwa chapati badala ya parata yenye kufanana nayo. Hata hivyo, nathubutu kusema kwamba mikate ya kusukuma ya Uswahilini ina ladha iliyo bora kushinda ile ya parata. Sijui ladha hiyo inatokana na namna tunavyoisukuma hiyo mikate au vipi.

 

 

 

Aidha mikate yetu ya kusukuma ni ya siha zaidi kuliko parata kwa vile tunapoipika, sisi huwa hatutumii mafuta au samli nyingi sana kama watumiavyo Wahindi, Wabengali au Wapakistani.

 

 

 

La kusikitisha zaidi ni kukisikia Kiswahili pia kikikorogwa. Katika miaka ya mwongo wa 1980 mimi binafsi nilianza kusikia watu katika mwezi kama huu tulionao wa Ramadhani wakisema kwamba wanafutari badala ya kuwa wanafuturu. Vipi kufuturu kukabadilika na kukawa kufutari pia sijui. Nijuavyo ni kwamba ni kosa kusema hivyo.

 

Katika sehemu zote za Uswahilini watu hufuturu futari. Kitendo cha kula baada ya kufunga swaumu ni kufuturu. Chakula kiliwacho wakati wa kufuturu ndio futari. Mtu akiwaalika watu kwenda kwake kufuturu huwa anafuturisha na wala hafutarishi.

 

 

 

Wafungao swaumu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani hufungua, yaani huruhusiwa kula, pale saa za kufunga zimalizikapo au mwadhini anapoadhini adhana ya swala ya Magharibi. Watu wengi hufungua kwa kula kitu kidogo, halafu huswali na baadaye ndo hukaa kitako wakafuturu mpaka wakashiba wakitaka kushiba. Sasa pale wanapofungua kwa kula kitu kidogo kama vile tende au kwa kupiga fundo au tama la maji huwa ‘wanafungua mwadhini’.

 

 

 

Ramadhani si kufunga na kuswali tu.  Na wala swaumu si kinga peke yake. Ramadhani ina mengi mengine lakini ya mwaka huu imekuwa ngumu zaidi kwa Waislamu wengi duniani.  Wao huona taabu kufuturu kwa raha ilhali wenzao wa Gaza wakifunga bila ya futari au hata maji. Wanaobahatika hufuturu kwa idhilali kwa kugaiwa vibakuli vya shurba, supu, au vijipande vya mikate. Tarawehe wanaiswali kwenye vifusi.

 

 

 

Hali duni za kufunga bila ya uhakika wa futari zinawafika pia wenzao wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

 

 

 

Hawana futari hawana furaha, hasa furaha ya baada ya kufuturu. Si ya watu wazima, si ya watoto. Alasiri watoto hawawezi kwenda kwenye ufuo wa bahari ya Gaza na kurusha vishada.

 

 

 

Mwaka huu Ijumaa ya tatu ya Ramadhani Gaza ilisadifu kuwa siku moja na Ijumaa Kuu. Wapalestina wanaiita Pasaka Id al-Kabir au Id al-Fish, na katika kipindi hiki Wakristo wa Palestina nao pia wamekuwa wakiabudu kwa dhiki na shida kubwa.

 

Israel imewawekea pingamizi Wakristo wa maeneo ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, inayoyakalia kwa nguvu, wasiingie Jerusalem ya Mashariki.  Israel imewazuia pia wasiiadhimishe Pasaka katika Mlima wa Hekalu wanakoamini kuwa Yesu Kristo (Nabii Issa) alikosulubiwa na kuzikwa.

 

 

 

Pasaka ya Wakristo waliobaki Gaza ilikuwa haisemeki kwa ugumu wake.  Wakatoliki wasiozidi mia walihudhuria ibada ya kesha na Misa ya Jumapili ya Pasaka katika kanisa lao la Holy Family (Familia Takatifu) lililo karibu na Hospitali ya Al Shifaa huku wapigano makali yakiendelea nje baina ya wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Hamas.

 

 

 

Watoto Palestina wana mazoea baada ya kufuturu ya kutoka nje na taa za kandili na cheche zao.  Mwaka huu hawanazo. Wala hawana nyimbo na kasida za Ramadhani.

 

 

 

Siku chache kabla ya kuandama mwezi wa Ramadhani, ndege za kivita za Israel zilidondosha vikaratasi vya stihizai katika sehemu za Gaza vikiwaombea Waislamu swaumu yao ikubaliwe, madhambi yao yaghufuriwe na futari yao iwe tamu.

 

 

Lakini tangu waanze kufunga, wakaazi wengi wa Gaza wamekuwa wakifunga na kufungua katika mazingira ya hofu, ya kutwangwa kwa mabomu na makombora. Wamekuwa wakifuturu majani, mashudu na mizizi ya miti.

 

 

Hata hivyo, juu ya masaibu yote yanayowasibu, Waislamu wa Gaza na wa Goma wameukaribisha mwezi huu kwa sababu Ramadhani ni mwezi wa baraka, uvumilivu na matumaini mema.

 

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X/@ahmedrajab

 

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.