Gazeti ambalo halitatoka: Kumbukumbu ya miaka 20

Na Ezekiel Kamwaga

 

WIKI hii nimetimiza miaka 20 tangu nianze rasmi kazi ya uandishi wa habari. Katika muda huo nimefanya kazi katika vyombo tofauti vya habari – kuanzia kampuni ya Habari Corporation iliyonipa kazi ningali kijana mdogo, na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania.

 

Nimeamua nitumie makala hii kuwakumbuka waandishi wenzangu niliowahi kufanya nao kazi ambao sasa wametangulia mbele ya haki. Hawa ni watu niliokuwa na uhusiano nao wa aina tofauti; kuanzia marafiki, mabosi, washauri na watu ambao kwa namna moja au nyingine waliongeza kitu katika maisha yangu kama mwanataaluma na mwanadamu.

 

Nimetengeneza gazeti kutoka kichwani mwangu. Hili ni gazeti ambalo ninadhani kama wangekuwa hai na wangekuwa timu moja, lingekuwa gazeti ambalo kila mtu angetamani kulisoma. Bahati mbaya pekee ni kwamba hilo ni gazeti ambalo halitakuja kutokea. Mwenyezi Mungu na awalaze mahali pema peponi wote nitakaowataja kwenye makala haya.

 

Mhariri Mkuu: Danny Mwakiteleko

 

Nilifahamiana na Danny wakati akiwa Mhariri wa Gazeti la Mwananchi labda miaka 15 hivi iliyopita. Hata hivyo, mimi nilianza kusoma magazeti ningali mwanafunzi wa shule ya msingi na jina lake nilikuwa nalijua kabla sijamuona.

 

Danny alikuwa mhariri aliyejua nini maana ya habari na nini wasomaji wanatarajia kutoka kwenye gazeti. Alikuwa pia na uwezo mkubwa wa kujua vipaji vya waandishi na namna ya kuvitumia. Kikubwa zaidi, Danny hakuwa mtu wa kukasirika. Na kama kulikuwa kuna kitu hakikukaa vizuri mchana, mngekutana mahali jioni baada ya gazeti kutoka ili kukiweka sawa.

 

Nilimfahamu vizuri zaidi wakati alipokuja kuongoza gazeti la Mtanzania. Mara nyingi tulikuwa tunataniana na kucheka. Tulizungumza zaidi nje ya ofisi kuliko ndani ya ofisi. Kama ningekuwa nahitaji mhariri kwenye gazeti langu, ningemchukua Danny pasi na kusita. Alikuwa mtu mzuri sana.

 

Mhariri wa Habari: Godfrey Dilunga

 

Katika waandishi wote wa habari niliowahi kufahamiana nao, hakuna aliyekuwa karibu yangu zaidi kuliko Dilunga. Tulianza kazi ya uandishi tukipishana kwa miezi michache tu – mimi nikitangulia kuajiriwa pale Habari Corporation miezi mitatu au minne kabla yake. Tangu tujuane hatukuwahi kuwa mbali tena.

 

Tulikuwa tunataniana kwamba hatukutakiwa kuwa marafiki. Yeye akipenda Yanga, mimi Simba, akipenda Manchester United, mimi Liverpool. Yeye hakuwa mtu wa mazungumzo mepesi, mimi nikitumia muda mwingi kutaniana na watu. Dilunga alipenda kuwahi kazini, mimi mchelewaji.

 

Dilunga alikuwa mtu mwenye akili na aliyependa kujiongezea maarifa kwa kujisomea na kuandika mara kwa mara. Kwa sababu Danny alikuwa mtu rahimu, Dilunga angemsaidia kuwafanya waandishi wakae kwenye mstari. Kubwa zaidi, Dilunga alikuwa mtu mwadilifu na asiye kigeugeu. Timu ya waandishi iliyo chini ya Danny na Dilunga ingekuwa timu ya maana.

 

Chief Sub: C. Stanley Kamana

 

Mzee Kamana aliwahi kuniponza nikachapwa fimbo nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mgulani jijini Dar es Salaam. Siku moja aliandika makala nzuri kwenye gazeti la Motomoto akilalamikia sera za “Ruksa” za Rais Ali Hassan Mwinyi wakati huo. Chini kabisa ya makala akaandika; “Let us come back to sanity”. Mimi, wa darasa la nne la wakati ule uswahilini, sikujua hata maana ya hayo maneno ya Kiingereza aliyoandika.

 

Nikajikuta siku moja nimeyaandika kwenye insha ya Kiswahili. Nilijua maneno hayo ni ‘swaga’ tu la kumalizia makala. Sasa insha ilihusu masuala ya wakazi wa Kijiji cha Mazae, sijui wapi huko, lakini mwishoni nikamwandikia mwalimu; “Let us come back to sanity”. Nikaulizwa maana yake nini, sikujua. Nikapigwa fimbo mbili au tatu hivi kwa kuandika lugha inayoudhi!

 

Nilimsimulia Mzee Kamana kuhusu tukio hilo katika siku yangu ya kwanza kumwona ofisini pale Sinza. Aliikumbuka makala ile na alicheka sana. Akanichukua chini ya mbawa zake na akaanza kunifundisha kazi na kunipa michapo ambayo sikuwahi kuisikia kabla siasa zetu.

 

Simjui mtu – achilia mbali waandishi wa habari, aliyekuwa na umahiri unaofanana wa lugha zote mbili; Kiswahili na Kiingereza. Kamana ndiye aliyekuwa anatafsiri makala za Kiingereza kutoka magazeti ya nje kwenye gazeti la RAI. Utapenda namna alivyokuwa anapata tafsiri ya maneno kama kasheshe, mtanziko, uraibu na mengine mengi. Yeye hakuwa akitafisiri maneno, alikuwa anatafsiri maana ili ieleweke.

 

Na kama unajiuliza ile herufi C mwanzoni mwa jina lake ilikuwa inasimama badala ya nini, jibu ni jina la Cassius. Kamana angehakikisha gazeti linakuwa na lugha nzuri, sanifu na inayoeleweka kwa wasomaji. Kiswahili kingepata balozi mzuri.

 

Mhariri wa makala: Innocent Munyuku

 

Munyuku na Dilunga walikuwa watu wa rika langu. Munyuku tulikuwa tunaweza kutoka naye Uwanja wa Taifa halafu tusipande gari na kutembea hadi Temeke tukipiga stori. Uzuri wa Munyuku ulikuwa kwamba mngeweza kuzungumza mada yoyote; kuanzia siasa, michezo, burudani na masuala ya uchumi na biashara bila kikomo.

 

Munyuku angefaa kwenye hili gazeti kwa sababu yeye alikuwa mtu wa ‘kitaa’ hasa. Hakuna jambo lilikuwa linatokea au linazungumzwa mtaani halafu yeye halijui. Lakini uwezo wake wa kufahamu mambo mengi ulimfanya awe hazina kwenye gazeti na angeweza kutumika popote na wakati wowote. Kama ingekuwa timu ya mpira, Inno ningemwita kiraka.

 

Mhariri wa makala: Aristariko Konga

 

Nilifahamiana na Konga muda mrefu lakini nilifanya naye kazi muda mfupi wakati tukiwa gazeti la MwanaHALISI. Ari alikuwa mtu muungwana na mpole. Kabla hali yake ya kiafya kuanza kuzorota, alikuwa akijulikana kwa uwezo wake mkubwa wa kuchapa kazi.

 

Wakuu wa Madawati

 

Siasa

 

Mayage S. Mayage

 

Nilianza kumsoma Mayage kabla sijakuwa mwandishi wa habari. Mara ya kwanza kumwona uso kwa uso nilikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Forodhani jijini Dar es Salaam. Nadhani nilikuwa Kidato cha Pili na ndani ya daladala kutoka Tandika kwenda Posta kupitia Chang’ombe nilikokuwa nikiishi.

 

Mayage alikuwa amekaa kwenye kiti na notebook yake iliyoandikwa Mayage S. Mayage. Nilikuwa mbali naye kidogo nilikuwa nilijisogeza mpaka nikamfikia. Nikajikaza na kumuuliza; “Wewe ndiye Mayage wa kwenye RAI?”

 

Akaniambia ndiyo – kwa ile sauti yake yenye mamlaka. Nikamwambia mimi ni mmoja wa wasomaji wake na akanijibu kwa kuitikia kichwa tu. Enzi hizo hakuna televisheni wala mitandao – nazungumzia mwaka 1993 au 1994 hivi na kukutana na mashujaa wako uso kwa uso halikuwa jambo la kawaida sana.

 

Nilipoanza tu kazi pale Habari Corporation, nikaenda kwake kujitambulisha tena. Akalikumbuka hilo tukio na tukacheka pamoja. Mayage alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi na alikuwa anajuana na karibu viongozi wote wa juu wa CCM na upinzani. Ilikuwa ukitaka namba yoyote ya mtu mashuhuri, nenda kwa Mayage na utaikuta.

 

Afya

 

Simon Adolf Kivamwo

 

Sikuwahi kufanya kazi na Kivamwo ofisi moja lakini tulikuwa tukifanya kazi kwa kushirikiana kupitia matukio yaliyokuwa yakitokea. Kwenye kazi zetu za uandishi kuna kazi ambazo mnaweza kufanya kwa kushirikiana na nilifanya naye kazi tofauti.

 

Kivamwo alikuwa mtu mwenye maarifa na aliyekuwa akifikiri nje ya boksi. Hakuwa anawaza kama waandishi wa habari wa kawaida – akiwaza kuhusu kuandika kuomba miradi, kuandika habari kwa upana na alikuwa anapenda kuandika habari za afya – kuna wakati akijikita kwenye habari za ugonjwa wa Ukimwi ambao kuna wakati ulikuwa ndiyo ugonjwa hatari zaidi.

 

Wakati ugonjwa wa Uviko -19 ulipokuwa unang’ata duniani miaka miwili iliyopita, nilimkumbuka Kivamwo. Nikawa nawaza – kama angekuwa hai, Simon angetafuta namna ya kuandika habari za ugonjwa huo katika namna ambayo ingevutia zaidi na kuongeza uelewa wa kutosha wa wananchi kuhusu magonjwa ya aina ya Uviko.

Uchumi na Biashara

 

Muganyizi Muta

 

Kitu cha kuhuzunisha kuliko vyote kuhusu maisha ya mwandishi mwenzangu huyu ni kwamba kifo chake kilikuja wiki moja tu baada ya kunichukua na kunipeleka katika jengo lililokuwa na ofisi mpya alizopanga pale Kinondoni kwa ajili ya kuanza maisha ya ujasiliamali.

 

Alikuwa amejijengea marafiki na wadau wa kutosha katika uandishi wake kiasi cha kufikia kuamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe. Muga alikuwa anajua jinsi ya kuwasiliana na wakubwa kwenye kampuni na kufuatilia mwenendo wa biashara ulivyo kwenye soko. Angekuwa mtu muhimu kwenye dawati la biashara.

 

Habari za Uchunguzi

 

Mkinga Mkinga

 

Mkinga pia anaangukia katika kundi la waandishi wa rika langu ambao tayari wametangulia mbele ya haki. Sikuwahi kufanya naye kazi ofisi moja – lakini tulikuwa tunakutana sana kwenye matukio tuliyokuwa tumetumwa na wahariri wetu kupitia vyombo tulivyokuwa tunavifanyia kazi.

 

Sikushangaa wakati Dilunga aliponiambia Mkinga ndiye aliyemshawishi hasa kuhama Raia Mwema na kujiunga na gazeti la Jamhuri alilokuwa akifanyia kazi Mkinga. Mara nyingi tulikuwa tukikutana nyakati za jioni kuzungumza masuala ya kikazi na maisha.

 

Uzuri wa Mkinga ni kwamba alikuwa anajua kujenga uhusiano mzuri na vyanzo vya habari. Akiwa magazeti ya Citizen na Mwananchi alikuwa sehemu ya uchunguzi wa kihabari ulioibua kashfa kama vile IPTL, Escrow na nyingine chungu nzima zikiwamo za ufisadi katika masuala ya mafuta na mengineyo alipohamia Jamhuri.

 

Kama nilimsifu Mayage kwa kuhifadhi kumbukumbu za wakubwa wote katika zama za analojia, Mkinga ndiye alikuwa mtu wangu wa kupata namba ngumu kuzipata. Mwaka 2017, wakati gazeti nililohariri la Raia Mwema lilipofungiwa na serikali, Mkinga alinipa ofa ya aina yake kumaliza jambo langu; “Nikupe namba ya JPM (Rais Magufuli) uzungumze naye myamalize?”. Sikumjibu, tuliishia kucheka tu. Lakini huyu ndiye Mkinga Mkinga.

 

Michezo

 

Willy Edward Ogunde

 

Kama ilivyo kwa Mkinga na Kivamwo, sikuwahi kufanya kazi na Emmanuel ofisi moja. Lakini huyu ni mtu tuliyekuwa tukifahamiana naye zaidi kwa sababu za kikazi na nje ya kikazi – tukiwa watu wa rika moja pia na hivyo baadhi ya matukio yetu ya nje ya kazi yalifanana.

 

Emmanuel alikuwa mtu makini na aliyejua sekta ya michezo na burudani nje na ndani. Angeweza kufika kazini asubuhi, kwenda kutazama soka uwanjani jioni, kurudi kazini kutengeneza stori na baadaye usiku mkakutana Sigara Club kule Chang’ombe kwa ajili ya kufaidi midundo ya Twanga Pepeta. Kuna siku tulikutana mahali majira ya saa nane usiku na wote tukasingizia tuko ‘kazini’. Nazungumzia miaka 13 au 14 hivi iliyopita.

 

Proof Reader: Idris Luguru

 

Mpaka wakati nakutana naye kwa mara ya kwanza, Mzee Luguru tayari alikuwa na zaidi ya miaka 35 kazini. Yeye ndiye msoma habari wa mwisho gazetini aliyekuwa ananiwekea kiti pembeni ili nimwone wakati akisoma habari yangu na kuondoa makosa ya kisarufi na mantiki yaliyopo.

 

Magazeti mengi ya sasa hayana watu wa aina ya Mzee Luguru – watu wanaofanya kazi ya kupitia habari kwa mara ya mwisho kabla hazijaenda kuchapwa au kurushwa hewani kwa mara ya kwanza. Kama unasoma habari na unaona kuna makosa kadhaa ya ama usahihi au usarufi, ina maana hakuna mtu wa mwisho aliyepewa jukumu la kufanya kazi hiyo.

 

Wakati mwingine makosa hutokea hata kama una ‘Mzee Luguru’ wako, lakini ukiwa naye inapunguza makosa kwa asilimia kubwa.

 

Ningeweza kuandika majina na watu wengine. Na kimsingi, kila ninavyoendelea kuandika kuna majina yananijia ya kutosha. Waandishi watatu ninasikitika kwamba sikuwahi kukutana nao maishani mwangu; John Rutayisingwa, Conrad ‘Kionambali’ Dunstan na Ben R. Mtobwa. Nadhani wangeingia kwenye orodha yangu hii lakini kwa bahati sikuwahi kuwaona wakiwa kazini wala kukutana nao nje ya kazi.

 

Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na baraka, na azibariki roho za marehemu hawa waandishi wa habari walioongeza kitu katika maisha yangu – ndani na nje ya kazi zetu.

 

Amina