Kwa nini Dk. Mpango hawezi kupoa (2)?

Na Ezekiel Kamwaga

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita, nilitaka kuweka historia kidogo ya nafasi ya Makamu wa Rais tangu mwaka 1995. Hii ni kwa sababu, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ndiyo ulikuwa wa kwanza ambapo nafasi ya mgombea mwenza (Makamu wa Rais) ilikuwepo.

 

Kabla ya mwaka 1995 – yaani kuanzia mwaka 1990 kushuka chini, hakukuwahi kuwa na mgombea mwenza. Watanzania walikuwa wakienda kupiga kura kuchagua Rais. Nafasi ya Makamu wa Rais kwanza ilikuwa ni ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) baada ya Muungano wa mwaka 1964 na baadaye ikaja kuwa ya Rais wa SMZ na Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano.

 

Na tangu mwaka 1995, kati ya Makamu wa Rais watano waliowahi kuwapo; hayati Dk. Omar Ali Juma, Dk. Ali Mohamed Shein, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, Samia Suluhu Hassan na Dk. Philip Isdor Mpango, ni Mpango pekee ndiye anatoka Tanzania Bara.

 

Kwa kuangalia takwimu za Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2020, idadi ya wapiga kura wa Tanzania Bara inakaribia kuwa milioni 29 huku wale wa Zanzibar wakikaribia kuwa 600,000. Hii maana yake ni kuwa kwa ujumla, Zanzibar inatoa asilimia mbili tu ya wapiga kura wote.

 

Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapokuwa na mgombea kutoka Tanzania Bara, ina maana anatoka katika eneo lenye takribani asilimia 98 ya kura zote na kwa sababu hiyo chama tawala hakikuwa na sababu ya kuhangaika sana kutafuta mgombea atakayeongeza kura zake Zanzibar tangu mwaka 1995.

 

Kwa vyovyote vile, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakuwa wa kwanza ambapo CCM itakuwa na mgombea kutoka Zanzibar kwa mara ya kwanza kwenye mfumo wa vyama vingi. Tabia ya chama kwenye kampeni na mwenendo mzima wa kampeni inaonekana utakuwa tofauti na ilivyozoeleka.

 

 Ni vizuri nikaweka msingi wa kinachonifanya nifikie kuandika nitakachoandika. Mahali pazuri pa kujenga msingi wa hoja yangu si pengine bali kwenye kuangalia taifa ambalo mfumo wetu wa uchaguzi umeiga wadhifa huu wa Makamu wa Rais – Marekani.

 

Kwenye uchambuzi mbalimbali unaofanyika nchini Marekani kutazama ni yupi alikuwa Makamu wa Rais mzuri na yupi mbovu katika historia ya taifa hilo – na wadhifa huo, vitu kadhaa huangaliwa kwa minajili ya uchambuzi.

 

Nimeona vitu vitatu vinavyojirudiarudia mara kwa mara. Mosi ni uwezo wa Makamu kuongeza kura za Rais, pili ni uwezo wake wa kuchukua madhaifu ya Rais na tatu ni uwezo wa kufafanua na kueleza yale ambapo pengine bosi wake – kwa sababu yoyote ile, hawezi kufanya kwa kiwango hicho.

 

Mfano mzuri wa sababu ya kwanza hupewa Lyndon B. Johnson, aliyekuwa Makamu wa Rais wa John F. Kennedy. Rais Keneddy alijulikana kwa tabia zake za kutetea usawa wa makundi yote – jambo ambalo Wamarekani wengi wa majimbo ya Kusini mwa nchi hiyo hawakupenda kusikia.

 

Johnson aliyekuwa akifahamika kwa ufupisho wa majina yake ya LBJ, alikuwa mzaliwa wa Texas – Jimbo la Kusini mwa Marekani ambalo ni la pili kwa ukubwa na idadi ya watu kwenye taifa hilo lenye uchumi mkubwa duniani.

 

Watafiti wa siasa za Marekani wanamwona Lyndon – aliyekuwa akiheshimika na mwenye ushawishi mkubwa Kusini mwa Marekani, kama mtu aliyesaidia zaidi ushindi wa Kennedy kwenye uchaguzi wa mwaka 1960.

 

Aina ya pili ya Makamu wa Rais ni ile ya Dick Cheney kwa George W. Bush (2000-2008). Watu wengi hulaumu sera mbovu za Rais Bush, hasa Vita ya Irak, kwa kusema zilitokana na ushawishi wa Cheney na wahafidhina mamboleo kama Donald Rumsfeld aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Paul Wolfowitz.

 

Ni kama vile Cheney alikuwa kinga ya Bush. Katika mambo yote mazuri aliyoyafanya bosi wake, jina la Dick halipo. Lakini yanapokuja mambo mabaya, utaona majina ya Cheney na wenzake yanaibuka mara kwa mara. Hii inaweza pia kuitwa kwa jina lingine kama “mnoko” kwenye utawala wa mtu rahimu.

 

Aina ya tatu ni kama ya Albert (Al) Gore aliyekuwa Makamu wa Rais wa Bill Clinton (1992 -2000). Gore na Clinton walikuwa vijana wenye maarifa. Hata hivyo, Gore alijikita kwenye masuala ya tabianchi na kuwa mtetezi namba moja wa masuala hayo ambayo ndiyo kwanza dunia ilikuwa imeanza kuyapa umuhimu iliostahili.

 

Clinton alikuwa mwanasiasa mzuri na mwenye ‘ulimi’ unaovutia. Lakini alitambua kwamba Al Gore alikuwa amejifunza zaidi na kumanya eneo la tabianchi na akamwachia atambe atakavyo. Kwa kufanya hivyo, aliongeza kura kwa wale ambao mijadala ya kila siku ya kisiasa ilikuwa imeanza kuwaboa. Kwa kuweka hoja mpya mezani, Gore alivutia hata wale ambao hawakuwahi kupiga kura kabla.

 

 Mpira mguuni mwa Mpango

 Enzi ya chama kimoja, ilitarajiwa Waziri Mkuu wa Tanzania awe mtu mwenye mojawapo ya sifa hizo tatu – na kama ana bahati zaidi ya moja. Kwa mfano, Rashid Kawawa alifanya kazi ya kumlinda Mwalimu Nyerere vizuri kiasi kwamba Baba wa Taifa alilisema hilo hadharani wakati akitangaza kung’atuka.

 

Edward Sokoine pia alifanya kazi hiyo vizuri wakati wa Nyerere. Katika wakati ambapo uchumi wa Tanzania ulikuwa umeathiriwa baada ya Vita ya Kagera na anguko la uchumi duniani, Nyerere angepata taabu kutawala kama angekuwa na Waziri Mkuu legelege.

 

Kama kuna watu wanalaumu kilichowapata wakati wa operesheni dhidi ya Wahujumu Uchumi, lawama nyingi huelekezwa kwa Sokoine. Ni wazi alikuwa na baraka za bosi wake lakini ilibidi suala hilo alibebe na kulisimamia vizuri, bila kuharibu taswira ya bosi wake wakati huo.

 

Niseme pia kwamba kuna tofauti moja kubwa baina ya Tanzania na Marekani; tofauti hiyo inaitwa CCM. Chama tawala kina nguvu na ushawishi karibu nchi nzima na hakuna mwanasiasa mmoja anayeweza kusema ana nguvu kukizidi chama.

 

Kuna wanasiasa wachache wa Tanzania wanaoweza kujisifu sasa kwamba ukimpa yeye nafasi, basi atakupa kura za mikoa yote ya Kaskazini, Kusini au Mashariki. Kwa hiyo hatuna LBJ wa Kusini mwa Marekani au ilivyokuwa kwa Maalim Seif na Pemba yake enzi zake akiwa CUF na ACT Wazalendo.

Kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, kama ilivyo tangu mwaka 1995, jina la Rais Samia linatarajiwa kuwa kwenye boksi la kura akiwa na Dk. Mpango. Ili Makamu huyu awe na mchango na ushawishi kwa wapiga kura, ni muhimu akawa tofauti na watangulizi wake.

Dk. Mpango kisiasa hatuwezi kusema ana ngome yake inayojulikana kisiasa kwa sababu ya uchanga wake kwenye siasa za ushindani. Hata hivyo, anaweza kutengeneza ngome hiyo kwa kufanya yafuatayo.

Kuongeza kura

Dk. Mpango ni mchumi wa daraja la juu. Kwenye kampeni za urais nchini Marekani mwaka 1992, Clinton alijijengea umaarufu kwa msemo wa “It’s Economy, Stupid” akimaanisha kwamba jambo muhimu kuliko yote kwenye siasa ni uchumi. Sidhani umuhimu wa uchumi kwenye siasa umepungua. Pengine kwa mazingira ya dunia ya sasa, uchumi ni muhimu zaidi.

Kama mtu ambaye amewahi kufundisha masomo ya uchumi na sasa mwanasiasa – kama atataka, Mpango anaweza kuibeba ajenda ya uchumi na kuifanya ya kwake. Anachohitaji tu ni kujenga taswira ya mtu anayejua anachokizungumza na kuzungumza ukweli.

Kama mara kwa mara atajikita kwenye masuala yanayowagusa watu kiuchumi kama bei za bidhaa, ukosefu wa ajira na kurahisisha misamiati migumu ya kiuchumi katika lugha nyepesi na kutoa matumaini kwa watu, Mpango atakuwa anaongeza kura kwa Rais.

Katika mazingira haya ambapo mgombea urais atatoka Zanzibar, ni muhimu kwa Makamu kutoka Bara kusimamia kitu kitakachoongeza thamani kwenye Urais. Haitasaidia kwake kukaa kimya na kuenenda kama ilivyokuwa kwa akina Shein.

 

Ni muhimu pia kwa Mpango kuonesha tabia tofauti na Rais. Kama Rais ni mtu muungwana na rahimu, Mpango anatakiwa kuonyesha picha tofauti. Zamani, kazi hii ingefanywa na Waziri Mkuu lakini kwa jinsi ukweli halisi ulivyo kwenye mfumo huu wa kuwa na mgombea mwenza, jina la Waziri Mkuu wa sasa halitakuwepo kwenye sanduku la kura la kuchagua Rais na Makamu wake.

 

Nimekuwa nikiamini kwamba mojawapo ya sababu ya kumpa Samia nafasi ya mgombea mwenza mwaka 2015 ilikuwa ni utulivu wake kisiasa – tofauti na aliyekuwa mgombea urais, hayati John Magufuli. Kama Magufuli alikuwa moto, Samia alipewa nafasi hiyo kwa sababu alikuwa maji. Kama Rais Samia ni Yin, Mpango anatakiwa kuwa Yang.

 

Kama Rais Samia amesema yeye hawezi kufokea watu hadharani kwa vile si tabia yake – lakini Watanzania wakawa wanatamani viongozi wanaofokafoka, hilo ni pengo linalotakiwa kuzibwa na Dk. Mpango.

 

Sauti ya Mpango si kali kama ya Magufuli lakini, kama tulivyojifunza wakati wa Sokoine, unaweza kuwa na sauti ya chini lakini ukawa mkali. Inawezekana kabisa kuwa kundi la Watanzania wanaopenda Rais anayefokafoka ni kubwa kuliko tunavyodhani.

 

Watanzania, kwa ujumla wao, wanapenda viongozi wa juu wanaotetea wanyonge, wasio washaufu, watu wa watu, wasiotukuza utajiri, wasiohusishwa na ufisadi na wale walio tayari kuwaambia watu ukweli hata kama ni mchungu kiasi gani.

 

Makamu wa Rais wa Tanzania ya kuelekea 2025, anatakiwa si tu kuwa na walau mojawapo ya sifa hizo, lakini Watanzania wanatakiwa kumwona na kumfahamu kwa sifa hiyo. Ikiwezekana, wamfahamu namna hiyo wakati wanaenda kupiga kura tarehe isiyojulikana mnamo Oktoba 2025.

 

Kupoa si sifa nzuri kwa Makamu wa Rais wa Tanzania kwenye uchaguzi ujao. Katika changamoto hizo zinazoikabili nchi yetu na dunia kwa ujumla, Philip Isdor Mpango ana kete za kusukuma.

Kwa vyovyote vile, hatakiwi kupoa.

Mwandishi wa makala haya ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi aliyefanya kazi hiyo ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 20. Ndiye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Dunia.