Kutawaliwa na dikteta mwenye vichwa zaidi ya kimoja

Caption: Viongozi wa juu wa CHADEMA katika picha ya pamoja wakati wakitangaza Operesheni Ukuta mnamo Julai mwaka 2016. Ukuta ndiyo ilikuwa jitihada za awali kabisa za vyama vya upinzani kupinga zilizoanza kuonekana kama dalili za awali za udikteta kwenye siku za mwanzo za utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

 

BARAZANI KWA RAJAB

Na Ahmed Rajab

NCHINI Haiti watoto wadogo walio watundu, wakitaka kutishwa, huambiwa kwamba wataitiwa “Tonton macoute” (Mjomba gunia). Huambiwa kwamba mjomba huyo atawatia kwenye gunia ende akawale kwa chakula cha istiftahi, cha kufungulia kinywa.

Utukutu huyayuka mara tu watoto hao wanapotajiwa Tonton macoute. Huliogopa zimwi wasilolijua litaloweza kuwala likawamaliza.

Kuna kipindi katika historia ya Haiti ambapo hata watu wazima walikuwa wakiharisha walipokuwa wakitajiwa Tonton macoute. Hayo yalitokea wakati Dk. Francois Duvalier alipokuwa Rais wa nchi hiyo (kuanzia Oktoba 22, 1957 hadi Aprili 21, 1971).

Duvalier, aliyekuwa maarufu kwa jina la “Papa Doc”, alikuwa na kikosi chake cha usalama ambacho watu mitaani wakikiita Tonton macoute. Kilikuwa kikosi cha watesaji. Kikitisha. Mateso yao yalikuwa hayasemeki.

Baada ya kufariki Papa Doc na urais wa Haiti kurithiwa na mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka 19, Jean-Claude Duvalier, maarufu kwa jina la “Baby Doc”, watesaji wa Tonton Macoute waliendelea na ukhabithi wao.

Ukatili wa aina hiyo umeshuhudiwa kwingi duniani katika nchi zilizokuwa zikitawaliwa na madikteta na zile za madikteta mamboleo. Umeonekana Ujerumani wakati nchi hiyo ilipokuwa chini ya uongozi wa Adolf Hitler. Ulikuwepo pia Italia wakati wa Benito Mussolini.

Wengine wataukumbuka ukatili huo wakati ule uliokuwa Muungano wa Kisovieti ulipokuwa chini ya Josef Stalin au Romania ilipokuwa chini ya Nicolai Ceausescu.

Viongozi wote hao walikuwa madikteta, wakisimamia tawala za kimabavu, zenye kutumia nguvu na zilizokuwa zikizikiuka haki za binadamu. Wengine duniani waliokuwa wakiongoza tawala za aina hizo ni pamoja na Saddam Hussein wa Iraq, Suharto wa Indonesia, Francisco Macias Nguema wa Equatorial Guinea na mpwa wake Rais wa sasa Teodoro Obiang Nguema Mbasogo pamoja na Jean-Bédel Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, aliyesilimu kwa muda akajipa jina la Salah Eddine Ahmed Bokassa.

Katika ukanda wa Afrika ya Mashariki kulikuwako tawala za mabavu nchini Kenya chini ya Daniel arap Moi, Uganda chini ya Jenerali Idi Amin Dada na Zanzibar wakati wa miaka minane ya utawala wa Sheikh Abeid Karume. Viongozi wote hao watatu wa Afrika ya Mashariki waliwatesa wapinzani wao na hata wale wasiokuwa wapinzani wao lakini waliokuwa wakiwatiliwa shaka tu.

Mateso waliokuwa wakifanyiwa wafungwa wa jela kuu ya Zanzibar hapo Kiinua Miguu , hasa katika ile sehemu iliyokuwa ikiitwa “Kwa Ba Mkwe”, hufafanishwa na waliokuwa wakifanyiwa wafungwa wa Haiti na Tonton macoute.

Kuishi katika nchi yenye utawala mbovu, tena wa kimabavu, mara nyingi huwa ni sawa na kuishi katika jahanamu. Kuna mambo yenye kufanana katika nchi zenye tawala za kimabavu zinazoongozwa na madikteta. Utadhani kama madikteta wana ubongo mmoja. Na kwamba wote wanatabaruku kwenye ubongo huo huo mmoja.

Wayatendayo huwa ni yayo yayo. Wayapendao huwa ni hayo hayo na yanayowachukiza huwa ni hayo hayo. Kwa mfano, tawala za aina hizo huwa hazivumilii mawazo mbadala. Wanaothubutu kutoa mawazo yasiyokubaliana na ya mtawala wa kimabavu hujikuta wanashughulikiwa na vyombo vya dola kwa kuteswa na kufanyiwa mambo maovu.

Hivyo vyombo vya dola vyenyewe vinakuwa vinatumiliwa, kinyume na Katiba ya nchi, kuyakidhi mahitaji ya mtawala aliye dikteta.

Kwa hakika, vyombo hivyo, vikiwa pamoja na idara ya polisi na mahakama huwa havina maana kwa sababu kazi zao zinakuwa ni kutekeleza yatakiwayo na kiongozi. Tena kinyume na sheria. Kwa hivyo, hata Katiba ya nchi huwa haina maana kwa sababu kila mara inakuwa inavunjwa bila ya mtawala kujali kwamba anakwenda kinyume na Katiba aliyokula kiapo kuilinda.

Kiapo cha kuitii na kuilinda Katiba pia huwa hakina maana kwa sababu hakiwi cha dhati, hakiwi cha kweli.

Katika nchi hizo zenye utawala wa kimabavu mfumo wa siasa za vyama vingi huwa ni wa kujidai tu. Mara zote dikteta huwa hapendi kuambiwa afanye nini seuze kuambiwa kweli kwamba amekosea. Hujiona kuwa yeye ndiye mwenye hatimiliki ya ukweli. Akiamini hivyo, hutaka anachokisema kiwe kinatekelezwa. Kwa hivyo, tamko lake huwa ni amri na amri yake huwa ni sheria.

Ijapokuwa katika mfumo wa kidikteta mtawala wa jamhuri huitwa “Rais”, kwa hakika yeye hujifanyia mambo kama ni mfalme. Hujifanyia atakavyo. Bunge lenye kuwawakilisha wananchi halifui dafu kwa Rais anayeamua atakavyo. Mambo huwa mabaya zaidi pale wabunge wa chama kinachotawala wanapojigeuza na kuwa vibaraka wa Rais.

Katika hali kama hizo wananchi, kwa jumla, huwa hawamuamini tena Rais na ndio maana Rais huwatumia wabunge wa chama chake kupambana na wapinzani walio bungeni.

Wabunge wote hao, wa chama cha Rais na wa upinzani, ni wawakilishi wa wananchi. Kwa mujibu wa Katiba wanatakiwa wawe wanayapigania maslahi ya wananchi na ya taifa zima. Lakini katika tawala za kidikteta, Rais huwategemea wabunge wa chama chake wawe wanamuunga mkono yeye na serikali yake.

Bunge linatakiwa liwe madhubuti lakini wakati huohuo liwe huru. Lisiwe kila mara linaelemea upande wa Serikali na kuzivuruga nia njema za wabunge wa upinzani. Lisiwe kichekesho kama, kwa mfano, linavyoonekana siku hizi Bunge la Tanzania mara kwa mara.

Ni wajibu wa wabunge wa chama kinachotawala na wabunge wa upinzani kulifanya Bunge liheshimiwe na wananchi. Wala si jambo la busara kulifanya Bunge liwe linaridhia tu kila akitakacho Rais.

Ubaya wa utawala wa kidikteta ni kwamba daima daima utawala wa aina hiyo huwa juu ya sheria. Chochote utachokisema wewe raia wa kawaida au utachokifanya ambacho utawala wa mabavu usichokipenda kitakufikisha korokoroni.

Hali ya mambo kwingi Afrika imebadilika tangu miaka ya mwisho ya 1980 pale nchi nyingi za Kiafrika zilipokuwa mbioni kuukumbatia mfumo wa demokrasia. Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba siku za utawala wa kimabavu katika Afrika zimekwisha na kwamba Afrika haitokubali tena kugubikwa na giza la utawala muovu usiowajibika.

Taifa haliwezi kuwa na sifa ya kidemokrasia ila ikiwa litafanya mambo fulani fulani. Kwanza kabisa litabidi liugeuze mfumo wa kisiasa na kuufanya uwe bora.

Jengine la kufanywa ni kuyageuza mahusiano baina ya Rais na wananchi na kuyafanya yawe mema. Ili papatikane mahusiano ya aina hiyo wananchi wanahitajika waweze kuwa na imani na Rais na wayaamini anayoyafanya.

Kuna mhimili mmoja wa dola ulio muhimu sana kwa utawala wa kisheria. Huu ni mhimili wa mahakama. Nchi au taifa lolote liwe halitoweza kuwa na utawala wa kisheria endapo haki haitotendeka mahakamani, endapo mahakama hayatokuwa huru na yakawa yanapendelea upande mmoja.

Mfumo wa kisheria unapaswa uwe wa haki na usiopendelea, uwe wenye kuheshimu haki za binadamu na kuwapa wananchi haki zao na uhuru wao wanaohakikishiwa na Katiba.

Wananchi wawe na uhuru wa kufikiri, wa kusema, wa kutoa mawazo yao hata ikiwa ni ya kumkosoa Rais, wa kukusanyika, wa kuandamana hata kama ni kwa sababu ya kumpinga Rais au serikali yake au sera zake.

Kadhalika ni muhimu kwamba kila baada ya muhula fulani pawe panafanywa uchaguzi ulio huru, wa kweli na wenye kuleta mageuzi ya uongozi. Sambamba na hayo lazima pawepo ushindani baina ya vyama vya siasa. Ushindani huo uwe wa kuheshimiana na wa kuvifanya vyama vyote vya siasa viwe vinatendewa haki na wenye kutawala bila ya upendeleo wowote.

Hivi sasa hatutokosea tukisema kwamba nchi kadhaa za kiafrika badala ya kusonga mbele zimerudi nyuma katika kuhakikisha kwamba mfumo wa demokrasia na utawala bora unashamiri. Viongozi kadhaa wakishauonja utamu wa uongozi huanza kupanga njama za kumwezesha aselelee madarakani. Ndipo huzuka vitimbakwiri vinavyompandisha mbinguni Rais na kuanza kushauri kwamba anafaa aendelee kupindukia mihula yake aliyowekewa na Katiba. Vitimbakwiri hivyo hutoa shauri hilo kwa maslahi yao au ya vizazi vyao.

Afrika pia imerudi nyuma katika siasa za kimataifa. Usemi wake katika masuala ya kimataifa umefifia. Kwa sasa si nchi za kiafrika, moja moja, wala si bara zima la Afrika, kwa pamoja, lenye sauti yenye kusikilizwa wakati yanapojadiliwa masuala yanayotafutiwa ufumbuzi katika medani ya siasa za kimataifa.

Kama nilivyokwishagusia, kuishi katika nchi yenye utawala wa kidikteta ni kama kuishi katika jahanamu. Dikteta huwa halioni raha mpaka liwatese wananchi na wananchi wote wasalimu amri kwake, wawe wakifanya litakavyo yeye bila ya kunung’unika au kulalamika.

Kila ninaposikia madhila wanayoyapata wenye kuishi katika nchi zenye kutawaliwa kimabavu, kiasi cha kwamba wanajihisi kuwa kama wafu wanaoishi katika jahanamu, basi mimi humfikiria Cerberus.

Katika mithiolojia au visasili vya Uyunani, Ugiriki ya Kale, Cerberus ni jibwa kubwa la kuwindia lenye vichwa zaidi ya kimoja. Kazi yake ni kulinda milango ya jahanamu ili kuwazuia wafu wasitoroke. Na hivyo ndivyo ilivyo midikteta.

Kwa hakika, wao ni wabaya zaidi kumshinda Cerberus kwa sababu wao huwafanya wananchi wenzao wajione kama wafu wanaoishi katika hali wanazoziona kuwa kama ni za jahanamu ya duniani. Isitoshe, wanawazuia wasiweze kufurukuta na kujitoa katika madhila na masaibu yaliyowafika.
Makala haya yalitumika kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Kiswahili la kila wiki la Raia Mwema mnamo Juni mwaka 2017.
Mwandishi ni mwanahabari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 50 – akiandika katika vyombo vya nchini na kimataifa. Kwa sasa ana makazi yake jijini London, Uingereza. Anapatikana kupitia; aruapepe: aamahmedRajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab