Mizengwe dhidi ya Maalim Seif na Dkt. Salim

Picha: Maalim Seif Sharif Hamad na Dk. Salim Ahmed wakizungumza wakati Salim akiwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge la Katiba.

 

Na Ahmed Rajab

 

NILIWAHI kuandika kuhusu mazungumzo yangu na Mwalimu Julius Nyerere alasiri ya tarehe 5 Desemba, 1994, chumbani kwake katika hoteli ya Intercontinental, jijini Nairobi. Ilikuwa miezi saba kabla ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumchagua mgombea wake katika uchaguzi wa urais wa mwaka 1995.

 

Mwalimu aliniuliza watu wanasemaje kuhusu mchakato huo, nami nikamjibu: “Wanasema una mgombea wako.”

 

“Nani?”

 

“Salim,” nikamjibu, nikimkusudia Dkt. Salim Ahmed Salim.

 

“Kwa nini?” Mwalimu aliendelea kunisaili.

 

“Kwa sababu wanasema ni mtoto wako.”

 

Mwalimu aliruka na akanambia: “Wote watoto wangu, hata Seif.”  Alikuwa na maana ya Maalim Seif Sharif Hamad.

 

“Nani kamjenga Seif?”

 

“Wewe,” nilimjibu kama alivyotaka nimjibu.

 

“Tena!” Akasema.

 

Niliikumbuka sehemu hiyo ya maongezi yetu yaliyokuwa marefu baada ya kuzinduliwa makavazi ya mtandaoni ya Dkt. Salim tarehe 30, Septemba. Nilikumbuka pia kuwa Marehemu Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, alizaliwa mwezi huu wa Oktoba, tarehe 22, mwaka 1943, miezi tisa baada ya Salim.

 

Si siri kwamba kuna kipindi ambapo Nyerere akiwapenda wote wawili, Salim na Maalim. Na wao wakimpenda, wakimhusudu hasa.  Lakini kwa Seif mapenzi yake juu ya Zanzibar yaliyapiku mapenzi yake juu ya Nyerere.  Mwishoni mwa uhai wake, Nyerere naye akimuona Maalim kuwa mkorofi.

 

Salim, kwa upande wake, aliendelea kumtetea Nyerere kwa dhati. Kwa Seif, Nyerere alikuwa chanzo cha balaa lote la Zanzibar. Hiyo ni tofauti kubwa, na ya msingi, baina yake na Salim.

 

Makala haya ni simulizi ya uhusiano wa wana hawa adhimu wa Zanzibar.  Hawa ni watu ambao nikiwajua tangu ujanani mwetu. Salim nikimjua zaidi kushinda Maalim kwa vile sote tulikuwa wafuasi wa Abdulrahman Babu, kiongozi wa chama cha Umma Party kilichokuwa kikifuata itikadi ya Umarx.

 

Kwa hakika, kwa muda mrefu nimekuwa msiri wake Salim. Siri ya kuwa msiri wa mtu ni kukigeuza kifua chako kiwe kaburi.  Kaburi la kuyazika yote ambayo hakutaka wengine wayajue. Kwa hivyo, kuna mengi ya Salim ambayo itabidi niyabanie na mengine ambayo lazima nizikwe nayo. Niliyoyazika katika kaburi la kifua nitazikwa nayo katika kaburi la udongo.

 

Salim ni Rais ambaye Tanzania haijajaaliwa kumpata kwa sababu ya majungu yaliyopikwa dhidi yake na baadhi ya viongozi wenzake wa Zanzibar na wa Tanganyika ambao siku mbili hizi bila ya kuona haya wamekuwa safu ya mbele wakimshangilia.

 

Maalim naye ni Rais ambaye Zanzibar haijajaaliwa kumpata kwa sababu ya vitimbi vya mahasimu wake, miongoni mwao wakiwa wale wale waliomchimba Salim. Nao pia siku hizi wako mbele wakimsifu Maalim kwa mengi. Unafiki wa kisiasa ndio huo. Hauna kikomo. Hauoni haya, wala karaha, hata kama ukijisuta.

 

Salim na Maalim waliwahi kuwa wamoja halafu wakafarikiana, lakini kiungwana, kistaarabu.  Hawakununiana; isipokuwa kila mmoja alishika njia yake wakawa hawawasiliani.

 

Hatimaye walishikana tena — ingawa misimamo yao, hasa kuhusu Zanzibar, haikuwa mimoja.  Mara ya kwanza kuwaona waungwana hawa wakiwa pamoja ilikuwa London kwenye hoteli ambayo siku hizo ikiitwa The Hyde Park Hotel na siku hizi inaitwa Mandarin Oriental Hyde Park.  Wakati huo, Salim alikuwa waziri mkuu wa Tanzania na Seif alikuwa waziri kiongozi wa Zanzibar.  Niliwakuta wakiwa wamejawa na furaha na nyuso zilizokunjuka huku wakiniperemba.

 

Kilichonijia mwanzo kichwani mwangu ilikuwa historia ya hiyo hoteli iliyo katikati ya eneo la Knightsbridge, moja ya maeneo ya kibwanyenye jijini London.  Nilibahatika kwa miaka michache katika mwongo wa 1960 kuishi nyumba namba 48 Brompton Square, mwendo wa miguu wa kama dakika saba kuifikia hoteli hiyo. Kwa hivyo, hiyo hoteli haikuwa ngeni kwangu.

 

Niliwahi pia kuisikia mikasa ya hotelini humo iliyowahusu vigogo wa Uingereza wakiwemo wafalme, aliyekuwa waziri mkuu Winston Churchill na wengine.

 

Nilichowaambia Salim na Maalim ni kwamba kwa kushukia hoteli hiyo walifuata nyayo za sultani Seyyid Khalifa bin Haroub, babu yake Seyyid Jamshid bin Abdallah bin Khalifa, aliyepinduliwa 1964.

 

Alipoizuru London mara ya mwisho mwaka 1960 Seyyid Khalifa alifikia hoteli hiyo na kuna picha aliyopiga na ndugu wawili wanafunzi wa Kizanzibari, Ali Adnan, ambaye miaka michache baadaye tulifanya kazi pamoja katika Idhaa ya BBC na kaka yake Taher Adnan, mwanafunzi aliyekuwa akisomea shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Oxford.

 

Hotelini humo pia ndipo mtangazaji mashuhuri wa Kizanzibari, David Wakati, alipomhoji Seyyid Khalifa na mahojiano yao yakarushwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC.

 

Baada ya kuwapa kidokezo hicho cha historia, tukaanza kuizungumza Zanzibar yetu.  Nilikuwa na matumaini kuhusu mustakbali wa Zanzibar nikiamini kwamba mipini ya uongozi ikiwa mikononi mwao, watendaji wakuu wa serikali mbili, Zanzibar itaonewa huruma na haitokabwa na muhafidhina.  Nikitumai kwamba Salim na Maalim kwa namna walivyokuwa wakishirikiana wangeweza kuleta mageuzi ya maana nchini mwetu.

 

Kosa langu lilikuwa ni kutoitambua mizengwe ya mfumo wa utawala wa Chama kimoja kama ule wa CCM ya miaka ile.

Niliona dalili pale pale hoteli kwani niliposhauri hatua fulani ambayo Maalim angeweza kuchukua dhidi ya baadhi ya wakorofi wa Zanzibar, wote wawili, walinipinga.

 

Salim na Maalim walitoka mbali; nadhani kwa Upemba wao wakijuana kwa vilemba.  Ingawa Salim alizaliwa Unguja kwenye hospitali ya Mwembeladu, alipokuwa mchanga alilelewa kwao Makombeni, Mkoani, Pemba. Aliporudi Unguja, Upemba ulimvaa hata lafudhi yake ilikuwa ya Kipemba.

 

Salim na Maalim walikutana mara ya kwanza katika skuli ya sekondari ya King George VI iliyo Unguja. Salim alikuwa mbele ya Seif kwa mwaka, na Seif alikuwa mbele yangu kwa miaka miwili.

 

Siku hizo hawakuwa na maingiliano ya karibu. Seif alikuwa zaidi akichanganyika na wanafunzi wenzake kutoka Pemba, hasa wale waliokuwa wakiishi kwenye dakhalia au bweni kule Beit el Ras.

 

Wakati ule wa miaka ya mwanzo ya mwongo wa 1960 jina la Salim likitajwa sana Beit el Ras katika rubaa za kisiasa.

 

Tulipokuwa skuli Seif alikuwa mwanaharakati wa siasa za kiwanafunzi lakini Salim tayari alikwishaibuka kuwa mwanasiasa wa kitaifa. Nakumbuka safari moja alitoroka skuli akenda Cuba kuhudhuria mkutano.

 

Baada ya mapinduzi ya 1964, Rais Abeid Amani Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar alimteua Salim, akiwa na miaka 22, awe balozi wa Zanzibar nchini Misri. Uteuzi huo ulithibitisha jinsi Salim alivyokuwa amepevuka kisiasa, hasa katika ulingo wa siasa za kimataifa.  Baada ya kuundwa Muungano, Nyerere hakumuondosha Salim Cairo na baadaye akamteua awe balozi India, China na, hatimaye, katika Umoja wa Mataifa, jijini New York.  Huko ndiko nyota yake ilipozidi kung’ara. Maisha ya Salim yakawa zaidi nje ya nchi yake.

 

Huku nyuma, Seif alimaliza masomo hadi kidato cha sita na baadaye akawa mwalimu, akisomesha skuli Unguja na hatimaye Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro, Pemba.  Aliuacha ualimu alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya shahada ya kwanza.

 

Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu, Rais wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, alimteua serikalini na baadaye akamteua waziri wa elimu na kumtumbukiza katika dimbwi la siasa.

 

Mwaka 1982 Maalim na Salim wakakutana katika sekretarieti ya CCM walipoteuliwa wakuu wa idara za chama — Salim akiongoza idara ya mambo ya nje na baadaye ya ulinzi na usalama na Maalim idara ya mipango na uchumi.  Mwenzao wa tatu alikuwa Salmin Amour.  Wakiwa katika sekretarieti Salim na Maalim walishirikiana kumzuia Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, asiwachukulie hatua wale aliowashutumu kuleta vurugu na migawanyiko Zanzibar mnamo 1982/1983.

 

Mwaka huo wa 1982 ndipo lilipochomoza lile kundi lililojiita “Frontliners” (Wa mstari wa mbele) lililokuwa likichuana na lile la “Liberators” (Wakombozi).  Mapande hayo yalikuwa ni ya wanasiasa kutoka Zanzibar waliokuwa katika ngazi za juu za uongozi wa CCM.

 

Salim na Maalim walikuwa katika kundi la “Frontliners”.  Mahasimu zao waliojiita “Wakombozi” wakitaka kuirejesha Zanzibar kwenye utawala wa kimabavu. Wakiwaita “Frontliners” mahizbu, yaani wafuasi wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP, maarufu Hizbu) cha serikali iliyopinduliwa 1964.  Miongoni mwa wenzao kina Salim alikuwa Adam Mwakanjuki, mfuasi kindakindaki wa chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).

 

Matukio mawili ya 1984 yaliyaathiri majaaliwa ya Salim na Maalim:  kuangushwa Jumbe Januari mwaka huo na kufariki waziri mkuu Edward Sokoine katika ajali ya gari, mwezi wa Aprili.  Salim aliteuliwa waziri mkuu na Maalim waziri kiongozi. Salim na Maalim wakiwa watendaji wakuu katika serikali mbili walishirikiana vizuri sana. Hivyo ndivyo walivyokuwa nilipokutana nao London.

 

Mwaka 1985 pakazuka sokomoko la nani atayemrithi Nyerere baada ya kung’atuka. Mwezi Novemba, 1985 niliandika makala marefu kwenye jarida la Africa Events, chini ya kichwa cha maneno “A Tale of Two Presidents” (Hekaya ya Marais Wawili). Makala hayo ndo yaliyoyataja kwa mara ya kwanza makundi ya “Frontliners” na “Liberators”.

 

Watu watatu waliibuka kutaka kumrithi Nyerere — Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu Rais wa Tanzania, Rashidi Kawawa, katibu mkuu wa CCM na Salim Ahmed Salim, waziri mkuu.

 

Nyerere alitaka Salim amrithi.  Aliwaeleza Kawawa na Mwinyi. Wote walimkubalia. Kawawa akajitoa kwenye mchuano.  Mwinyi alikuwa kigeugeu. Mara akionekana kumpongeza Salim, mara akisikika akisema kwamba yeye si wa kuomba omba lakini akipewa [urais] hatoukataa.

 

Ilikuwa wazi kwamba “Liberators” (Wakombozi) wakimshajiisha Mwinyi asijitoe kwenye mchuano.  Pia wakitaka Idris Abdulwakil, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, agombee urais wa Zanzibar.

 

Salim alianza kujitenga na “Frontliners” baada ya 1985. Mahusiano yao yalikatika Maalim alipofukuzwa CCM mwaka 1988 na kuwekwa kizuizini mwaka 1989.  Salim naye alihamia Addis Ababa, Ethiopia, akiwa katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

 

Wadhifa huo mpya ulimpa fursa ya kuwasiliana na Maalim pamoja na Amour akiwanasihi wapunguze ukali katika hotuba zao.  Salim akihisi hotuba hizo zikipandisha sana jazba za kisiasa na akiona kulikuwa na hatari.

 

Mahusiano ya kidugu baina ya Salim na Maalim yalirudi 1996 Maalim alipopita Addis Ababa akiwa katika safari za kuihamasisha jumuiya ya kimataifa ichukuwe hatua za kuufumbua mgogoro uliozuka Zanzibar baada ya uchaguzi wa 1995 ambao matokeo yake yalibadilishwa na Dkt. Salmin Amour akatangazwa mshindi badala ya Maalim.

 

Kwa mujibu wa Maalim walipokutana Addis Ababa alimwambia Salim kwamba Zanzibar ilimfanyia mengi Salim lakini yeye hajaifanyia kitu Zanzibar.  Salim alijiteteta kuwa alijitahidi lakini pia alikiri kwamba pengine angeweza kufanya zaidi.

 

Kuanzia hapo kila walipopata fursa wakikutana.  Salim akihisi kwamba yeye binafsi asingekubalika kuwa mpatanishi huru katika mgogoro wa Zanzibar. Kwa hivyo, alizungumza na Chifu Emeka Anyaoku, katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola na mwananchi wa Nigeria, awe msuluhishi. Na yeye Salim aliingilia mgogoro wa Nigeria ambao Anyaoku asingeweza kuwa mpatanishi.

Baada ya Salim kumaliza muda wake OAU na kurudi Tanzania, ikawa pia wanakutana Dar es Salaam au Zanzibar. Walikuwa wakialikana chakula nyumbani kwa mmoja wao na hivyo kupata nafasi ya kubadilishana mawazo.

 

Salim alisikitishwa sana yalipovunjika mazungumzo ya Muafaka wa Tatu yaliyokuwa yakifanyika Bagamoyo lakini alitiwa moyo na akaunga mkono kwa dhati Maridhiano ya Zanzibar yaliyofikiwa 2009. Alikuwa akimshajiisha Maalim aendelee na juhudi za kuwaunganisha Wazanzibari kwa sababu akiamini ndiyo njia pekee ya Zanzibar kusonga mbele.

Salim na Maalim ni waumini wakubwa wa haja ya Wazanzibari kuwa na umoja. Salim aliligusia hilo alipokuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Ali Sultan Issa na Maalim Seif. Alisimulia pia jinsi Hassan Nassor Moyo aliyekuwa katika kundi la “Liberators” lililowapiga vita Maalim na Salim kwenye uchaguzi wa 1985, alivyomfuata Salim na kumuomba radhi kwa siasa chafu walizofanya dhidi yake na akaahidi kumuunga mkono 2005. Na ni Moyo huyo huyo ambaye baadaye aliungana na Maalim kupigania Zanzibar irejeshewe Mamlaka Kamili.

Mwaka 2013 Salim aliungana na Jaji Mstaafu Joseph Warioba na Makamishna wengine wachache wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenda kusikiliza maoni ya Maalim, wakati huo akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Maalim alizungumza kinaga ubaga kuhusu Zanzibar inavyokandamizwa kwenye Muungano na akataka Muungano ubadilishwe kutoka ule wa Kikatiba uwe wa Mkataba. Hatimaye, Tume hiyo ilipendekeza paanzishwe Shirikisho la Serikali Tatu.

Ni wazi kwamba mahusiano ya Salim na Maalim yalijengeka juu ya kuheshimiana hata pale walipotofautiana.

Awali Maalim aking’ara zaidi kushinda Salim ndani ya CCM, lakini baada ya yeye na wenzake kufukuzwa kutoka kwenye chama hicho ndipo Salim alipopanda haraka haraka.

 

Si kwamba Salim hakuwa na uwezo. Hasha.  Inamkinika kwamba labda Nyerere alihisi angeweza kumtumia Salim kupunguza ushawishi wa Maalim.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; /X@ahmedrajab

 

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.

 

 

 

 

 

 

 

.

 

.