Wasaliti ni wenye kupinga Muungano wa Mkataba  

Picha: Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.

 

 

Na Ahmed Rajab

 

MENGI yameandikwa na mengi yataendelea kuandikwa kumhusu Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa mwanzo na wa pekee wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambaye Aprili, 26, mwaka 1964 alikubali kuiunganisha nchi yake na ile ya Tanganyika.

 

Hadi sasa walioandika kumhusu Karume ni waandishi wa habari, wanahistoria na wataalamu wa fani ya sayansi ya siasa. Waandishi wa riwaya hata wa riwaya sahili na wa tamthilia bado hawajajitokeza uwanjani kumuandika Karume.  Sitoshangaa pakitokea magwiji wa tanzu hizi mbili za fasihi watakaoamua kumtoa ukumbini Sheikh Karume kwa kumjadili na kumzungumza ama katika riwaya za kisiasa au katika michezo ya kuigiza.

 

Pengine tutaweza kupata taswira iliyokamilika ya Sheikh Karume endapo atachambuliwa katika fani zote hizo mbili au mojawapo ya fani hizo kwani hutokea simulizi za kubuni zikaukaribia sana ukweli kushinda simulizi za kitaalamu, ziwe za wanahistoria au za wataalamu wa sayansi ya siasa.

 

Kwa upande mwingine, hutokea pia simulizi za wanahistoria au za wataalamu wa sayansi ya siasa zikawa sawa na za kubuni kwa vile huandikwa ama kwa kutouzingatia au kwa kuupotosha ukweli.

 

Waandishi wa riwaya au wa tamthilia watakuwa na uwanja mkubwa wa kuandika mengi kuhusu nyanja mbalimbali za Ukarume na Karume — namna alivyoishi yeye mwenyewe binafsi, jinsi alivyoitawala nchi na maingiliano yake na Mwalimu Julius Nyerere.

 

Baadhi yatawachekesha watu waumwe na mbavu; mengine yatawahuzunisha na kuwafanya watokwe na machozi.  Bila ya shaka, watakaoandika riwaya au tamthilia kumhusu Karume watakuwa na fursa ya kuyaanika mema na mabaya yake.

 

Fursa nyingine watayokuwa nayo ni ya kunukuu matamshi yake. Kati ya misemo maarufu ya Karume inayokumbukwa sana na Wazanzibari siku hizi ni ule usemi wake wa kuulinganisha Muungano wa Tanzania na koti.  “Muungano ni kama koti tu, likikubana unalivua,” aliwahi kusema.

 

Tunavyofahamu ni kwamba kabla ya mauti kumkuta Sheikh Karume alikuwa na azma ambazo lau angelizitimiza basi hii leo Muungano huo ungekuwa na sura nyingine kabisa. Miongoni mwa mipango aliyokuwa nayo ni kuifanya Zanzibar iwe na Benki Kuu yake yenyewe badala ya kuitegemea Benki Kuu ya Tanzania. Tena akitaka Zanzibar iwe na sarafu yake yenyewe kama ilivyokuwa nayo kwa karne kadhaa kabla — tangu ilipokuwa na sarafu ya riyali, rupia na hatimaye ya shilingi.

 

Karume alikuwa akiamini kwamba kwa kuchukua hatua hizo atakuwa anayatetea na kuyalinda maslahi ya Zanzibar. Zaidi akiamini kwamba kutimizwa kwa malengo hayo kutairejeshea Zanzibar uungwana wake wa kitaifa.

 

Hii kanuni ya kutetea na kulinda maslahi ya Zanzibar ni muhimu sana wakati huu wa mchakato wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Kwa hakika, miongoni mwa mambo ambayo Wazanzibari wanapaswa kuyazingatia wakati wa mchakato huo ni hili suala la maslahi ya jumla ya nchi yao na ile kanuni ya kimsingi ya kwamba taifa lao ni muhimu zaidi kushinda chochote kingine. Hivyo maslahi ya nchi yao ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya vyama vyao vya kisiasa kiwe cha  CCM, CUF, CHADEMA ama chochote kile kingine.

 

Wazanzibari hawatoweza kuyatetea na kuyalinda maslahi ya nchi yao endapo watagawanyika hasa kwa vile hawana kiongozi mshupavu mithili ya Sheikh Karume. Kwa sababu hiyo basi lazima wawe waangalifu wasibabaishwe na kugawanywa kama walivyokuwa wakigawanywa zamani. Wakijiachia wakagawanywa itakuwa rahisi kwa wasioitakia kheri nchi yao kuunda mifumo ya utawala itakayoyadhuru maslahi yao.

 

Hali hiyo ikizuka na wakijikuta wamegawika tena, basi wao wenyewe ndio watakaolaumiwa na vizazi vijavyo vya Wazanzibari kwa ‘kuiuza’ nchi yao.  Njia moja ya kuiuza nchi yao ni kukubali mfumo wa Muungano utakaoyadhuru matarajio ya kuleta mageuzi na maendeleo nchini Zanzibar.

 

Bahati waliyonayo Wazanzibari kwa sasa ni kwamba wananchi kwa jumla na viongozi wao si tu kuwa wana umoja lakini wanatambua kwamba lazima wawe na sauti moja na fikra moja.
Wanatambua kwamba lazima wawe na msimamo mmoja hasa pale utakapowadia wakati wa kutakiwa watoe maoni yao katika shehia zao kuhusu Katiba waitakayo na watapotakiwa  waiidhinishe au waikatae katiba mpya wakati wa kupiga kura ya maoni.

 

Kura hiyo itakuwa na lengo la kuihalalisha Katiba mpya pamoja na Muungano ambao haujapata kamwe kukubaliwa rasmi na wananchi au na taasisi yoyote ya Kizanzibari.
Umoja huo walionao sasa Wazanzibari unawapa fursa nzuri ya kuyatimiza malengo yao ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii. Aidha, kwa vile ajenda yao inaungwa mkono na kanuni za kisheria na za kimaadili hawastahiki kuwa na hofu katika kuitetea ajenda hiyo ambayo inataka pawepo na uhusiano mpya na Tanganyika juu ya msingi wa mkataba au mikataba na sio juu ya msingi wa Katiba kama ilivyo sasa.

 

Pamoja na hayo Serikali ya Zanzibar na wawakilishi wa Kizanzibari katika Tume ya Kuipitia Katiba na wale wataoiwakilisha Zanzibar katika Baraza (au Bunge) la Katiba lazima wawe wanashauriana kwa karibu sana na wawe kitu kimoja wanapofanya kazi zao.

 

Lililo muhimu ni kwamba wasipoteze fursa yoyote ya kuyawakilisha matakwa ya nchi yao, nchi ambayo inahitaji mageuzi makubwa katika sera zake za ndani na za nje hasa katika uhusiano wake na jirani zake.

 

Hivi sasa kuna mjadala mkubwa unaoendelea Zanzibar kuhusu mustakbali wa visiwa hivyo. Kwa vile Zanzibar ni nchi yenye demokrasia changa ni muhimu kwamba wananchi wasiwekewe mipaka kwa yale ambayo wanastahili kuyajadili hata ikiwa watataka Muungano uyayushwe na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar isimamishwe tena.

 

Kuna baadhi ya watu Tanzania Bara wasikiapo matamshi kama haya huruka na kuanza kuwashutumu wenye fikra hizo kuwa ni wasaliti au wachochezi.  Ukweli ni kwamba wasaliti na wachochezi ni wale wenye kwenda kinyume cha matakwa ya Wazanzibari walio wengi wenye kutaka pafanywe mageuzi makubwa kwa namna nchi yao inavyoongozwa. Wao ndio wenye kuhatarisha usalama wa sehemu zote mbili za Muungano kwa kuwalazimisha watu waache kufikiri na wafuate amri za wenye nguvu.

 

Hata hivyo, haishangazi kuwaona baadhi ya ndugu zetu wa Bara wakitoa shutuma kama hizo kwani wakati tulio nao ni wakati nyeti.  Kwa upande wao, Wazanzibari nao  wanapaswa wawe makini na wasitoe matamshi ya uchokozi. Wanachopaswa kufanya ni kutoa mwito wa kutaka pawepo uhusiano patanifu utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili katika mfumo mpya wa Muungano.

 

Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni Muungano pekee uliobuniwa na nchi mbili zilizo huru — hakuna Muungano aina hiyo popote pengine duniani.  Ulibuniwa kwa kuungana nchi mbili zilizo huru na zilizo na haki sawa na wajibu sawa mbele ya sheria ya kimataifa na pia mbele ya sheria zisizoandikwa.

 

Dosari iliyokuwepo ni kwamba kwa muda wa takriban miaka 50, Muungano huo umegeuka na kuwa Muungano usio na usawa na umeipelekea Zanzibar inyang’anywe uhuru wake na madaraka yake ya utawala bila ya ridhaa yake. Nguvu hizo za utawala zikahamishiwa Tanzania Bara, yaani kwa Serikali ya Muungano ambayo kwa hakika ni Serikali ya Tanganyika.

 

Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na michakato ya kutunga Katiba au ya kuipitia upya Katiba ya nchi. Na hapa ninawajibika kukumbusha namna CCM ilivyoandika na kuishurutisha Katiba ya mwaka 1977 ambayo ndiyo inayotumika sasa.

 

CCM iliyafanya hayo kwa njia isiyo ya halali. Ninasema hivi kwa sababu Hati za Muungano za Aprili 1964 kati ya Tanganyika na Zanzibar zilikuwa bayana kwamba Bunge la Katiba litaundwa kabla ya mwezi Aprili mwaka 1965 likiwa na idadi sawa ya wawakilishi kutoka Zanzibar na Tanganyika kuzingatia mfumo wa kudumu wa Muungano na Katiba yake.

 

Kama tujuavyo hayo hayajatendeka. CCM iliweza kuishurutisha Katiba iliyopo sasa bila ya upinzani wowote kwa sababu taifa lilikuwa na mfumo wa chama kimoja tu cha kisiasa na chama ndicho kilichokuwa taasisi adhimu nchini kushinda taasisi yoyote nyingine. Kwa hivyo, pale muswada muhimu wa Katiba mpya ulipofikishwa bungeni mwaka 1977 muswada huo ulipitishwa bila ya mjadala kwani siku hizo Bunge likichukuliwa kuwa ni kama kamati ya chama.

 

Jengine lililotokea ni kwamba wawakilishi wa Kizanzibari katika Bunge walipewa maamrisho na viongozi wao akina Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa Zanzibar wa wakati huo, wasiupinge muswada huo. Hivyo kimya kimya wabunge wa Zanzibar waliziridhia hatua kama vile ile ya kuongeza Mambo ya Muungano kutoka 11 hadi idadi ya sasa ya mambo 22.

 

Hatua hiyo iliidhuru Zanzibar kwa vile iliiondoshea serikali yake uwezo wa kupanga na kujiendeshea mambo yake ya kiuchumi na ya kijamii bila ya kuingiliwa. Matokeo yake ni hali hii iliyopo sasa ya Zanzibar kuwa nchi lakini isiyo na uhuru wala nguvu zozote.

 

Wazanzibari wametanabahi na wanapiga kelele kuipinga hali ilivyo na hawana tena hofu katika jaribio lao la kuirejeshea serikali yao mamlaka yake kamili. Wanayataka yale aliyokuwa akiyapanga Sheikh Karume katika siku za mwisho za uhai wake, yaani nchi yao iwe na sarafu yake yenyewe, iwe na Benki Kuu yake yenyewe, kwa jumla iwe na uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe bila ya kuingiliwa. Kadhalika wanataka nchi yao iwe na uhusiano na Tanganyika katika mfumo unaoshabihi uhusiano wa nchi zilizo katika Jumuiya ya Ulaya.

 

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Makala haya yalichapwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Raia Mwema mwaka 2012.  Tunayachapa hapa baada ya kuhaririwa upya kwa ridhaa ya mwandishi.