Rais Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Picha ya Shirika la AP
Na Ahmed Rajab
ZAIDI ya siku mia zimekwishapita tangu majeshi ya Israel yaanze kulitwanga eneo zima la Ukanda wa Gaza, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi mashambulio yakushangaza dhidi ya Israel yaliyofanywa na Mvuvumko wa Muqawama wa Hamas mnamo Oktoba 7, 2023. Waisraeli 1,200 walikufa na watu 240 wa mataifa kadhaa walishikwa mateka na Hamas.
Mashambulio hayo ya Oktoba 7, ambayo Hamas inayaita Gharika ya Al-Aqsa, yalikuwa ya kulipizia kisasi madhila, unyanyasaji, mateso, na mauaji ya Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi wa Jordan na hujuma zilizokuwa zikifanywa, na zinazoendelea kufanywa, na walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa huko Jerusalem. Msikiti huo ni wa tatu kwa umuhimu kwa Waislamu.
Walowezi hao, wakisaidiwa na wanajeshi wa Israel, wamekuwa wakiingia kwa nguvu msikitini humo, wakiwapiga na kuwazuia Waislamu wasiswali. Idhilali walizokuwa wakifanyiwa Waislamu msikitini humo hazisemeki. Kuna nyakati ambapo wanajeshi wa Kiisraeli wakiingia katika msikiti huo na wakizipangua kwa nguvu safu za watu waliokuwa tayari wanaswali.
Walowezi hao, wakisaidiwa vile vile na wanajeshi wa Israel, wamekuwa wakinyakua kwa nguvu ardhi, mashamba na nyumba za Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi, eneo ambalo Israel inalikalia kwa nguvu.
Israel imekuwa ikisema kwamba mashambulizi yake katika Gaza yana malengo matatu: kulishinda nguvu kundi la muqawama la Hamas; kuwakomboa mateka walioshikwa na Hamas Oktoba 7 na lengo la tatu, kuondosha kabisa kitisho kinachoikabili Israel cha kushambuliwa kutoka Gaza.
Hadi sasa, zaidi ya siku 100 tangu ianze kuitwanga Gaza, Israel haikulifikia hata lengo moja kati ya hayo. Bila ya shaka serikali ya Hamas inayoliendesha eneo la Gaza imepata pigo lakini bado serikali hiyo ipo, na inafanya kazi. Wizara yake ya afya, kwa mfano, imeushangaza ulimwengu kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu tangu Israel ianze kuibumuta Gaza baada ya Oktoba 7.
Pili, mpaka sasa Israel imeshindwa kumuokoa hata mateka mmoja miongoni mwa mateka wanaoshikwa na Hamas pamoja na Islamic Jihad, kundi jingine lililo katika muqawama wa Palestina. Wapiganaji wa Muqawama wa Hamas wa Brigedi za Izz ad-Din al-Qassam bado wanaishambulia Israel kwa makombora.
Katika muda wote huu wa siku mia ushei, Israel imewaua wakaazi wa Gaza wasiopungua 24,000 wengi wao wakiwa watoto na wanawake. Wapalestina wasiopungua 60,000 wamejeruhiwa na zaidi ya 7,000 hawajulikani walipo. Haijulikani kama wameuliwa na maiti wamegubikwa na vifusi au vipi.
Maelfu kwa maelfu ya wakaazi wa Gaza wamegeuzwa kuwa wakimbizi katika ardhi yao. Wamelazimishwa kuzihama nyumba zao Kaskazini mwa Gaza na kukimbilia Kusini. Israel iliwaambia kwamba wakenda huko watakuwa salama. Lakini ahadi hiyo haikuwa ya kweli. Hata huko Kusini ndege za kivita za Israel ziliwapiga mabomu na kuwaua. Baadhi yao waliuliwa wakiwa njiani kutoka kaskazini wakielekea Kusini.
Hivi sasa maelfu kwa maelfu ya wakaazi wa Gaza wanaishi katika mahema. Na siku hizi majira ya baridi yameingia yakizidi kuwapa shida. Hawana chakula, hawana madawa, hawana maji. Hawana mbele, hawana nyuma.
Inavoonesha ni kwamba Israel imekusudia kuliangamiza kabisa eneo zima la Ukanda wa Gaza na kulifanya liwe eneo ambalo hata paka asiweze kuishi.
Hivi si vita hivi vilivyo Gaza. Jeshi lenye kutumia kila aina ya silaha dhidi ya watu wasio na nyenzo za kujihami huwa halipigani vita. Linaua tu. Majeshi ya Israel yanawaua watu wasio na jeshi la angani au la wanamaji, wala silaha nzito. Hawana ndege za kivita; hawana manowari.
Ile iitwayo “jumuiya ya kimataifa’ imekataa kuichukulia hatua Israel, ingawa inakiri kwamba Israel imefurutu ada. Joe Biden, Rais wa Marekani, amesema wazi , tena hadharani, kwamba ingawa kweli Israel imewaua watu wengi mno na imefanya maangamizi makubwa hatoichukulia hatua. Hiyo dharau ya Biden ndiyo inayoizidishia jeuri Israel.
Lakini mambo huenda yakamgeukia Biden kwani hata ndani ya serikali yake, wapo wengi wasiokubaliana naye. Wameghadhibika kuiona Israel inaua idadi kubwa ya watu. Na wanajua kwamba mauaji hayo yangelisita mara moja lau Marekani ingekataa kuipa Israel silaha za kisasa pamoja na msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola za Marekani bilioni tatu.
Wiki iliyopita Afrika Kusini ilithubutu kupanda juu ya jukwaa la kimataifa ikionesha misuli yake ya uadilifu kwa kuwa tayari kupambana na Israel na kaka yake Marekani. Afrika Kusini iliishitaki Israel mbele ya Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, jijini Hague, kwa kufanya mauaji ya kimbari Gaza.
Huo ulikuwa ujasiri mkubwa. Afrika Kusini imefanikiwa kuliibua suala hilo katika medani ya sheria za kimataifa. Ijapokuwa Afrika si nchi moja lakini ni bara la nchi huru 54 lenye nia ya kuwa taifa moja. Na bara hilo lina chombo, Muungano wa Afrika (AU), chenye kuziunganisha nchi zote za Afrika kwa manufaa ya Waafrika. Chombo hicho kinaongozwa na itikadi au imani ya Umajumui wa Afrika.
Kuna mengi tunayoweza kuyasema dhidi ya utawala wa ANC Afrika Kusini. Lakini kwa hili serikali hiyo na watu wake wametukosha. Hawakuisahau ile kauli ya Nelson Mandela kwamba Afrika Kusini haitokuwa huru mpaka Palestina nzima itapokuwa huru.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alikuwa wa mwanzo kuikebehi Afrika Kusini. Kwa dharau Blinken alisema kwamba hatua hiyo ya Afrika Kusini haina nguvu na kwamba ati Afrika Kusini inaubabaisha ulimwengu katika wakati ambapo kunatafutwa njia za kuleta amani.
La kushangaza na jambo la aibu kabisa, ni kuziona nchi nyingi za Kiafrka zikiiacha Afrika Kusini ipambane na Israel peke yake. Hapa naifikiria hasa Tanzania, nchi iliyokuwa safu ya mbele kupigania kutetea ukombozi si barani Afrika tu bali hata nje ya Afrika. Leo i wapi?
Si lazima tuwe tunakubaliana na Hamas. Si lazima tuwapende. Tunaweza hata tukawachukia. Lakini tutakuwa kweli wanadamu wenye utu tukiwaona wanadamu wenzetu, pamoja na watoto wachanga, wakiuliwa kinyama kama wanavyouliwa Gaza? Kweli tutakuwa na moyo wa kutoyakemea mauaji hayo ya kimbari?
Historia ya Israel barani Afrika si ya kupendeza. Inachusha. Inakirihisha. Inanuka. Tangu miaka ya mwongo wa 1960 Israel imekuwa ikijihusisha na vitendo viovu katika nchi mbalimbali za Afrika. Imezifisidi nchi kadhaa kwa kupora madini yao, kuziparaganya chumi zao na hata kujihusisha katika mapinduzi ya serikali halali.
Tunakumbuka jinsi Israel ilivyokuwa ikiiunga mkono na ikishirikiana na serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini kwa kila hali. Mwaka 1977, kwa mfano, Israel iliipa serikali hiyo ya kibaguzi teknolojia ya kijeshi na uwezo wa kutengeneza mabomu ya kinyuklia. Ni Israel hii hii iliyokuwa ikisema kuwa kina Mandela na wakombozi wengine wa Afrika Kusini walikuwa magaidi. Na hivyo ndivyo Israel inavyowaita kina Ismail Haniyeh, Yahya Sinwar, Mohammed Deif na viongozi wengine wa Hamas.
Katika kipindi cha miaka kama 20 hivi Israel imekuwa ikiinyemelea tena Afrika, ikijaribu kujiingiza kwa mapana na marefu katika bara letu. Inafanya hivyo katika wakati ambapo inazidi kuwaangamiza Wapalestina. Ni wazi, kwa mfano, kwamba Israel imekusudia kulifanya eneo la Ukanda wa Gaza liwe eneo ambalo hata paka asiweze kuishi.
Wakaazi wa Gaza na Wapalestina wote wamekuwa wakitupa somo kubwa kuhusu utu. Wamekuwa wakifanya hivyo wakikabiliwa na dharau ya Marekani na jeuri ya Israel. Marekani imekuwa ikiyadharau madhila yanayowafika Wapalestina na Israel imekuwa ikiendelea kwa ujeuri kuwadhalilisha na kuwaangamiza kwa kila hali. Wanaangamiza roho zao, maisha yao, miundombinu yao, utamaduni wao na hata utambulisho wao. Lengo lao ni kuwafanya Wapalestina wawe watu wasio na kwao, wasio na chao, wasiojitambua.
Hatujui walio barabarani Afrika — kina Paulo na Mbaruku — wanafikiri nini kuhusu suala hili. Na hata wakiwa wanaupinga unyama wa Israel tusisahau kwamba kwingi Afrika hakuna uhuru wa kusema au wa kuandamana, hata kama kwa amani. Tumeona, kwa mfano, jinsi serikali ya Tanzania ilivyoyapiga marufuku maandamano ya amani ya kuitaka Israel ikomeshe mashambulizi yake dhidi ya Gaza.
Baadhi ya Waislamu wa Afrika wametiwa sumu na mashekhe wa nchi fulani za Kiarabu wenye kusema kwamba ni stahili yao wakaazi wa Gaza wafikwe na yanayowafika kwa sababu ati wao ndio walioichokoza Israel. Wanapuuza madhila ya miaka zaidi ya 75 waliyofanyiwa Wapalestina na Wazayuni.
Mashekhe hao hao ambao ni wa Kisunni wanasemekana pia kutia fitina za kimadhehebu baina ya Masunni na Mashia. Kwa vile wapiganaji wa Hizbullah wa Lebanon na wale wa Ansarullah (Wahouthi) wa Yemen ni Mashia, wanawachochea wafuasi wao wasiuunge mkono ule mhimili wa muqawama unaopigania haki za Wapalestina.
Miongoni mwa pande na nchi za mhimili wa muqawama ni Hamas, wanamgambo wa Islamic Jihad, chama cha Harakati ya Wananchi kwa Ukombozi wa Palestina (PFLP), Afghanistan, Iran, chama cha Hezbollah cha Lebanon, Syria, Iraq, na mvuvumko wa Ansarullah wa Yemen (Wahouthi).
Wainjilisti wa Kikristo wa Afrika huenda wakawaiga wenzao wa Marekani wale wajiitao Wazayuni wa Kikristo, wakaziunga mkono sera za Israel dhidi ya Wapalestina. Wao wanaamini kwamba kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948 kumetimiza ahadi iliyo kwenye Biblia na kwamba ni lazima taifa hilo liwepo ili Nabii Issa (Yesu Kristo) aweze kurudi duniani kutoka mbinguni atawale akiwa mfalme.
La ajabu ni kwamba Wazayuni Wayahudi, kwa upande wao, hawana junaha. Kwa imani zao wanaweza wakawameza Wazayuni wa Kikristo (Wainjilisti) wazima wazima. Tumeziona dalili kwa namna ambavyo Wazayuni walivyokuwa wakiwatemea mate Wakristo Jerusalem. Kuna dua iitwayo Dua ya Amidah ambayo husomwa na Wayahudi mara tatu kwa siku kuwalaani Wakristo, wafalme, na watu wote wengine pamoja na hata Wayahudi wakorofi.
Nini kinachozifanya nchi nyingi za Afrika ya leo zisiwe na msimamo kama wa Afrika Kusini kuhusu suala hili la mashambulizi ya kinyama ya Israel? Ni woga usio na sababu au unafiki wa kujipendekeza kwa wasiopenda haki?
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.