Badawi Qullatein, mtetezi wa wanyonge

Picha: Badawi Qullatein

Na Ahmed Rajab

BADAWI Qullatein aliyefariki dunia Makkah, Saudi Arabia, asubuhi ya Oktoba 31, 2011 akiwa na umri wa miaka 81 alikuwa ni mtu wa vipaji vingi: mpigania haki za wafanya kazi, mwanamapinduzi, mhariri wa magazeti na mcha Mungu. Alikuwa mtu wa dhihaka nyingi na maskhara mengi ingawa baadhi ya nyakati akipandisha hamaki. Na ulipomwambia mbona umekasirika, akijibu: ‘Unanikasirisha, kwa nini nisikasirike? Sifa nyingine ya Badawi ilikuwa ya ukaidi.

 

Hata hivyo, atakumbukwa zaidi kwa jinsi alivyoutumia ujana wake kuwatetea walala hoi na kupigania haki zao. Yeye ni mfano mzuri wa mtu wa tabaka la wenye kujiweza aliyejitolea kuwapigania wasiojiweza. Hivyo ndivyo walivyokuwa wengi wa wafuasi wa Abdulrahman Babu waliojiengua kutoka chama cha Hizbu au Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na kuanzisha Umma Party mwaka 1963.

 

Wengine watamkumbuka Badawi kwa mchango wake katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Akiwa mmoja wa viongozi wakuu wa Umma, Badawi alikuwa na mahusiano mazuri na wanaharakati wa Afro-Shirazi Party (ASP). Kati yao walikuwa akina Seif Bakari, Hassan Nassor Moyo, Saleh Saadalla na Abdulaziz Twala, ambaye wakati mmoja akiishi pamoja naye. Wakimuamini; naye akiwaamini.

 

Siku moja Seif Bakari alimdokozea Badawi kwamba baada ya uhuru kutoka Uingereza watafanya fujo Unguja mjini na kutia moto majumba ya serikali. Badawi akamwambia: ‘La, lengo lisiwe kutia moto bali kuichukua serikali.’ Usiku wa manane wa kuamkia 12 Januari 1964, serikali ya Zanzibar ilipinduliwa. Miongoni mwa waliopindua walikuwa akina Seif Bakari, Yusuf Himidi, Said Washoto, Pili Khamisi, Ramadhani Haji, Said Idi Bavuai, Khamis Darweshi na Abdallah Said Natepe.

 

Baadaye Badawi aliwaita vijana wa Umma waliokuwa wamerudi kutoka Cuba walikopata mafunzo ya mbinu za kupindua serikali wawasaidie wapinduzi. Badawi hali kadhalika ndiye aliyekaa pamoja na ‘Field Marshal’ John Okello, Twala na Jumbe na kuwateua wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza pamoja na mawaziri wa serikali mpya ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

 

Badawi aliwahi kuniambia kwamba walipokuwa wanapanga nani ashike wizara gani, Okello alimwambia: ‘Ile ya Ali Muhsin mpe Babu.’ Okello ama alisahau au hakujuwa ni wizara gani aliyokuwa nayo Sheikh Ali Muhsin, aliyekuwa kiongozi wa Hizbu. Ndipo Babu akatangazwa kuwa waziri wa mambo ya nje na biashara.

 

Kuna baadhi ya wafuasi wa Umma waliomlaumu Badawi kwa kutofanya jitihada ya kuwaingiza makomredi zaidi kwenye Baraza la Mapinduzi. Jibu lake lilikuwa kwamba hakutaka wana-Afro wadhanie kuwa makomredi walikuwa na uchu wa madaraka.

 

Ndio maana Baraza hilo lilikuwa na makomredi watatu tu: Salim Rashid, aliyekuwa Katibu wa Baraza, Abdulrahman Babu na Khamis Abdallah Ameir. Badawi mwenyewe aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Utangazaji. Moja ya hatua alizochukua ni kulibadilisha gazeti la serikali la ‘Maarifa’ liwe ‘Kweupe’. Baadaye akateuliwa waziri mdogo.

 

Kama wengi waliokuwa wakiyaunga mkono Mapinduzi, baadaye Badawi akisikitika kuwa mapinduzi yaliendeshwa sivyo. Nakumbuka siku moja katika miaka ya 1990 nikitembea Dar es Salaam pamoja na mwandishi Mohamed Said wa Tanga na tukasadif kukutana na Badawi njiani. Nilipokuwa ninawajulisha watu wawili hao nilimwambia Mohamed kwamba akitaka kuyaandika ya Mapinduzi ya Zanzibar basi amwendee Badawi.

 

Papohapo Badawi akasema kwa masikitiko: ‘Mapinduzi gani, ilikuwa ni wanawake tu.’ Nilishangaa na kumuuliza alikusudia nini. Alijibu kwamba Mapinduzi yalifisidika na akanitajia visa vya watu waliofungwa gerezani na waliouliwa kwa sababu baadhi ya viongozi wa Mapinduzi wakiwataka ama wake zao ama hawara zao.

 

Komredi Badawi, ambaye jina lake kamili lilikuwa Ahmed Badawi bin Abubakar Shibli bin Omar Qullatein alizaliwa Malindi, Unguja, ingawa nyumba ya ukoo wake na alikolelewa ni Hamamni, Mji Mkongwe, hukohuko Unguja. Ametokana na ukoo wa kisharifu. Asili ya ukoo wa Qullatein imeanzia Tarim, Hadhramaut huko Yemen ya Kusini. Ukoo huo ni tawi la kabila la Al Nadhiri la huko Tarim ingawa Maqullatein wanapatikana Afrika ya Mashariki tu.

 

Kutoka Tarim mababu zake Badawi wakateremkia Somalia; kwanza Mogadishu na halafu Barawa na baadaye kwenye kisiwa cha Pate karibu na Lamu, Kenya, kabla ya kuishia Unguja ambako ndiko alikozaliwa babu yake, Sayyid Omar Qullatein. Bwana huyu ana umaarufu mkubwa katika historia ya tariqa ya Kisufi ya Qadiriya iliyoshamiri katika nchi nyingi za Afrika ya Mashariki.

 

Yeye alipewa ijaza ya kuwa “khalifa” yaani kiongozi wa tariqa hiyo na Sheikh Uweys bin Muhammed bin Bashir al Barawi kutoka Barawa, Somalia, aliyefika Zanzibar mnamo karne ya 19 na ambaye ndiye aliyeiasisi tariqa hiyo Afrika ya Mashariki. Tangu siku hizo hadi leo miongoni mwa makhalifa wa Qadiriya huko Zanzibar mmoja hutoka kutoka ukoo wa Qullatein.

 

Huyo babu yake Badawi ndiye aliyelijenga hilo jumba la Hamamni la ukoo wao. Linaitwa Hamamni kwa sababu jumba hilo, ambalo sasa limeporomoka, limepakana na hamamu za Waajemi wa kale. Kwenye hamamu hizo waungwana wa zama hizo walikuwa wakienda kuoga, kukandwa na kusingwa.

 

Tunaweza, kwa kiwango fulani, kumfananisha Badawi na babu yake. Wote waliwakumbatia watu wa chini — Badawi katika medani ya kisiasa na babuye kwenye tariqa ya Qadiriya. Wala sitokosea nikisema kwamba hata huko kwenye dhikiri kulikuwa na siasa. Wafuasi wa Qadiriya walikuwa na mtandao wao ulioenea sana Tanganyika na walikuwa miongoni mwa wapinzani wa kwanza wa ukoloni huko.

 

Visiwani Zanzibar lakini hali ya mambo ilikuwa tafauti na siasa hazikuchanganywa na dhikiri za Qadiriya. Badawi alizivaa siasa licha ya kukatazwa na baba yake, Sayyid Shibli, aliyekuwa mara kwa mara akimkumbusha kwamba wao ni watu wa dini na ‘siasa si mambo yetu.’ Pingine ilikuwa rahisi kwa Badawi kuziingia siasa kwa vile Sayyid Shibli kwa muda wa miaka mingi alikuwa akifanya kazi katika eneo la Wasomali, kaskazini mwa Kenya.

 

Hadi leo jina la Sayyid Shibli ni maarufu sana katika eneo hilo. Alianzisha skuli Isiolo, Garissa na halafu Wajir ambako aliishi kwa miaka mingi. Mwishomwisho wa ukaazi wake katika eneo hilo alikuwa na cheo cha Afisa wa Elimu na aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Kenya. Hivyo, Badawi akimuona babake kila mwezi wa Ramadhani alipokuwa akienda kwao Unguja.

 

Baada ya masomo ya sekondari huko Unguja Badawi alipata kazi ya ukarani serikalini, kwanza akiwa karani wa Forodha na baadaye wa Idara ya Kazi (PWD). Mara alijiingiza katika harakati za wafanyakazi na kuwa mmoja wa waasisi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanya Kazi vya Kimaendeleo (FPTU). Akishirikiana na kina Ali Sultan Issa, Khamis Abdallah Ameir pamoja na Bwanakheri Musa, ambaye baadaye aliishi Liverpool, Uingereza, kwa muda wa miaka mingi. Alifariki huko akiwa na umri uliopindukia miaka 90 na alikuwa maarufu sana katika harakati za kuwapigania watu weusi Uingereza.

 

Mwanzoni mwa harakati zake, Badawi akifanya mambo yake chini kwa chini kwa vile alikuwa mtumishi wa serikali. Mnamo mwaka 1960 Badawi alitoroka kazini akaelekea Ujerumani ya Mashariki ya Wakomunisti. Alibaki huko mwaka mzima akisomea uchumi na fani ya kuendesha vuguvugu la wafanyakazi.

 

Aliporudi Zanzibar alijitumbukiza moja kwa moja katika vuguvugu la wafanyakazi. Akiwa katika uongozi wa chama cha FPTU Badawi alikuwa akishirikiana sana na viongozi wa shirikisho jingine la wafanya kazi, Zanzibar and Pemba Federation of Labour (ZPFL), la chama cha ASP. Hao walikuwa pamoja na Hassan Nassor Moyo, Adam Mwakanjuki na Mohammed Mfaume.

 

Badawi akisifika kuwa mchapa kazi hodari na kati ya shughuli zake ilikuwa kuhariri magazeti ya ‘Kibarua’ lililokuwa la Kiswahili na ‘The Worker’ lililokuwa la Kiingereza.

 

Mbali na Khamis Abdalla Ameir mtu mwingine aliyekuwa na ushawishi mkubwa kwa Badawi ni Ali Sultan Issa, sahibu yake toka utotoni. Watatu hao walipokuwa kwenye Kamati Kuu ya Umma Party ndio waliokuwa na uwezo wa kifikra wa kushindana kiitikadi na mwenyekiti wao Babu. Wote wane walikuwa wafuasi wa siasa za Kimarx za mrengo wa Mwenyekiti Mao wa China.

 

Kuna siku wafuasi wa Hizbu walipakaa kinyesi kwenye nyumba ya Badawi iliyokuwa Malindi, kwenye shina la Hizbu. Ikabidi Badawi na makomredi wenzake wahamie Miti Ulaya kulikokuwa na wafuasi wengi wa ASP. Kitimbi hicho cha kutiliwa kinyesi nyumbani kwake hakijamzuia Badawi kuandika makala ya kumsifu Sheikh Ali Muhsin kiongozi huyo wa Hizbu alipofariki.

 

Baada ya kuyatumikia Mapinduzi tangu 1964 Badawi, aliyekuwa waziri mdogo, na Ali Sultani, aliyekuwa waziri, waliondoshwa kwenye nyadhifa zao tarehe 20 Februari 1972. Wakati huo Babu alikuwa amekwishatolewa kwenye uwaziri katika serikali ya Muungano na Julius Nyerere. Badawi alikuwa miongoni mwa watu waliokamatwa, takriban wote wakiwa makomredi, kufuatia kuuliwa Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Karume tarehe 7 Aprili, 1972. Alihukumiwa kifo.

 

Hatimaye aliachiwa huru mwaka 1978 na akahamia Dar es Salaam. Jijini humo haikumchukua muda kuendelea kuishi maisha ya mtu wa kawaida. Alijiingiza katika biashara mbalimbali na mwishowe akaishia kuuza duka la nguo katika eneo la Kariakoo. Huko Dar pia akihudhuria darsa za Sharif Abdulkader Junayd katika Msikiti wa Ijumaa wa Kitumbini. Akifuata wasia wa babake kwamba awe akimtumikia Sharif Junayd. Hali kadhalika akisali sana katika Msikiti wa Makonde.

 

Unyenyekevu na ucha Mungu wake ulizidi muda wote huo. Aliwahi kuonekana Makkah miaka mingi iliyopita akifagia katika Msikiti Mkuu wa Haram Sharif. Mauti yalipomkuta alikuwa Makkah katika ibada ya Hijja.  Akiwa mzima, siku moja au mbili kabla ya kufariki alimwambia mmoja wa wanawe Mohammed aliyekuwa naye kwamba angelipenda maisha yake yamalizikie huko katika Mji Mtakatifu.

 

Jumatatu asubuhi alifanya tawafu (ibada ya kuzunguka Kaaba) katika Haram Sharif na aliporudi nyumbani pumzi zikampanda na akatutoka.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Makala hii ilichapwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Raia Mwema