Rais Samia wa G20

MAELEZO YA PICHA: Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo ya uwili (bilateral)  na Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto, pembezoni mwa mkutano wa G20 uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil, wiki iliyopita.

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

MOJAWAPO ya taswira zilizobaki kwenye kumbukumbu zangu kuhusu Mkutano wa Nchi Tajiri Duniani maarufu kwa jina la G20 uliomalizika jijini Rio de Janeiro, Brazil wiki iliyopita, inahusu mkutano ambao Rais Samia Suluhu Hassan alifanya na wahariri wa vyombo vya habari vya Tanzania waliokuwa kwenye msafara wa Rais kwenye tukio hilo.

 

Nakumbuka kumwona Rais Samia akiingia kwenye ukumbi wa mkutano huku akijaribu kusoma maandishi ya yaliyokuwa yamebandikwa kwenye maeneo tofauti jirani na chumba cha mkutano kwenye Hoteli ya Atlantis ulikofanyikia mkutano huo. Lugha ya Taifa ya Brazil ni Kireno na maneno yale yalikuwa yamebandikwa kwenye lugha hiyo. Ni wazi alikuwa anajaribu kushusha “presha” ya waliokuwa wakimsubiri.

 

Na mara tu baada ya kusalimia na kuketi, neno lake la kwanza lilikuwa; “Nasikia mnataka kunitwanga maswali. Haya tuanze”.. Wote tuliokuwa ukumbini tulicheka na hiyo ni namna nzuri ya kuanza mkutano. Kama lengo lilikuwa kushusha presha ya waandishi, lengo lilikuwa limefanikiwa.

 

Tangu awe Rais wa Tanzania takribani miaka mitatu iliyopita, nadhani Samia niliyemuona Rio de Janeiro wiki iliyopita, alikuwa mwenye kujiamini zaidi na katika kilele cha mamlaka yake. Kuna vitu kadhaa ambavyo alivionyesha Rio ambavyo vinaweza kuchangia kwenye hoja yangu hii.

 

Samia amesomea uchumi katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza na ingawa nchi imepata mafanikio ya kiuchumi chini ya utawala wake – ingawa ni nyakati ngumu za baada ya COVID 19, Vita vya Ukraine na kupanda kwa gharama za maisha duniani, si mara nyingi amewahi kuzungumza hadharani na kuonyesha mapana ya uelewa wake kwenye eneo hilo.

 

Kwa ambao wamepata bahati ya kusikiliza mahojiano yake na wahariri wa vyombo vya habari, watakuwa wamesikia namna alivyotumia muda mrefu kujenga hoja kuhusu namna ya kupambana na umasikini duniani. Kwa ufupi, maelezo yake yalikuwa kwamba tafsiri ya sasa inayotumika kuamua nani aitwe masikini au tajiri ni fyongo kwa sababu umasikini unatofautiana kati ya mahali na mahali.

 

Lakini pia ni namna alivyoweza kuunganisha uwepo wa umasikini na masuala ya vita vinavyoendelea duniani katika nchi kama Ukraine na Gaza. Kwamba kabla ya vita hizo, watu walikuwa wanajitafutia riziki na kuendesha maisha yao. Lakini vita hizi zimewarudisha nyuma kiuchumi. Si kauli inayoweza kupokewa vema na mabeberu lakini ukweli ni kwamba kuna umasikini unaosababishwa na vita.

 

Tangu awe Rais, maelezo yake yale ya Rio de Janeiro ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kupambanua mawazo yake na kuyaweka hadharani kama mchumi na kiongozi anayejua mwenendo wa dunia ulivyo. Kwa Watanzania wengi, utawala wake unanasibishwa zaidi na zile 4R lakini akiwa Rio, alionyesha upande wake mwingine kifikra.

 

Jambo lingine ambalo Rais Samia alilionyesha ni hamu ya kufanya kazi. Kwa ujumla, kwa siku mbili za mkutano wa Rio alikuwa kwenye ukumbi wa mkutano wa Jumba la Makumbusho ya Sanaa kwa zaidi ya saa 15. Saa nane katika siku ya kwanza na saa saba katika siku ya pili. Huo ni muda alioutumia ndani ya ukumbi.

 

Lakini kila siku asubuhi kabla hajakwenda kwenye ukumbi huo wa Makumbusho, Rais alikuwa na vikao na baadhi ya viongozi wa Tanzania waliokuwa Rio, na nilielezwa pia alikuwa kila siku asubuhi akipokea ripoti na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali na vyombo vya dola waliokuwa Dar es Salaam kuhusu kinachoendelea kwenye uokoaji wa watu walionaswa lilipoanguka jengo la Kariakoo.

 

Kimsingi alitumia muda mwingi wa safari ya saa 12 angani kutoka Dar es Salaam kwenda Rio kufanya mawasiliano na kutoa maelekezo kuhusu tukio hilo la Kariakoo lililotokea wakati tayari tukiwa angani. Kwa bahati nzuri, ndege ya Shirika la ATC tuliyosafiri nayo ilikuwa na huduma ya internet na hivyo ilikuwa rahisi kufanya mawasiliano. Nilishangaa kuona watu wakidai mitandaoni kuwa hakuna uwezekano wa kufanya mazungumzo ukiwa angani. Ndege yetu ya ATC ina huduma hiyo.

 

Kukupa picha halisi ya ratiba yake, labda nizungumzie siku ya mwisho tu ya ziara yake. Asubuhi alikuwa na mikutano kama kawaida, akaenda G20 mpaka walipofunga mkutano, akafanya mikutano ya uwili na viongozi wawili, akarejea hotelini, akafanya mahojiano na chombo cha habari cha Globo cha Brazil, akafanya mazungumzo na wahariri wa Tanzania na tukaondoka ukumbini dakika chache kabla ya ndege kupaa angani.

 

Baada ya kukaa angani kwa takribani saa 12 kutoka Rio kurejea Dar, hakwenda kupumzika Ikulu. Moja kwa moja alielekea Kariakoo kujionea hali halisi ilivyo na kisha akaenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenda kuwajulia hali wagonjwa walionusurika kwenye ajali ile. Aliporejea Ikulu baada ya hapo, alianza na mikutano mingine.

 

Akina sisi ambao hatukuingia ndani ya ukumbi wa G20, wala kufanya mikutano ya uwili, tayari tulikuwa tumechoshwa na uchovu wa safari. Kwa ambaye alimwona Samia akiwa Rio na akawa na umri kama wa kwangu na zaidi, angeyakumbuka maneno ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliyehoji watu wanaokimbilia kutaka kuwa Rais kwa sababu ya majukumu mazito anayoyabeba mwenye mamlaka hayo.

 

Mmoja wa wasaidizi wake aliniambia kwamba mara nyingine huwa wanachoka na kazi lakini wanapomwona Rais Samia akichapa kazi pasi na kuchoka wala kulalamika, inawapa nguvu nao ya kuendelea kutimiza majukumu yao. Kama Rais ambaye ana majukumu mazito kuliko wao hajachoka, wao wanaanzia wapi kuchoka? Ndiyo ilikuwa hoja ya msaidizi huyo.

 

Jijini Rio ilikuwa pia muhimu kuangalia ni watu wa aina gani ambao Rais alikutana nao. Kwenye mkutano mkubwa kama wa G20, kuna aina tofauti za viongozi wa kukutana nao na kwa kiongozi mgeni, anaweza kukutana na kupiga picha na yeyote. Hali haikuwa hivyo kwa Rais na ujumbe wake Rio.

 

Mkutano wake wa kwanza wa uwili alifanya na Rais Prabowo Subianto wa Indonesia. Uhusiano wa nchi hizi mbili unaelekea kuwa muhimu kibiashara hasa ikizingatiwa kuwa taifa hilo linafikiria kufanya uwekezaji kwenye mradi mkubwa zaidi wa uwekezaji katika historia ya Tanzania endapo utafanikiwa ambao ni ule wa kuchakata gesi wa LNG mkoani Lindi.

 

Rais pia alikutana na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye kuanzia mwezi ujao atakuwa ndiye Mwenyekiti wa G20 na mwenyeji wa mkutano ujao. Kwenye G20 hii, Ramaphosa alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa wakitafutwa kuonwa kwa sababu mwenyeji ana nafasi kubwa kwenye kupanga ajenda za mkutano ujao. Lakini pia Afrika Kusini ni marafiki zetu zaidi kuliko nchi nyingine zote wanachama wa G20. Ilikuwa jambo muhimu kusimika uhusiano huu wa kihistoria.

 

Rais pia alikutana na kiongozi wa Norway. Kwa watu waliosoma takwimu za karibuni zaidi za NBS, kwa mwaka uliopita, Norway ndilo taifa lililoongoza kwa kufanya uwekezaji nchini Tanzania. Mkutano wa uwili kama huo ulikuwa ni muhimu kwa sababu ya kukuza uhusiano huu wa kiuchumi.

 

Lakini kubwa zaidi Rais alifanya mazungumzo na viongozi wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bara la Asia. Tanzania inatafuta wawekezaji zaidi kwenye reli ya SGR ili kumalizia kipande cha kwenda Mwanza na tuliambiwa kwamba benki hiyo ni miongoni mwa taasisi zinazoangaliwa kwa karibu ili zilete uwekezaji kwetu.

 

Samia na wana diplomasia wetu hawakuwa na muda wa kutafuta kupiga picha na viongozi mashuhuri wa dunia ili kuonyesha nasi tupo kama ambavyo ingekuwa kawaida kwa kiongozi mgeni au ambaye hajui hasa anachotaka kwenye mikutano ya namna hii. Samia wa Rio alionyesha kwamba kwenye nyakati hizi, Tanzania tunajua nini tunakitaka linapokuja suala la kuhudhuria mikutano ya namna hii.

 

Safari ya Rio ilikuwa ya siku chache lakini ilinipa fursa adhimu ya kumtazama kwa karibu Rais wetu na wajumbe wa msafara wake. Jambo pekee ambalo naweza kulisema pasi na kificho ni kwamba kama taifa, kuna hatua tunapiga.

 

Na kwa Samia huyu ambaye nimemuona Rio de Janeiro, na kama ataendelea kufuata njia aliyoamua kuipita kiuchumi, yajayo yatakuwa mazuri zaidi.