Waisraeli wanaiogopa hata furaha ya Wapalestina

Picha kwa Hisani ya Pars Today

Na Ahmed Rajab

KISWAHILI chetu hakina neno moja lenye tafsiri ya neno la
Kiingereza ‘resistance.’ Lakini lugha za Kiarabu na Kifarsi
(Kiajemi), ambazo tumezoea kuazima misamiati yao, zote
zinalo neno moja lenye maana ya ‘resistance.’ Na lugha zote
hizo mbili zinalitumia neno hilo hilo moja lililoanzia kwenye
Kiarabu: ‘muqawama.’

 

Baadhi ya Waswahili wenye uzoefu wa mojawapo wa lugha
hizo, ama Kiarabu au Kifarsi, nao pia huliangukia neno
‘muqawama’ linaposibu kutumika. Kwa mfano, Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Tehran hulitumia neno hilo kwenye
matangazo yake na pia katika mtandao wake wa Pars Today.

 

Lugha ni chombo muhimu cha mawasiliano. Umuhimu wake
huzidi vitani katika medani ya propaganda. Namna mahasimu
wa vita wanavyojiita wenyewe au wanavyoitana huwa ni
sehemu ya mapambano baina yao.

 

Hebu tuvitupie macho vita vya sasa katika Ukanda wa Gaza.
Hivi ni vita baina ya Israel na wapiganaji wa Hamas. Israel,
yenye kuungwa mkono na Marekani, inawaita wapiganaji wa
Hamas kuwa ni magaidi. Hamas wanasema kwamba wao ni
wapiganaji wa muqawama wenye kupigania ukombozi wao.

 

Jina ‘Hamas’ ni ufupisho wa Harakat al Muqawama al Islamiya,
yaani Mvuvumko wa Muqawama wa Kiislamu. Nimetumia
‘mvuvumko’ badala ya ‘vuguvugu’ kwa sababu ingawa neno
vuguvugu hutumika kuwa na maana ya harakati, mapambano
au makingano, neno hilo pia lina maana ya kitu au jambo lenye
joto la wastani. Mapambano ya kweli huwa ya moto wa kweli
siyo joto la wastani.

 

Historia imetufunza kuwa yule mabeberu wamuitaye gaidi leo,
kesho yake hugeuka akawa mkombozi. Mfano mzuri ni Nelson
Mandela na chama chake cha ANC huko Afrika Kusini.

 

Hamas inaungwa mkono na ule iuitao mhimili wa muqawama.
Mhimili huo ni mtandao wenye kuvijumuisha vyama vya siasa
na makundi ya wanamgambo. Umeshamiri Palestina, Lebanon,
Syria, Iraq, Afghanistan na Yemen.

 

Walio kwenye mhimili huondani ya Palestina, hasa Gaza kwenyewe ni Hamas, pamoja
na wanamgambo wa Islamic Jihad, chama cha Popular Front
for the Liberation of Palestine (PFLP) yaani Harakati ya
Wananchi kwa Ukombozi wa Palestina. Nje ya Palestina
inaungwa mkono na Afghanistan, Iran, chama cha Hezbollah
cha Lebanon, Syria, Iraq, na mvuvumko wa Ansarullah wa
Yemen (maarufu kama Wahouthi).

 

Mhimili wa muqawama unasema kwamba adui yake ni ‘mhimili
wa uovu’ wenye kuongozwa na Marekani na unaozijumuisha
pia nchi za Ulaya ya Magharibi na Israel. Mhimili huo huungwa
mkono kichini chini na baadhi ya nchi za Kiarabu.

 

Mhimili wa muqawama unazikusanya itikadi tofauti za kidini.
Kwa mfano, Hamas, Islamic Jihad na Afghanistan zinafuata
madhehebu ya Sunni huku PFLP kikiwa hakina udini kikifuata
itikadi ya Umarx na Ulenin; madhehebu ya Shi’a yanafuatwa na
Iran, Hezbollah, Syria, Iraq na Ansarullah.

 

Muadhama mhariri wetu ameniruhusu niiachie akili yangu
irande kwenye vichochoro, mabonde na milima ya muqawama
ili iweze kuzikusanya baadhi ya kumbukumbu zangu
zinazohusika na muqawama wa Palestina.

 

La kwanza lilalonijia ni uhusiano baina ya mwenzetu mmoja
aliyekuwa mfuasi wa chama cha zamani cha Umma Party cha
Zanzibar, Dkt. Said Himidi, na chama cha PFLP katika wakati
ambapo PFLP kikiongozwa na Dkt. George Habash. Vyamavya PFLP na Umma Party vikifuata itikadi moja ya falsafa ya
Umarx na Ulenin.

 

Miongoni mwa viongozi wa PFLP alikuwa Ghassan Kanafani,
aliyekuwa mwananadharia, mwanaharakati, mhariri wa
majarida kadhaa na pia mwandishi wa riwaya na wa hadithi
fupi. Kanafani, aliyekuwa na mke kutoka Denmark, alikuwa wa
mwanzo kutumia dhana ya fasihi ya muqawama (kwa Kiarabu
“adab al-muqawama”) kuhusika na maandishi ya kubuni ya
Wapalestina.

 

Riwaya yake iitwayo “rijal fi-a-shams” (Wanaume
juani), iliyochapishwa mwaka 1962 imesifiwa na wahakiki kuwa
ni mfano mzuri wa fasihi ya muqawama.

 

Kwa hivyo, unaweza kuufuata uzi wa muqawama kutoka
kwenye siasa hadi kwenye utamaduni — kwenye nyimbo,
ngoma, ushairi, tamthilia na fasihi. Ni uwanja mpana.
Sijakusudia kuichambua fasihi ya muqawama. Kufanya hivyo
kutaniondosha katika njia niliyopanga kupita itayokiunganisha
kichochoro kimoja cha muqawama na chengine au mlima
mmoja na mwingine.

 

Ninachotaka kufanya ni kuwaunganisha
wanaoweza kuunganishwa katika muktadha wa muqawama ili
tuweze kupata taswira — hata kama ni ya juujuu — ya
mvuvumko huo wa muqawama.

 

Shirika la Ujasusi la Israel, Mossad, lilimuua Kanafani jijini
Beirut, Lebanon, tarehe 8 Julai, 1972. Taabini ya Kanafani
iliyoandikwa na gazeti la The Daily Star la huko Lebanon
ilisema kwamba Kanafani alikuwa mpiganaji asiyewahi
kufyetua bunduki, ambaye silaha yake ilikuwa kalamu na
kurasa za gazeti ndizo zilizokuwa uwanja wake wa mapigano.

 

Licha ya hayo, Kanafani akiamini kwamba ukombozi wa
Palestina utapatikana kwa mtutu wa bunduki. Shirika la ujasusi
la Mossad lilimuua kwa sababu alikuwa na maingiliano
makubwa na magaidi wa Kijapani wa Japanese Red Army
(JRA).

 

Kundi hilo la JRA, lililokuwa likifuata itikadi ya Umarx na Ulenin,
liliushambulia uwanja wa ndege wa Lod ulio karibu na jiji la Tel
Aviv, Israel, 30 Mei, 1972. Watu 26 walifariki katika shambulio
hilo na 80 walijeruhiwa. Israel ilisema kwamba magaidi hao wa
Kijapani walitumwa na chama cha PFLP.

 

Kilichomponza Kanafani, aliyekuwa msemaji wa PFLP, ni picha
aliyopiga na wanachama watatu wa JRA, muda mfupi kabla ya
shambulio hilo. Mtu ambaye mimi nilikuwa na uhusiano naye
na aliyekuwa akiwajua wanachama wa PFLP pamoja na wa
JRA alikuwa komredi Masao Kitazawa, Mjapani aliyekuwa
mfuasi wa itikadi ya Kimarx.

 

Kitazawa pamoja na aliyekuwa mkewe walikuwa wanaharakati
washupavu waliokuwa na mtandao mkubwa wa mrengo wa
kushoto. Mtandao wao ulianzia kwao Japani ukatambaa
kwenye nchi nyingine za Asia, ukapita Mashariki ya Kati na
ukaingia katika bara la Ulaya.

 

Kitazawa pia alipata umaarufu kwa kufasiri kwa Kijapani kitabu
muhimu cha mwananadharia wa Kimisri, Samir Amin, kiitwacho
“Imperialism and Unequal Development”.

 

Mwezi Septemba 1970 chama cha PFLP kilikuwa katika ndimi
za wengi na kikitajwa sana kwenye vyombo vya habari vya
dunia nzima kwa utekaji nyara wa ndege. Kiliamua kuziteka
nyara ndege kwa sababu. Na sababu yenyewe ni kwamba
kikiamini ya kuwa Palestina ilikuwa imeachwa mkono na
viongozi wa Kiarabu, wakiwa pamoja hata na Gamal Abdel
Nasser, aliyekuwa Rais wa Misri na ambaye wengi wakiamini
kwamba alikuwa kiongozi mshupavu kushinda wenzake wa
Kiarabu.

 

Tujikumbushe yaliyojiri siku hizo. Tarehe 23 Julai, 1970 Nasser
aliukubali ule uliokuwa ukiitwa ‘Mpango wa Rogers’
uliopendekezwa na William Rogers, aliyekuwa waziri wamambo ya nje wa Rais Richard Nixon wa Marekani. Mpango
huo ulikuwa na lengo la kuutanzua mzozo baina ya
Wapalestina na Israel.

 

Wapalestina waliupinga kwa sababu waliuona kuwa
ukiipendelea Israel. Lakini baada ya Nasser kuukubali, serikali
ya Jordan nayo ikaukubali wiki moja baadaye. Wapalestina
chambilecho Kanafani waliona kama ‘wamewekwa kwenye
shubaka’, yaani wametupwa.

 

Katikati ya mwezi wa Agosti 1970 serikali ya Nasser iliifunga
Radio ya Wapalestina iliyokuwa ikitangaza kutoka Cairo.
Mwezi Septemba, 1970 mambo yakatokota Jordan. Tarehe 6
ya mwezi huo, wanachama wa PFLP waliziteka nyara ndege
nne za abiria — tatu zikielekea New York na moja ikielekea
London.

 

Ndege ya shirika la ndege la Marekani la TWA
iliyokuwa ikisafiri kutoka Frankfurt, Ujerumani, ilitekwa nyara;
na ndege ya shirika la ndege la Uswisi, Swiss Air, iliyokuwa
ikisafiri kutoka Zurich, Uswisi, nayo pia ilitekwa nyara. Ndege
zote hizo zililazimishwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa
Dawson ulio jangwani karibu na mji wa Zarqa (mji wa buluu),
Jordan. Uwanja huo wa ndege ukabandikwa jina la ‘uwanja wa
ndege wa kimapinduzi’.

 

Siku hiyo hiyo palifanywa jaribio la kuiteka nyara ndege ya
shirika la ndege la Israel, El Al, iliyokuwa ikisafiri kutoka
Amsterdam. Jaribio hilo halikufanikiwa. Mteka nyara mmoja,
Patrick Argüello, Mmarekani aliyekuwa na asili ya Nicaragua,
aliuliwa na mwenzake, Leila Khaled, Mpalestina, alishindwa
nguvu na akakabidhiwa polisi wa London. Wote wawili
wakisafiria paspoti za Senegal.

 

Wateka nyara wengine wawili wa PFLP walioshindwa kupanda
ndege ya El Al, badala yake waliiteka nyara ndege ya shirika la
ndege la Marekani la Pan Am wakailazimisha iruke hadi Beirut
na halafu Cairo.

 

Tarehe 9 Septemba, ndege ya tano ya shirika la ndege la
Uingereza, BOAC, kutoka Bahrain ilitekwa nyara na
kulazimishwa kutua uwanja wa ndege wa Dawson, huko
Jordan.

 

Mfalme Hussein wa Jordan alighadhibika. Mwezi huo ukaingia
katika historia ya Jordan kwa jina la ‘Septemba Nyeusi’ (kwa
Kiarabu ‘Aylul al-Aswad’). Mfalme Hussein aliyaamrisha
majeshi ya serikali yake yawashambulie Wapalestina na
pakazuka vita baina ya majeshi ya Jordan na wapiganaji wa
Palestina.

PLFP kwa miaka sasa kimekuwa kikisema kwamba kina
maadui wane: Israel, Uzayuni wa dunia, ubeberu unaoongozwa
na Marekani, na nchi za Kiarabu zilizo vibaraka wa Marekani.

 

Huo kwa kweli ndio msimamo wa mhimili mzima wa
muqawama wa Palestina wenye kuitia hofu Israel. Nilishangaa
niliposikia kuwa Israel imewapiga marufuku Wapalestina
wasisherehekee na kuonesha furaha kwa wafungwa wa
Kipalestina walioachiwa huru na Israel. Ni kana kwamba
furaha ya Wapalestina ni sehemu ya muqawama pia. Na Israel
inaiogopa.

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; @ahmedrajab/X
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya
Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma
(Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na
shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature)
kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.