Kujenga au kubomoa si usanii, ni siasa

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

KUNA uhusiano wowote kati ya siasa na majengo? Kuna uhusiano wowote baina ya viongozi na matukio ya kujenga au kubomoa vitu? Jibu langu ni ndiyo na makala yangu hii itaeleza juu ya mifano na namna kujenga au kubomoa kunavyoweza kumjenga mwanasiasa au utawala mbele ya wananchi wake.

 

Ninaandika makala haya kwa sababu wiki hii nimebaini kuwa kuna wanasiasa na viongozi wetu mashuhuri ambao kwa bahati mbaya somo kuhusu hili halijawaingia  – na pengine halijawahi kuwa vichwani mwao. Na nadhani, tatizo kubwa la wanasiasa wa mrengo wa kiliberali duniani hivi sasa ni kwamba hawajapata somo la kutosha kuhusu hili.

 

Wakati huohuo, wanasiasa wa mrengo mkali inaonekana wanalijua somo na kulielewa – kuanzia miaka 300 kabla ya Kuzaliwa Kristo hadi leo. Naamini kwamba mwanasiasa au kiongozi yeyote anayethubutu kujenga au kubomoa, si mwanasiasa wa “kumchukulia poa” – iwe unakubaliana au hukubaliani na kinachofanyika. Iwe kinachofanyika kinaingia akilini au hakiingii akilini.

 

Nianzie kwanza nyumbani kabla sijaenda ughaibuni. Hivi karibuni, Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa, alionekana katika tukio ambako nyumba ya bei ilionekana ikibomolewa kwa madai kwamba aliyeijenga alikuwa amevamia kiwanja cha mtu. Kulikuwa na ushauri na maneno kadhaa kuhusu nini kilipaswa kufanywa.

 

Kuna walioamini kwamba badala ya kubomoa, serikali ilipaswa kuitaifisha nyumba ile na kumpa aliyenyang’anywa kiwanja. Kuna waliosema hatua nzuri zaidi ilipaswa kuwa kwa mwenye kiwanja kile kulipwa fidia na mwenye nyumba ambayo ingemwezesha kununua kwingine. Na kuna waliounga mkono kubomolewa kule kama kulivyotokea.

 

Kuna rafiki yangu mmoja mwanasiasa maarufu wa Tanzania akaniambia kupitia mtandao wa X kuwa alichofanya Silaa ni usanii tu na kwamba kinachotakiwa kufanywa ni kuimarisha mfumo mzima wa ardhi na si tukio moja moja kama hilo la Silaa. Bahati mbaya kwangu ni kwamba – wakati wowote ninapoona mwanasiasa au kiongozi anajenga au kubomoa kitu mbele ya watu; huo kwangu ndiyo huwa wakati wa kuanza kumtazama kama mwanasiasa wa kuangaliwa kwa karibu. Hakuna sinema wala usanii kwenye kujenga na kubomoa.

 

Nina mifano ya kushajiisha ninachosema. Chukulia mfano wa Ukuta wa Berlin. Kujengwa kwake ilikuwa alama ya kuanza kwa mpasuko wa iliokuja kujulikana kama Vita Baridi. Wakati Rais Ronald Reagan wa Marekani alipoibuka na ile kauli maarufu ya mwaka 1987; “Tear down that wall”, ulikuwa mwanzo wa kubomolewa kwa ukuta huo. Kujengwa na kubomolewa kwa ukuta ule kulikuwa na maana pana ndani yake.

 

Mchukulie mwanasiasa kama Edward Lowassa. Hakuwa anajulikana sana kufikia mwaka 1993. Lakini mwaka huo, alizuia uvamizi wa Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwa kushuhudia ubomolewaji wa uzio uliokuwa umewekwa na mfanyabiashara mmoja tajiri aliyedai kauziwa eneo hilo.

Nyota ya kisiasa ya Lowassa ilianza kung’aa baada ya tukio lile. Hizo ni nyakati ambazo kulikuwa na dhana kuwa kuna matajiri walikuwa na nguvu kuliko serikali. Ujasiri ule ulioonyeshwa na Lowassa dhidi ya tajiri ulimweka kwenye picha tofauti mbele ya wananchi. Serikali baadaye ilikuja kujenga uzio kuzunguka viwanja vile. Mtu anaweza kusema, si Lowassa na wananchi wale wenye hasira wangeichukua tu Mnazi Mmoja bila kuvunja uzio? Jibu ni hapana, kuvunjwa kwa ule uzio kulikuwa na maana yake kisiasa.

 

 

Kwenye maandiko matakatifu ya dini ya Kikristo, kuna hadithi moja maarufu kuhusu Ukuta wa Babeli. Watu walitaka kufika alipo Mungu. Walifanya nini kuonyesha hisia zao hizo? Walijenga ukuta wa Babeli. Hivi, ujenzi wa Ukuta wa Babeli ulikuwa na akili au mantiki yoyote? Unaweza kusema hapana. Lakini wakati ule na kwa watu wale, ujenzi ule ulimaanisha kitu kwao.

 

Katika miaka ya karibuni, hakuna mfano mzuri zaidi wa “siasa za ujenzi” kuliko mfano wa Donald Trump kule Marekani. Yeye alisema namna pekee ya kukabili wahamiaji haramu kuingia Marekani ni kwa ujenzi wa ukuta mpakani. Kimsingi hiyo ilikuwa ni mojawapo ya ahadi muhimu kwa watu wake. Alishinda urais – pamoja na sababu nyingine, watu wakiamini atajenga ukuta.

 

Kwanza Trump mwenyewe hakujenga ukuta wote kama alivyoahidi lakini tukiulizana hapa, tutaona kwamba suala la ujenzi wa ukuta halikuwa na maana yoyote. Yako mambo ya msingi yanayosababisha Marekani iwe na changamoto ya wahamiaji lakini ujenzi wa ukuta si suluhisho. Yule rafiki yangu wa mtandaoni, angekuwa Mmarekani angesema Trump anazungumzia jambo la hovyo lakini angeshuhudia Trump anaenda Ikulu kwa ahadi hiyo ya hovyo.

 

Kwa Tanzania, hakuna mfano mzuri wa siasa za kujenga na kubomoa kuliko siasa za hayati Rais John Magufuli. Huyu alijipatia umaarufu kwa kujenga na kubomoa. Alipokuwa waziri alijenga vitu. Alipokuwa Rais, aliamua kufanya ujenzi wa Bwawa la Nyerere na Reli ya SGR. Mradi wa bwawa uliwekewa vikwazo mpaka na mojawapo ya taasisi za Umoja wa Mataifa.

 

Hata sasa, bado kuna mjadala kuhusu kama tulihitaji kutumilia mabilioni ya shilingi kujenga bwawa lile au tungetumia fedha zile kuendeleza miradi ya gesi na njia nyingine za uzalishaji umeme. Lakini, sidhani kama mwananchi wa kawaida anamlaumu Magufuli kwa ujenzi wa bwawa au reli ya SGR. Miaka mingi sana baada ya kifo chake, Magufuli atakumbukwa kwa sababu ya bwawa na reli ile.

 

Kama mwana sayansi ya siasa, inanisumbua kuona kuna wanasiasa ambao hadi sasa hawajafahamu nguvu ya kujenga na kubomoa. Kwamba mpaka katika karne hii, mwanasiasa kijana hajui nguvu ya kuonekana unabomoa kitu ambacho kwa wananchi wa kawaida ni alama ya uonevu, ufisadi au ukoloni.

 

Kuna mfano mwingine wa karibuni zaidi. Chama cha ACT Wazalendo kimekamilisha ujenzi wa jengo kubwa ambalo sasa litatumika kama ofisi za Makao Makuu ya chama hicho. Wale wasioamini kwamba kujenga na kubomoa kuna siasa yake, walikuwa wa kwanza kusema chama si majengo bali nini kimo ndani ya mioyo ya watu. Lakini, kwa mifano ambayo tayari nimeitoa awali kwenye makala haya, unaweza kujua kwamba kilichofanywa na ACT Wazalendo kina mwangwi mkubwa kwenye duru za kisiasa.

 

Je, nakubaliana au sikubaliani na alichofanya au anachoendelea kufanya Silaa kwenye migogoro ya ardhi? Jibu la nakubaliana au sikubaliani halina maana sana. Lakini kilicho cha muhimu zaidi kwangu kama mfuatiliaji wa siasa kwa zaidi ya miongo mitatu sasa ni kuwa kuna mwanasiasa amebomoa jengo kubwa na wananchi wengi wameshuhudia tukio hilo.

 

Uzoefu wangu kwenye siasa unaniambia hili si suala la kisanii. Maelfu ya wananchi waliotazama, wanaelewa kilichotokea. Na kwa mwanasiasa au mtu anayetaraji kuwa kiongozi wa watu, hili ndilo jambo la muhimu kuliko yote. Kwamba wananchi wa kawaida wameona nini kwenye hicho ulichokifanya.

 

Ni kweli kwamba kuna shida kwenye mifumo yetu ya ardhi nchini lakini Waziri – ambaye muda wake na kipindi chake cha kushika wadhifa huo kiko nje ya uwezo wake, pengine hana muda wa kufanya makubwa sana kwenye kipindi kifupi. Jambo pekee analoweza kufanya ni kuwa tayari kuonyesha yuko tayari kupambana na wale wanaoumiza wananchi wa kawaida.

 

Mapungufu au udhaifu ulio katika mifumo ya kiserikali ni fursa kubwa zaidi kwa mwanasiasa awe wa chama tawala au upinzani. Ndiyo sababu wako wanachama wa chama tawala cha Conservatives nchini Uingereza ambao wanalalamikia kuhusu mifumo ya kuingiza wahamiaji kwao ingawa wenyewe ndiyo wako madarakani.

 

Siasa za kisasa, kwa mtazamo wangu, si suala kuonyesha una akili nyingi za kutatua changamoto. Siasa za leo zinaangalia zaidi hisia za wale walio nje ya madaraka. Na kwa maana ya hisia, hakuna picha yenye  nguvu kama ya kuonekana unabomoa mojawapo ya alama za mfumo wa uonevu.

 

Ndiyo tafsiri yangu ya alichofanya Jerry.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.