Ruto katupiga bao? Ijue nchi yako

Picha: Ramani ya Afrika ikionyesha idadi ya kambi za kijeshi za mataifa makubwa ndani ya bara hilo. Hizi ni takwimu za mtandao wa REDDIT. 

 

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

KATIKA moja ya mahojiano muhimu zaidi niliyowahi kufanya kama mwana habari, nakumbuka niliyofanya wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Nilipata fursa ya kuzungumza na mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

 

Kulikuwa na minong’ono kuwa Marekani ilikuwa na mpango wa kufanya Tanzania kuwa Makao Makuu ya Kamandi yake ya Kijeshi Afrika (AFRICOM). Afande yule, alinieleza kuwa JWTZ haitaki kambi ya Marekani – au ya jeshi lingine lolote lile ndani ya ardhi yetu.

 

Wakati huo Marekani na Tanzania zilikuwa na uhusiano mzuri sana. Rais George W Bush alifanya ziara nchini kwetu na kukaa takribani siku nne – ambayo si kawaida kwa rais wa taifa hilo kubwa kufanya kwenye nchi ya Afrika.

 

Marekani pia – kupitia kwa Rais Bush, ilikuwa imefadhili mradi mkubwa wa PEPFAR wa kupambana na Ukimwi, unaotajwa kuokoa maisha ya watu wengi barani Afrika, ikiwemo Tanzania. Kulikuwa na dalili kwamba Marekani ilikuwa inaitongoza nchi kwa jambo fulani.

 

Jenerali yule wa JWTZ, alitumia muda mrefu kunipa darasa la kwa nini jeshi letu haliwezi kukubali Tanzania kuwa na kambi ya jeshi ya nchi nyingine. Kila ninapoona viongozi wa kijeshi wa Mali, Niger na Burkina Fasso wakianza kufukuza askari wa kigeni waliokaribishwa na serikali zao huko nyuma, narejea darasa lile nililopewa na afande yule zaidi ya miaka 10 iliyopita.

 

Tulipoandika habari ile kwenye gazeti la The African wakati ule likihaririwa na Hilal Sued, tulipata simu kadhaa za kutakiwa kuweka mambo sawa. Kwanza tuliambiwa aliyetupa taarifa ile alitoa msimamo binafsi na si wa jeshi lakini tulipongezwa pia kwa kuweka hadharani msimamo wetu kama taifa.

 

Nimekumbuka mahojiano haya wakati kukiwa na mjadala kuhusu ‘mafanikio’ ya ziara ya Rais William Ruto nchini Marekani. Wapo wanaosema kuwa kualikwa Marekani kwa ziara ya kitaifa na misaada ambayo Kenya imepata kutoka kwa serikali ya Rais Joe Biden, ni ushahidi mwingine kuwa diplomasia ya Kenya inafanya kazi vizuri kuliko ya Tanzania. Kwa maneno mengine, Ruto kaipiga bao Tanzania!!

 

Mara moja nikafahamu kwamba kuna namna ambayo Watanzania wenyewe hatufahamu nchi yetu inasimamia nini kwenye masuala ya uhusiano wetu na watu wengine.

 

Labda nitoe mifano michache kueleza hili. Kwenye harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika, Tanzania ilijipambanua – kwa hali na mali, kusaidia ukombozi wa weusi wenzetu kuanzia kwa ukoloni wa Makaburu kule Afrika Kusini, Wareno wa Msumbiji na Angola na walowezi wa Kiingereza kule Zimbabwe.

 

Kenya haikuwahi kujishughulisha na mambo hayo. Yenyewe, kwa kufuata sera yao ambayo hatuwezi kuikosoa, waliamua kufanya mambo yao wenyewe.

 

Ndiyo sababu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilikuwa kimbilio la wasomi wa kimapinduzi kutoka kote duniani – wakiwemo hata wa kutoka Kenya na Uganda, kwa sababu msingi wetu kama taifa ulikuwa msingi wa kimapinduzi na wa kupinga ubeberu.

 

Kwenye miaka ya 1970 wakati Dk. Salim Ahmed Salim, akiwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, nchi yetu ilipigania masuala anuai ikiwemo haki ya China, haki ya Wapalestina na mataifa mengine yaliyokuwa yakibanwa kama vile Timor Mashariki.

 

Kenya wala haikuwa kwenye kampeni hizo. Kama sisi tulikuwa tunaelekea Kusini, wao walikuwa wanaenda Magharibi. Haikuwa ajabu kwamba ingawa sisi ni nchi jirani, kulikuwa na kurushiana maneno makali ikiwemo kuitana majina kama vile “Nchi ambayo watu hawana kitu cha kula” na “Nchi ambayo watu wanakulana wenyewe”.

Hata hapa karibuni, Balozi wa Kenya Umoja wa Mataifa, ni miongoni mwa mabalozi wachache wa Afrika walioishutumu Russia kwa kuivamia Ukraine. Tanzania, kwa sababu zake, haijawahi kuikemea Russia walau kuiunga mkono Ukraine. Sisi hatufungamani na upande wowote.

 

Upande mwingine wa shilingi kwa Kenya ni kuwa yenyewe haioni shida kuwa na kambi za kijeshi za nchi nyingine ndani ya mipaka yake. Hivi tunavyozungumza, tayari Uingereza na Marekani zina kambi zake kwenye mipaka ya Kenya.

 

Pili, Kenya haioni shida kupeleka askari wake nchini Haiti kupambana ingawa wananchi wa Haiti hawaitaki. Msimamo wa Tanzania, miaka yote, ni kuwa kama inakwenda kulinda amani mahala, itafanya hivyo si katika mazingira ya mamluki bali kupitia misingi yake ya kiulinzi na kiusalama.

 

Hivyo, Tanzania haiwezi kutuma JWTZ kwenda kulinda mali ya kampuni ya TOTAL ya Ufaransa au kufanya kazi kwa sababu ya kulipwa. Lakini Tanzania hiyohiyo, inaweza kupeleka kikosi Comoro kama itapata baraka za taasisi kama Umoja wa Afrika (AU) au SADC.

 

Kenya wana utaratibu wao wa kuendesha mambo yao. Tanzania ina utaratibu wake wa kuendesha mambo yake. Kenya inaweza kupeleka askari wake Haiti kulinda Amani kwa makubaliano na Marekani lakini Tanzania haiwezi. Haiko hivyo.

 

Kenya inaweza kuruhusu vikosi vya nje kuweka kambi zao kwake lakini Tanzania haiwezi. Hatuko namna hiyo. Kenya imeamua kuwa yenyewe itaweka nguzo ya ulinzi wake kwa Marekani na mataifa ya Magharibi kupitia NATO lakini sisi tumesema hatutakuwa na upande kwenye ulinzi na usalama wetu.

 

Tangu enzi za Baba wa Taifa, tulikuwa na wanajeshi waliosoma Sandhurst ya Uingereza lakini walikuwepo pia waliokwenda Algeria, India, China, Korea Kaskazini mpaka Panama kwa akina Manuel Noriega. Hata hapa majuzi, ninafahamu askari wetu wanaopewa mafunzo mpaka katika nchi zisizojulikana sana kijeshi kama Bangladesh.

 

Kuna gharama kuwa Tanzania. Kuwa Tanzania maana yake ni kuwa ulinzi wako unategemea uimara wako wa ndani na uhusiano wako na pande tofauti za dunia. Lakini muhimu zaidi, ni kuwa na uhusiano mzuri na wa kirafiki na jirani zetu.

 

Kenya wataendelea kufanya mambo yao kama Kenya. Na Tanzania tutabaki kuwa Tanzania. Ni nchi yao, ni mustakabali wao. Lakini hakuna bao lolote ambalo Tanzania imepigwa kwa sababu Kenya imepewa vifaru na ndege za kijeshi.

 

Ni msimamo wetu huo na heshima ambayo tumeijenga kwa miaka mingi, ndiyo umetufanya tuwe Tanzania ambayo tunaiona leo. Binafsi, naamini Tanzania ndiyo taifa la kipekee na kubwa zaidi katika eneo hili la Afrika Mashariki.

 

Na simaanishi ukubwa wa eneo letu kijiografia au Pato la Taifa. Naamanisha ukubwa ambao haupimwi kwa urefu, upana au kipato. Ukiyajua ya kwako, ya jirani hayatakuhangaisha.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.