Picha: Kiongozi wa Upinzani nchini Burundi, Agathon Rwasa, akizungumza na Mhariri wa Gazeti la Dunia, Ezekiel Kamwaga, katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita. Picha ya Maktaba.
Na Ezekiel Kamwaga
KIONGOZI wa chama cha upinzani cha Congress for National Liberty (CNL) nchini Burundi, Agathon Rwasa, amesema chanzo kikubwa cha migogoro ya kisiasa barani Afrika ni viongozi kutofahamu nini hasa maana ya nchi kuwa huru. Katika mahojiano maalumu aliyofanya na Gazeti la Dunia (GD) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Rwasa alisema tatizo hilo limeanzia tangu kizazi cha viongozi wa kwanza baada ya Uhuru zaidi ya miongo sita iliyopita.
“Viongozi wengi wa Afrika hawajui nini maana ya nchi kuwa huru. Tatizo hili limeanzia kwenye kizazi cha kwanza cha viongozi wa Afrika waliopigania Uhuru. Wapo ambao kwao kuwa huru ilimaanisha kuchukua nafasi ya wakoloni. Nchi kuwa huru haikuwa na maana ya kufukuza wakoloni peke yake. Ilimaanisha kujenga taifa lenye umoja, kuheshimiana, kutawala kwa haki, kuwapa wananchi maendeleo na kila mwananchi kujiona ana haki na fursa za kisiasa, kiuchumi na kijamii kama ilivyo kwa raia wengine. Huo sasa ndiyo Uhuru na kwa bahati mbaya viongozi wengi wa Afrika hawaoni hili,” alisema.
Katika mahojiano hayo, Rwasa alisema kiongozi anayefahamu maana ya nchi na watu wake kuwa huru, hawezi kuwanyima watu uhuru wa kujieleza na kufanya siasa, hawezi kuendesha siasa zinazochochea migawanyiko katika jamii, hawezi kuruhusu rushwa na ufisadi wa mali ya umma kwa kisingizio chochote na hawezi kujenga mfumo wa haki unaokandamiza wengine na kuwapendelea wengine.
Mahojiano kamili kati ya Rwasa na GD yatarushwa mwishoni mwa wiki hii katika podcast ya Ezekiel Kamwaga Show na yamejadili kwa kina hali ya kisiasa nchini Burundi hivi sasa.
Mwanasiasa huyo ambaye atafikisha umri wa miaka 60 mwakani, ameshiriki katika siasa za Burundi kwa takribani miongo minne – kuanzia kuingia msituni na kuongoza kikosi cha waasi baada ya mauaji ya Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, Melchior Ndadaye, mwaka 1993 hadi Naibu Spika wa Bunge la taifa hilo wakati wa utawala wa Rais Pierre Nkurunziza.
Kuhusu hali ilivyo Burundi hivi sasa, Rwasa alisema utawala wa Rais Evariste Ndayishimiye umeanza kuelekea katika njia za kidikteta; akitoa mfano wa kukamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa viongozi wanaopinga utawala wake.
Rwasa alisema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na eneo la Maziwa Makuu kwa ujumla, zina wajibu wa kufuatilia kwa karibu kinachoendelea nchini humo kwa sasa kwa vile kuharibika kwa amani ya Burundi kutakuwa na athari mbaya kwa jirani wote wa taifa hilo.
“Baada ya uchaguzi wa Rais uliopita ambao najua nilimshinda lakini yeye alitangazwa kuwa mshindi, Ndayishimiye ameamua kuweka pembeni chama chetu cha CNL na kuamua kufanya kazi na vyama vidogo.
“Katiba yetu haimzuii kufanya anavyofanya lakini vitu vingine kiongozi anatakiwa kutumia busara. Sehemu kubwa ya mazungumzo ya kutafuta amani yaliyokuwa yakifanyika Arusha yalikuwa kwenye kuhakikisha vyama vinavyofanya vizuri vinafanya kazi kwa karibu.
“Hivi ninavyozungumza nawe, kuna viongozi wenzangu kadhaa wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa makosa ambayo yanaonekana kabisa yanatokana na siasa. Hii hali inatakiwa kubadilika haraka sana na hilo ndilo ombi langu kwa viongozi wa Tanzania na EAC kwa ujumla,” alisema.
Alipoulizwa na mwandishi kama ana mawasiliano yoyote na Rais Ndayishimiye kwa sasa, Rwasa alisema hawana mazungumzo ya aina yoyote na kwamba mara ya mwisho kuwa naye katika eneo moja ilikuwa ni katika mojawapo ya mikutano ya vyama vya siasa uliyofanyika Septemba mwaka jana.
Mwanasiasa huyu aliwahi kuishi Tanzania kama mkimbizi kati yam waka 1988 hadi mwaka 1991 na katika muda wote wa mazungumzo yetu alizungumza kwa kutumia lugha ya Kiswahili pasi na kukwama.
Kuhusu unaoonekana kama mgogoro ndani ya chama chake, Rwasa alisema unapandikizwa na chama tawala kwa lengo la kukivuruga ili kisije kuleta ushindani mkali kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi uliopita wa mwaka 2020.
Gazeti la Dunia linafahamu kwamba akiwa nchini Tanzania kwa mapumziko, Rwasa alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi kadhaa wa vyama vya siasa na serikali nchini – akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Sharif, ambaye picha za mkutano wao zilisambazwa kwa vyombo vya habari.
Pia, ujumbe wa watu 14 kutoka Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kikiongozwa na Mwenyekiti wake wa sasa, Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF), umekwenda nchini Burundi wiki hii kwa ajili ya kujionea hali ya kisiasa ilivyo nchini humo.
Burundi na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri wa kijamii, kisiasa na kiuchumi na enzi za utawala wa kikoloni wa Ujerumani, Tanganyika na Burundi ziliwahi kuwa nchi moja.