Na Ezekiel Kamwaga
MUONGO mmoja uliopita, nilikuwa na mazungumzo na mmoja wa maofisa waandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ofisini kwake na mara akapita mtu mmoja wa makamo mbele yetu. Rafiki yangu akaniuliza “unamfahamu yule”, nikajibu hapana. Akanitajia jina la Khamis Mussa Omar, wakati huo akiwa Mjumbe wa Bodi ya BoT, na kwa maelezo ya ofisa huyo, kama angeambiwa ataje Wazanzibari mahiri watatu aliopata kukutana nao, Khamisi angekuwa mmoja wao.
Huyu ndiye Khamis ambaye wiki iliyopita alitangazwa na Ikulu kuwa Balozi mpya wa Tanzania nchini China. Kwa wanaomfahamu mtumishi huyu wa serikali kwa zaidi ya miaka 30, wanaweza kupata picha ya kwa nini Rais Samia Suluhu Hassan kampeleka kwenye taifa ambalo sasa linaonekana kuwa mpinzani halisi wa Marekani kama taifa lenye nguvu zaidi za kiuchumi na kijeshi.
Khamis ni mmoja wa waanzilishi wa Zanzibar Chamber of Commerce, amepata kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar na anafahamika kama mmoja wa Wazanzibari wenye uwezo mkubwa wa maarifa na utendaji.
Huyu ni mtu ambaye anapelekwa China kwa sababu ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi baina ya Tanzania na taifa hilo kubwa ambalo tuna uhusiano nalo wa kihistoria wa muda mrefu. Ikumbukwe pia kwamba Zanzibar ina uhusiano wa kipekee na China. Hayati Abdulrahman Babu, Mzanzibari, alikutana na akina Mao Zedong na Chou En Lai kabla ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na anatajwa kama mtu aliyefungua uhusiano baina ya mataifa haya mawili.
Uteuzi huu wa Khamis Mussa Omar unafanya mambo mawili makubwa; mosi unapeleka mtu mwenye maarifa na mwenye uelewa mkubwa wa biashara na uchumi katika taifa linalopanda kiuchumi katika mfumo wa kidunia wa sasa. Na kwa kuwa kwake Mzanzibari, kunawapa Wachina fursa ya kukumbushwa kuhusu Mzanzibari mwingine muhimu kwao – Dk. Salim Ahmed Salim.
Dk. Salim ana heshima kubwa China kwa sababu akiwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, aliongoza kampeni ya kuirejesha China ndani ya Umoja wa Mataifa. Wachina wengi ni wafuasi wa imani ya Confucius ambapo dhana ya Guanxi – inayohusu uhusiano wa kidunia ndiyo huongoza namna China inavyohusiana na mataifa mengine.
Kwenye Guanxi mahusiano ya kidunia yako ya aina tano; Mfalme kwa Watawaliwa, Mume na Mke, Baba kwa Watoto, Kaka kwa Wadogo zake na Rafiki kwa Rafiki. Kwa sababu ya uhusiano wa muda mrefu uliojengwa huko nyuma, China inajiona kama kaka mkubwa ambaye ana wajibu wa kusaidia wadogo zake kujikwamua kiuchumi. Kuwa na Mzanzibari Beijing, kunaleta picha ya kipekee kwenye uhusiano huu.
Mabalozi wa Tanzania wakati wa Rais Samia
Jambo la kwanza kulielewa kuhusu uteuzi wowote wa balozi unapofanyika, ni kuwa hakuna uteuzi unaofanyika bila sababu. Yaani hakuna balozi anayepelekwa kwenye nchi yoyote pasipo sababu ya kimsingi iliyo nyuma yake – hata kama kuna watu watahoji “yule anaenda kufanya nini kule?”.
Rais yeyote, wa taifa lolote, anaweza kumwondoa mtu kutoka nchini kwake na kwenda kwingine ilia pate nafasi ya kupumua nchini kwake. Kwa watu wa kawaida, uteuzi huo unaweza kuwa hauna maana lakini kwa mamlaka ya uteuzi, ina maana kubwa kwa mamlaka kupata nafasi ya kufanya mambo yake bila kughasiwa mara kwa mara.
Uteuzi wa Balozi unaweza kuzingatia urafiki au uhusiano binafsi baina ya balozi na nchi anayokwenda, uwezo wa balozi kumudu mazingira ya nchi husika, kuruhusu kufanyika kwa mabadiliko pasipo aliyeondolewa kupoteza hadhi yake kwenye jamii na weledi na uelewa wa majukumu.
Chukulia mfano wa Marekani. Mara baada ya Rais Xi Jinping kuukwaa Urais wa China, Rais Donald Trump alimteua Gavana wa Iowa, Terry Branstad kuwa Balozi wa Marekani nchini China. Trump alifahamu kuwa Branstad na Xi waliwahi kukutana na kufahamiana kwenye miaka ya 1980 na alitaka kutumia uhusiano wao huo kujenga mahusiano ya China na Marekani. Branstad wala hakuwa na sifa yoyote ya kibalozi.
Tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, uteuzi wake wa mabalozi wa Tanzania hasa kwenye nchi za kimkakati umekuwa ukizingatia zaidi weledi, diplomasia ya uchumi na kujaribu kuirejesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoheshimika katika duru za kimataifa.
Katika weledi – yaani kwa kutazama watu waliosomea na kukulia katika Wizara ya Mambo ya Nje, Rais ameonyesha imani kubwa kwa kundi hili. Katika uteuzi wa hivi karibuni, uteuzi wa mtu kama Caesar Waitara kuwa Balozi wa Tanzania nchini Namibia ni mfano halisi wa hili. Balozi Waitara ni mtu aliyepikwa na kuivishwa kwa majukumu ya kibalozi anayokwenda kuyafanya Namibia.
Rais Samia pia ndiye aliyemteua Togolani Mavura kuwa Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini. Hili ni miongoni mwa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani na haijachukua muda mrefu kwa balozi huyu kijana kuonyesha uwezo wake kwa kuanza kuvutia mitaji ya Korea Kusini kuja Tanzania. Balozi Togolani amekulia katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Mteule mwingine wa Rais Samia ni Macocha Tembele ambaye ndiyo kwanza ametoka kufanikisha ujio wa Rais Joko Widodo wa Singapore takribani miaka miwili tu tangu Tanzania ifungue ubalozi wake katika taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu Kusini mwa mstari wa Ikweta.
Balozi Mbelwa na Uingereza
Uteuzi uliotangazwa zaidi na vyombo vya habari wiki iliyopita ulihusu kuhamishwa kwa Balozi Mbelwa Kairuki kutoka China kwenda Uingereza. Katika miaka ya karibuni, Mbelwa – kijana mwingine Wizara ya Mambo ya Nje, alikuwa mmoja wa mabalozi maarufu wa Tanzania katika nchi za kigeni.
Uteuzi wa Mbelwa unafanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja. Mosi unamhusu mtu ambaye ametoka kufanya kazi katika mojawapo ya nchi kubwa na anapelekwa katika mojawapo ya mataifa makubwa duniani. Bila shaka, inamaanisha ataingia kazini siku ya kwanza akijua nini anatakiwa kufanya.
Lakini Balozi Mbelwa ni mtu anayeifahamu vizuri Uingereza – akiwa amepata masomo katika Chuo Kikuu cha Hull nchini humo na anayejua mengi kuhusu taifa hilo ambalo kuna nyakati lilikuwa linatawala takribani theluthi moja ya dunia nzima.
Naweza kuelewa pia uteuzi huu wa Mbelwa katika eneo lingine. Inaonekana kwamba Tanzania imeamua kuongeza nguvu katika uhusiano wake na nchi za Jumuiya ya Madola na sasa Mtanzania, Liberata Mulamula, anatajwa kuwa mgombea kinara miongoni mwa wanaotajwa kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.
Kama Tanzania inataka kurejea kuwa mbele kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa, ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza unahitaji mtu mwenye kuijua kazi yake, mwerevu na anayeijua nini nchi yake inahitaji kupata kutoka jumuiya tofauti ambazo ipo. Katika duru za kidiplomasia, Mbelwa anatajwa kuwa mmoja wa mabalozi mahiri zaidi wa Tanzania na uteuzi huu wa Rais unamaanisha taifa limepeleka mwanadiplomasia mahiri katika mojawapo ya mataifa ya kimkakati.
Takwimu zinaonyesha Tanzania imeanza tena kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa mfululizo, idadi ya kampuni kutoka mataifa makubwa zinazotaka kuja kuwekeza Tanzania inaongezeka na taratibu – inaonekana wanadiplomasia wa Tanzania wanaanza kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi kama ambavyo Rais wao anataka.
Na kama unataka mfano mzuri wa nini wanadiplomasia wa Tanzania wanafanya nje, tazama kilichotokea Saudi Arabia. Taifa hili lilikuwa limepiga marufuku manunuzi ya nyama kutoka Tanzania kwa takribani miongo miwili. Lakini kazi kubwa ya aliyekuwa Balozi, Ali Mwadini, ambaye sasa amehamishiwa Paris, Ufaransa, imesababisha Tanzania kuruhusiwa tena kuuza nyama kwenye taifa hilo.
Alipokuja Tanzania mwaka huu kushawishi wadau wa nyama kutumia fursa hiyo ipasavyo, aliwaambia wadau hao; “Saudia wameniambia soko ni kubwa kiasi kwamba hata kama tutauza ng’ombe wetu wote waliopo sasa, bado hatutaweza kukidhi mahitaji ya soko lao. Kazi kwenu”.
Hawa, ndiyo mabalozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.