Hadaa kama mbinu ya kivita: Mabadiliko ya Kagame Jeshi la Rwanda

Picha: Rais Paul Kagame. Kwa hisani ya tovuti ya PML Daily

 

Na Ezekiel Kamwaga

 

All warfare is deception.

 

Sun Tzu, The Art of War

 

MOJAWAPO ya habari kubwa katika eneo la Afrika Mashariki mwezi huu ilikuwa ni mabadiliko makubwa kwenye sekta ya Ulinzi na Usalama yaliyotangazwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda mwanzoni mwa mwezi huu. Kwenye mabadiliko hayo, vigogo kadhaa wa sekta hizo walibadilishwa majukumu na wengine kuondolewa kabisa katika nyadhifa zao.

 

Mtandao wa Al Jazeera katika taarifa yake ulieleza kwamba “siku moja baada ya kumteua waziri mpya wa Ulinzi na Mkuu Mpya wa Majeshi, Rais Kagame amewafukuza kazi maofisa kadhaa wa ngazi za juu wa Jeshi la Rwanda”. Katika hatua hii ya makala haya, ni muhimu kupigia mstari neno “kuwafukuza kazi” maofisa wa ngazi za juu wa jeshi. Kuna mambo machache kwenye mabadiliko haya ya Jeshi la Rwanda (RDF) ambayo yanafanya mabadiliko haya yasiwe ya kawaida. La kwanza linahusu idadi ya walioathiriwa na mabadiliko hayo na pili ni aina ya watu walioguswa moja kwa moja na mabadiliko hayo. Zaidi ya kufukuza kazi maofisa 14, taarifa ya Ikulu ya Rwanda ilitangaza pia kufukuzwa kwa askari wengine 116 huku wengine 112 wakitenguliwa nyadhifa zao. Mabadiliko ya aina hiyo kwa wakati mmoja si ya kawaida.

 

Lakini kuna pia suala la nani na nani wamehusika. Vigogo mashuhuri waliofukuzwa ni Meja Jenerali Aloys Muganga aliyekuwa Kamanda wa Vifaa vya Kivita wa RDF tangu mwaka 2019 na Brigedia Jenerali Francis Mutiganda aliyekuwa Mkuu wa Ujasusi wa Nje wa Shirika la Usalama wa Taifa la Rwanda (NISS) hadi mwaka 2019 aliporejeshwa Makao Makuu ya RDF kwa majukumu ambayo Al Jazeera limeandika “hayakuwahi kuwekwa wazi.”

 

Kuna mengine mawili makubwa; Mosi, kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya kimataifa, mabadiliko haya ya Kagame yametokea takribani wiki moja tu baada ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kutoa tuhuma kwamba kundi la waasi la M23 likisaidiwa na RDF linajiandaa kushambulia mji wa Goma ulio Mashariki mwa DRC.

 

Jambo la pili ambalo lilipita bila kuzungumzwa na wengi ni kuwa katika taarifa ya kutangaza mabadiliko hayo, Wizara ya Ulinzi ya Rwanda ilitajwa kama moja ya vyombo vya ulinzi vya nchi hiyo. Kwa kawaida, nchi nyingi huchukulia wizara hiyo kama taasisi ya kiraia lakini uteuzi wa Juvenal Marizamunda kuwa Waziri wa Ulinzi akichukua nafasi ya Albert Murasira, ulitangazwa kama sehemu ya mabadiliko ya vyombo vya ulinzi vya Rwanda.

 

Kwa nini naona kuna dalili za hadaa kwenye mabadiliko haya? Ni kwa sababu hadaa – kama ambavyo imejulikana kwa miaka mingi sasa, ni sehemu ya utamaduni wa kivita duniani kote. Kwa mtu ambaye anaamini katika suala zima la umuhimu wa ujasusi wa kivita, Kagame atakuwa anajua umuhimu wa hadaa (deception) katika mazingira ya vita.

 

Kwa sasa, Rwanda ina maeneo matatu ya kimkakati kivita ambako Jeshi lake linatazama kwa karibu. Kuna eneo la Msumbiji ambako RDF inasaidia jitihada za kupambana na vikundi vya kigaidi vinavyotishia uhai wa mradi mkubwa wa mafuta na gesi nchini humo. Vikosi vya Rwanda viko pia Jamhuri ya Afrika ya Kati vikisaidia kulinda amani na bila kusahau mgogoro wa Mashariki mwa DRC ambao unafukuta nyakati zote.

 

Kama tuhuma za Jeshi la DRC zina chembe ya ukweli kama vilivyoripoti vyombo vya habari vya kimataifa – taarifa za mabadiliko haya makubwa ya jeshi na kufukuza askari, zinatoa picha ya jeshi ambalo linapita katika mgogoro au kuna hali ya sintofahamu. Lakini, ni Lao Tzu huyo huyo wa The Art of War aliyesema vita zote ni hadaa ndiye aliyesema pia kwamba “katika wakati ukiwa imara, onyesha una udhaifu. Katika wakati ukiwa dhaifu, onesha uko imara.” Tafsiri hii ya sintofahamu kwenye RDF inaweza kuwa wimbo mzuri kwa FARC lakini pia unaweza kuwa mtego – hadaa.

 

Lakini idadi hii kubwa ya askari waliotenguliwa nyadhifa zao au kufukuzwa, inatoa picha nyingine. Picha ambayo naiona ni kwamba inawezekana askari hao wakawa wanapewa majukumu mengine ambayo inawezekana si ya RDF kabisa lakini ni majukumu ya kufaidisha taifa hilo.

 

Katika historia ya masuala ya kivita duniani, ziko simulizi nyingi za askari na makamanda wa vikosi ambao walionekana kama wamefukuzwa au kutelekezwa na watawala – lakini wakaja kuibuka baadaye wakiwa upande uleule wa watawala huku ikija kufahamika kuwa walikuwa kwenye “kazi maalumu” wakati wakionekana wametelekezwa na hawana nafasi tena.

 

Inajulikana kuwa Jenerali James Kabarebe, pengine Kamanda asiye Mkongomani anayeijua zaidi DRC kuliko mwingine yeyote hivi sasa -akiongoza vikosi chini ya Laurent Desire Kabila vilivyompindua Rais Mobutu Sseseseko, na baadaye kuwa Mnadhimu wa Jeshi la DRC, sasa ni mshauri wa Kagame wa masuala ya Ulinzi – baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Waziri wa Ulinzi mwaka 2018.

 

Hii maana yake ni kuwa Kagame sasa anaweza kumtumia Kabarebe atakavyo – sirini na hadharani, kupitia wadhifa wake wa ushauri ambao umemuondolea majukumu ya kiraia aliyokuwa nayo kama Waziri wa Ulinzi. Kwa kumwondoa Mutiganda RDF ambako, kwa mara nyingine nanukuu Al Jazeera, alikuwa akitekeleza majukumu ambayo hakuna ajuaye zaidi ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, Kagame sasa ana uwezo wa kumtumia atakavyo popote.

 

Wakati watu wengine wakiona ni mabadiliko makubwa na yasiyo na maelezo ya kutosha – mimi naona hadaa ya kivita.

 

Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Maridhiano ya Kisiasa  mwenye Shahada ya Uzamili katika African Politics kutoka Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.