Na Ezekiel Kamwaga
MFANO mmoja unatosha kumueleza Waziri wa Mambo ya Nje, January Makamba, na utendaji wake tangu alipoingia kwenye wizara hiyo mwaka huu. Kwenye ndege wakati tukirejea Dar es Salaam kutoka India kwenye ziara ya kitaifa ya Rais Samia nchini humo, mmoja wa mawaziri alinieleza kwamba tangu awe waziri – ziara ile ilikuwa ndiyo imeandaliwa vizuri zaidi na Wizara ya Mambo ya Nje kuliko nyingine zote alizowahi kuwepo.
Na alichosema kilikuwa na maelezo. Tangu January ateuliwe kwenye nafasi hiyo Agosti mwaka huu, kila ziara imekuwa na vitu kadhaa vya tofauti; kwanza ameanzisha utaratibu wa kutoa maelezo kuhusu ziara za Rais na nini hasa kinakwenda kufanyika, kuweka utaratibu wa mawaziri na wafanyabiashara kushiriki kwenye ziara hizo ili ziwe na tija kiuchumi na kutengeneza vijitabu vidogo vya kueleza kuhusu ziara hizo, masuala ya itifaki, Tanzania na malengo ya ziara.
Lakini kuna jambo lingine ambalo ameanza kulifanya linaloongeza thamani ya wizara yake. Katika ziara ya India, kwa mfano, January alihakikisha anatengeneza uhusiano binafsi kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Subrahmanyam Jaishankar, kiasi kwamba ziara ya Rais wetu India ilikuwa na mafanikio makubwa kwa mikutano na wafanyabiashara wakubwa na Tanzania kuwa taifa la kwanza kufanya ziara India baada ya mkutano wa G20 uliofanyika New Delhi.
Kabla ya kwenda Mambo ya Nje, January alikuwa Waziri wa Nishati ambako moja ya mambo aliyofanikisha lilikuwa ni suala la kugeuza madeni ya shirika la umeme la TANESCO kuwa mtaji. Suala hilo lilipigiwa kelele kwa muda mrefu na January alilifanikisha chini ya mwaka mmoja wa uongozi wake na kufikia katikati ya mwaka huu, TANESCO kwa mara ya kwanza ikatangaza faida ya shilingi bilioni 109.
Muktadha ni kitu muhimu. TANESCO lenye wafanyakazi zaidi ya 10,000 ni shirika kubwa zaidi la umma hapa nchini. TANESCO yenye faida ni chachu muhimu kwenye ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa ujumla wake. Mwaka wa 2023 umeshuhudia TANESCO ikitengeneza faida kwa mara ya kwanza na waziri wakati huo alikuwa January.