Mwandishi wa makala haya, Ahmed Rajab, akizungumza kwenye Baraza la House of Lords jijini London Julai 5, 2023. Hapa alikuwa akitoa mada kuhusu Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili. Picha kwa Hisani ya Karam Bharij.
Na Ahmed Rajab
JUMATANO ya wiki iliyopita, nilimpigia simu mhariri wetu wa Gazeti la Dunia nikamwambia kwa ukali kwamba lau ningelikuwa karibu naye ningechukua bakora nikamchapa. Namna mhashamu huyu alivyonijibu kulinifanya nimuonee huruma kidogo kwa sababu alinijibu kwa unyonge na mshangao.
“Kwani nimefanya nini?” aliniuliza.
Nikamueleza kwamba aliandika kwenye Twitter neno “RUKSA”, tena kwa herufi kubwa, neno ambalo halimo katika Kiswahili. Kunisikia nikisema hivyo akaangua kicheko na akacheka kwa muda. Lakini hili si jambo la mzaha. Si jambo la kudhihakiwa. Ni jambo la uhai. Uhai wa lugha yetu tunayoitukuza na ustaarabu wake. Uhai wa Kiswahili na ustaarabu wake.
Jinsi Kiswahili kinavyonyongwa siku hizi ndio iliyokuwa sehemu kubwa ya maudhui ya hotuba niliyoitoa Ijumaa iliyopita kwenye Ukumbi wa River Room katika Baraza la House of Lords la Bunge la Uingereza. Niliitoa hotuba hiyo nikiwa msemaji mkuu kwenye shughuli iliyoandaliwa na Taasisi ya MTM kuitukuza lugha yetu ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani. Mwenyeji wetu katika House of Lords alikuwa Lord Boateng.
Ilikuwa ni fahari na hishima kubwa kwangu kuwa mzungumzaji mkuu katika hafla hiyo. Si tu kwamba ilinipa fursa ya kuizungumza, kuisifu na kuitukuza lugha yetu lakini pia iliniwezesha kusema mawili matatu juu ya yale yenye kutuudhi, kutuhuzunisha na kututia unyonge sisi Waswahili.
Sisi Waswahili na wenzetu wenye kuizungumza lugha hii sote kwa pamoja tunajivunia kuadhimishwa kwa mwaka wa pili sasa Siku ya Kiswahili Duniani. Maadhimisho kama hayo yalifanywa wiki iiyopita katika sehemu nyingi duniani. Pia tunajivunia kwamba Kiswahili kinatambuliwa kuwa ni moja ya lugha rasmi za Muungano wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Hali kadhalika Kiswahili ni moja ya lugha za kigeni zinazosomeshwa katika vyuo vikuu mbalimbali na hata katika skuli katika sehemu tafauti za ulimwengu. Hili ni jambo muhimu tukizingatia kwamba lugha ni kama kioo cha kuuonesha utamaduni wa jamii fulani. Kwa hivyo, Kiswahili kinauonesha na kuutangaza utamaduni wetu katika pembe mbalimbali za dunia.
Waandishi wengi wa Kiswahili wa riwaya, mashairi na tamthiliya wanachomoza katika nchi zetu, hususan miongoni mwa vijana, wake kwa waume. Na hapa ningependa kuzipongeza tuzo zinazotolewa kuwashajiisha waandishi, hasa chipukizi, wazidi kuwa na ujasiri wa kuandika. Tuzo kama ile Tuzo ya Kiswahili ya Safal Cornell ya Fasihi ya Kiafrika au ile Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu iliyoasisiwa mwaka jana.
Tumeshuhudia pia maendeleo katika uchapishaji wa tafsiri za Kiswahili za riwaya zilizoandikwa kwa lugha za kigeni. Kwa mfano, tafsiri ya kitabu cha Paulo Coelho cha The Alchemist (Mkemia) ya ndugu yetu Ali Attas aliyezungumza mwaka jana kwa video katika hafla hii au ile tafsiri ya kitabu cha Abdulrazak Gurnah cha Paradise (Peponi), kilichofasiriwa na Dkt. Ida Hadjivayanis, ambaye wiki iliyopita alikuwa New York alikotoa hotuba kwenye shughuli nyingine ya Siku ya Kiswahili Duniani ilioyoandaliwa katika Umoja wa Mataifa.
Tafsiri hizo za vitabu vya lugha za kigeni zinachangia katika kukitanua Kiswahili kifikra. Nasema hivi kwa sababu lugha zote hazifikiri namna moja: hutafautiana katika miundo yao. Sasa kuweza kuihaulisha miundo hiyo ya kifikra kutoka lugha za kigeni na kuifikisha katika lugha ya Kiswahili ni kuutanua upeo wa kifikra wa Kiswahili. Kiswahili kinaweza kikazidi kukolea utamu kwa kuona jinsi lugha nyingine zinavyotumia tamathali mbalimbali za usemi (tashbihi, tashihisi, istiara, jazanda na kadhalika).
Mwenyezi Mungu ametupa waja wake uwezo wa kujieleza kwa matamshi na kauli. Qur’ani inasema: “Khalaqal insaan 3allamahul bayaan”. [Tumemuumba mwanadamu na tukamfunza kauli, namna ya kusema kwa ufasaha]. Viumbe vengine havitufikii. Wanyama, kwa mfano, ingawa wana njia zao za mawasiliano lakini njia hizo hazina sifa zilizo nazo lugha za wanaadamu.
Kwa hakika, wataalamu wa lugha/isimu kina Noam Chomsky na Joseph Greenberg wanakubaliana kwamba lugha zote za wanaadamu zina mshabaha fulani. Kuna misingi fulani inayozifanya lugha zote duniani zishabihiane hata kama hazihusiani kihistoria.
Lakini juu ya kuwako mshabaha huo, kuna lugha nyingi duniani. Na sisi Waislamu tunaambiwa katika Qur’ani kwamba tafauti hizo za lugha ni miongoni mwa alama (aya) za uumbaji wake Mwenyezi Mungu:
“Miongoni mwa ishara (alama/aya) zake ni kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na tafauti za lugha na rangi zenu. Hizi hakika ni ishara kwa wale wenye kujua [yaani wenye kutambua]”.
[Wa min ayatihi khalqul samawaati wal ardhi waakhtilaaful alsinatikum waalwaanikum inna fi dhaalika la ayaati lil3alaamin.]
Lugha ni chombo kinachotegemea kiwango cha utamaduni wa wasemaji wa lugha hiyo. Lugha huzaliwa, hukua na hufa pia. Na hapo ndipo penye khofu. Tusipotahadhari tutajikuta hatuna lugha.
Ukweli ni kwamba tumeporwa vingi — ardhi, sharafu yetu, mamlaka yetu na sasa tunaona majaribio ya nguvu ya kutaka kutupokonya lugha yetu na hata kuuingilia utamaduni wetu.
Miaka ya hivi karibuni kumekuwako na mabadiliko makubwa ya wakaazi katika sehemu za Uswahilini. Ninachokusudia ni kwamba kumekuwako na mabadiliko ya kidemografia
ambayo yameathiri kwa kiwango kikubwa lugha ya Kiswahili. Nisifahamike vibaya; nisifahamike kwamba ninapinga uhamiaji wa watu ajinabi katika jamii zetu za Waswahili. Hasha. Kila panapokuwako mchanganyiko wa watu na mila, jamii yenyeji hunufaika kwa mchanganyiko huo maalum.
Na siwezi pia kupinga kwa sababu uhalisia wa mambo ni kwamba katika mfumo wa demokrasia lazima patakuwako na uhamiaji wa aina hiyo. Demokrasia na demografia huenda sambamba.
Lakini tunapaswa tuwe waangalifu, tusiruhusu lugha yetu ikachafuliwa. Wale ambao kwa vile tu wanaisema na wanaisema zaidi ya kuweza kuombea maji, wasitushurutishe tuisarifu lugha yetu watakavyo wao. Kwa vile mamlaka ya utawala hayamo mikononi mwetu, yamo mikononi mwao, wanayatumia madaraka yao kutudumaza hata katika utumiaji wa lugha yetu.
Mwananadharia wa Kitaliana, Antonio Gramsci, ameielezea vizuri hali hii anapochambua jinsi wenye madaraka, katika jamii yoyote ile, wanavyoyatumia madaraka yao kuhodhi mambo katika uwanja wa fikra na utamaduni. Huwa hawatumii nguvu lakini huwafanya wasio na madaraka waridhie wenyewe wanayofanyiwa.
Wanaweza kufanya hivyo kwa sababu ndio waliokithiri katika usomeshaji vyuo vikuu, ndio wenye kutunga mitaala, ndio wenye kumiliki vyombo vya habari, ndio wenye kusimamia matangazo ya biashara na ndio hata wenye kuhodhi mijadala ya kisiasa.
Yote hayo yangekuwa si kitu lau wangekuwa na ari na lugha hii; lau wangekuwa na uchungu nayo.
Makosa makubwa hutokea katika tafsiri. Tafsiri ni sanaa. Mtu anahitaji awe na ustadi maalum ili aweze kuwa hodari wa kufasiri. Tunapofasiri tunahitajika kufasiri maana ya sentensi nzima, kwa mfano, na si kufasiri neno kwa neno. Ni kuihaulisha maana ya lugha moja na kuipeleka kwenye maana ya lugha nyingine. Kwa bahati mbaya, kufasiri neno kwa neno kumekuwa mtindo siku hizi kwa wale wenye kufasiri kutoka Kiingereza.
Tunaziona hata tovuti za mashirika makubwa ya utangazaji yakichapisha makala yenye kukirihisha kwa jinsi yanavyokiponda Kiswahili. Mashirika haya yana uwezo wa kifedha wa kuwaajiri watu wa kuyapitia makala wanayochapisha. Lakini hayajali. Wanaona yote ni sawa madhali ukurasa umejaa. Japokuwa umejaa utumbo. Tena usiowiva; unaoweza kukutapisha au hata kukuharisha.
Najua kuna nadharia mbalimbali za tafsiri kama sanaa; na nadharia hizo zinaweza zikaingizwa katika mifumo ya kiitikadi za siasa, lakini kuhusika na tafsiri kuna mambo ambayo lazima tuyaseme bila ya hata kuzizingatia nadharia hizo.
Kwenye tafsiri ndipo Kiswahili kinavyobadilishwa umbo na kuvishwa nguo zisizokistiri. Hapo ndipo tunapoisoma au kuisikia miundo ya kigeni ya sentensi za Kiswahili. Miundo ya ajabu ajabu. Wakulaumiwa tunawajua. Ni wale wenye kusema wakasikilizwa (“influencers” Waingerea huwaita). Miongoni mwao ni wahariri wa magazeti; wa tovuti; na wa vyombo vingine vya habari. Ni wanasiasa na wenye kusimamia matangazo ya biashara.
Mifano iko mingi, tena mingi sana. Nitaitaja michache tu:
Siku hizi wagonjwa wakipelekwa hospitali huwa hawatibiwi tena bali huwa “wanapokea matibabu” (tafsiri ya neno kwa neno ya “receive treatment”).
Wanasiasa nao huwa hawaelezi tena mambo waziwazi au paruwanja au kinagaubaga bali huwa “wanafunguka” (tafsiri ya “open up”).
Sijui kama mnajua lakini siku hizi upishi una kazi kwa sababu hakuna tena mafuta ya kupikia. Yaliyopo ni mafuta ya kula (tafsiri ya “edible oil”). Balaa kubwa hili.
Watu si tena wanane lakini wanakuwa watu nane. Bei rahisi au ya nafuu imegeuzwa na kuwa “bei rafiki”. Au huwa bei poa “cool”. Hata wakati nao huwa “si rafiki” unapokuwa “hauruhusu”. Huu ni mfano wa istiari iliyochakaa (cliché) — hata katika Kiingereza “cliches” zinakemewa kutumiwa katika maandishi mazuri.
Haidhuru jinsi kadha wa kadha sasa inakuwa “haijalishi” jinsi kadha wa kadha.
Na harufu au herufi ya “h” imekosa nini? Nauliza kwa sababu siku hizi inakatwa kabisa katika maandishi. Huko kunakuwa “uko”; hivi kunakuwa “ivi”; na hapa kunakuwa “apa”. “Gh” na “kh” zimekatwa zamani kwa sababu watu fulani hawawezi kuzitamka na sasa tumebakishiwa “gorofa,” (badala ya ghorofa), “muktasari” (badala ya mukhtasari au muhtasari) na “ruksa” (badala ya rukhsa au ruhusa).
Na kuna kitu siku hizi kinachoitwa “lisaa” (badala ya saa).
Hakuna neno linalofasiriwa vibaya kama lile la Kiingereza “produce”. Siku hizi hufanya kazi za ajabu ajabu.
Mchele, kwa mfano, siku hizi “unazalishwa” badala ya mpunga kuvunwa; ng’ombe hawakamwi tena ila maziwa “yanazalishwa”, umeme umeacha kufuliwa siku hizi “unazalishwa” na hata skuli hazielimishi watoto bali “huzalisha” wahitimu. Siku hizi pia mtu akifariki mauti hayamkuti bali hukutwa na “umauti”.
Siku hizi hatuna tena mwanamme bali tuna “mwanaume”, ingawa bado sijasikia “mwanauke”. Dada amekuwa “mdada” na dada zetu wamekuwa “wadada”. Hicho si Kiswahili. Inasikitisha sana kwamba baadhi yetu tumekuwa tukisema hivyo pia bila ya kujali.
Nadhani kuna sababu mbili kuu zinazochangia kuzuka kwa mchafukoge huu katika lugha yetu: uvivu na kutokujua. Tunasononeka. Ni muhimu kwamba mabaraza yanayohusika na Kiswahili pamoja na wizara za elimu, ziwe na mkakati wa pamoja wa kusimamia lugha yetu inavyotumiwa. Vyombo vya habari navyo vinahitaji kuajiri watu wenye uwezo na ujuzi wa lugha hii. La sivyo tutaikuta hii lugha tunayoitukuza leo ikiwa na umbo jengine. Au hata ikafa.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com ; Twitter: @ahmedrajab
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.